Fimbo FKF yaichapa Mathare United

MASAIBU bado yanazidi kuiandama Mathare United kufuatia Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kupitia Idara ya Uadilifu kuwasimamisha wachezaji wawili tegemeo kutokana na madai ya kuhusika katika upangaji wa matokeo.

Wachezaji waliyokumbana na rungu la FKF ni beki wa kati Lennox Ogutu na kiungo mkongwe Alphonce Ndonye.

Katika barua ambayo FKF ilimwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Mathare United, Jeckton Obure, ilisema uchunguzi umeshaanza kuhusu hao wawili.

“FKF imepokea ripoti zinazodai wachezaji hao wawili wamehusika katika upangaji matokeo, hivyo kufungua uchunguzi kuhusu madai hayo,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya FKF kwenda kwa bosi wa Mathare United.

Mathare United haijakua na matokeo mazuri msimu huu ambapo kabla mechi ya jana dhidi ya vibonde wenzao Ligi Kuu Kenya, Vihiga Bullets, walikua wanaburuza mkia wakiwa na pointi nne tu.

Mabingwa hao wa zamani FKFPL wiki iliyopita walipeana mkono wa kwaheri na kocha Boniface Omondi na kumteua Samuel Koko kukaimu nafasi hiyo.