Gabon yamleta Thierry kisa Stars

GABON wameanza kuweweseka kuelekea mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya timu ya soka ya Kenya, Harambee Stars, itakayopigwa baadaye mwezi huu.

Timu hiyo kutoka magharibi mwa Afrika itawakaribisha Harambee Stars inayofundishwa na Engin Firat Novemba 15 mjini Franceville kwenye ngarambe za Kundi F.

Kulikua na utata hususan kuhusu usalama wa kikosi cha Harambee Stars kuelekea mechi hii ikizingatiwa mwishoni mwa Agosti mwaka huu, wanajeshi nchini Gabon walipindua Serikali ya Rais Ali Bongo.

Lakini ukimya wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) unaamanisha wameridhika na utulivu wa hali ya siasa nchini humo ambapo Jenerali Brice Oligui Nguema aliyeongoza mapinduzi hayo ameapishwa Kaimu Rais.

Na ndani ya uongozi Shirikisho la Soka Gabon (FEGAFOOT), hawajafurahishwa na utendaji kazi wa kocha mkuu wa timu ya taifa raia wa Ufaransa, Patrice Neveu, hususan kushindwa kuipeleka timu hiyo michuano ya Kombe la Afrika itakayofanyika mwakani nchini Ivory Coast hivyo kuchukua maamuzi magumu ya kumtimua.

Neveu alikumbana na shoka hilo wakati akianda kikosi chake kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Guinea iliyopigwa jijini Lisbon nchini Ureno mwezi uliyopita kujiweka sawa kabla ya kuwavaa Harambee Stars.

Nafasi ya kocha huyo Mfaransa imechukuliwa na mchezaji wa zamani wa Gabon, Thierry Mouyouma, atakayesaidiana na wachezaji wengine wa kimataifa kutoka taifa hilo, Daniel Cousin, Eric Mouloungui na Cedric Moubamba.

“Kutokana na matokeo ya hivi karibuni ambayo Gabon imekua ikipata, Waziri wa Michezo, Rais wa FEGAFOOT na kocha mkuu wa timu ya taifa wamekubaliana kusitisha ushirikiano wote,” alisema Rais wa FEGAFOOT, Pierre-Alain Mounguengui.

Mechi ya kwanza ya kocha mpya Mouyouma ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Guinea katika siku ambayo pia Harambe Stars waliwalazimisha waliyokuwa wenyeji wa Kombe la Dunia 2018, Urusi, sare ya mabao 2-2 mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa Uturuki.

Kocha Mouyouma anamatumaini kikosi atakachokiteua kitarudisha makali yake dhidi ya Harambee Stars japo anakiri gemu itakua ngumu kutokana na kuimarika kwa Stars na kwamba hii ndiyo mara ya kwanza timu hizo zinakutana.

Kwenye viwango vya ubora wa soka vilivyotolewa mwezi uliyopita na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gabon ipo nafasi ya 86 wakati Kenya ikikamata nafasi ya 110.