FKF yapata bosi mpya, Mwenda nje
Muktasari:
- Hussein amechaguliwa kuwa rais mpya wa Shirikisho la Kenya (FKF), katika uchaguzi uliofanyika leo jijini Nairobi
MWENYEKITI msaidizi wa timu ya Murang’a Seal na mkurugenzi wa kampuni ya Extreme Sports, Hussein Mohamed ameshinda urais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), akimwaga bosi wa muda mrefu wa shirikisho hilo, Nick Mwenda.
Wajumbe 90 wanaowakilisha matawi ya kaunti ya FKF, klabu za Ligi Kuu, Ligi ya Taifa (NSL), Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL) na Chama cha Ustawi wa Wanasoka Kenya (Kefwa) walipiga kura kuchagua viongozi ambao wataliongoza soka la Kenya kwa miaka minne ijayo.
Mohammed alipata kura 42 kutoka kwa wajumbe kwenye uchaguzi huo uliofanyika katika viwanja vya ndani vya Moi Kasarani jijini Nairobi.
Amechaguliwa pamoja na mgombea mwenza wake nyota wa zamani wa Inter Milan ya Italia na timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars), Mc Donald Mariga ambaye anatazamiwa kushika nafasi ya makamu wa rais.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, Doris Petra na mgombea mwenza Mwenda ambaye ni rais wa FKF aliyemaliza muda wake waliibuka washindi wa pili kwa kupata kura 31.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa M
mkurugenzi wa FKF aliyejiuzulu, Barry Otieno aliyepata kura 10 kifuatiwa na Cleophas Shimanyula kwa kura nne.
Kufuatia matokeo hayo Hussein anatazamiwa kuchukua nafasi ya Mwenda ambaye alidumu katika shirikisho hilo kwa miaka tisa tangu 2016.
Kwenye uchaguzi huo pia walichaguliwa wajumbe wa kamati kuu ya taifa (NEC) kutoka kanda nane ambapo Robert Macharia alishinda nafasi ya ujumbe Kanda ya Kati.
Wengine ni Charles Njoka (Kanda ya Mashariki), Peter Kamau Kasskas (Bonde la Ufa), Mohammed Dabar (Kaskazini Mashariki), Daniel Shikanda (Nairobi Mashariki), Collins Kalele (Nyanza), Caleb Amwayi (Magharibi) na Gabriel Mughendi Kanda ya Pwani.