FIFA YAIHANDA INGWE KISA MADENI KIBAO

Saturday May 29 2021
fifa pic
By Mwandishi Wetu

AFC Leopards imeshikwa pabaya tena na FIFA manzee. Unamkumbuka yule kocha wao mzungu Marko Vasilvejic waliyemtimua Februario, 2019? Ndiye sasa kawaingiza Ingwe kwenye ngori mbaya na FIFA imetishia kuwashusha daraja kama tu ilivyofanya na Zoo Kericho.
Ipo hivi. Ingwe ilimchuja kazi kocha huyo Mserbia baada ya mechi 10 tu kufuatia msururu wa matokeo mabaya.
Jamaa akawasilisha kesi mbele ya kamati ya kinidhamu ya FIFA alikoishtaki Ingwe kwa kumchuja wera bila ya kufuata utaratibu unaofaaa.
Baada ya kusikiza kesi hiyo kamati hiyo imewapa Ingwe siku 30 kuwa imemlipa fidia yake ya Sh450,000. Aidha FIFA imeipiga Ingwe faini ya Sh120,000.
"AFC Leopards wamepatikana na hatia ya kwenda kinyume na uamuzi wa jajdi wa Player's Status Commitee aliyoitoa Januari 12, 2021. AFC Leopards sasa wanaamrishwa kumlipa kocha Marko Vasiljevic USD3,400 kama fidia pamoja na riba ya asilimia 5% kuanzia Machi 11, 2019." sehemu ya barua kutoka kwa FIFA ilieleza. Kamati hiyo sasa imetishia kuifungia klabu kutofanya usajili wa wachezaji, kuwapokonya alama kwenye ligi kuu na hata kuwashusha daraja hadi ligi za nyasi endapo watakosa kumlipa kocha huyo ndani ya muda waliopewa.
Kocha huyo Mserbia alisimamia mechi 10 pekee kisha akafutwa. Kwenye mechi hizo 10, alishinda mbili pekee akatoka sare nne na kupoteza mara nne.
Ngori hii imewakuta Ingwe wakiwa wanahangaika kumfidia mchezaji Vincent Habamahoro aliyezawadia fidia ya Sh1.6 milioni baada ya kuishtaki klabu hiyo kwa kumtimua bila ya kufuata utaratibu.
Vile vile kocha wao mwingine wa zamani Andre Cassa Mbungo anayeifunza Bandari kwa sasa, aliwashtaki Ingwe akilalamikia kutolipwa mshahara wake wa miezi mitano. Ingwe waliamrishwa kumlipa Sh6 milioni.
Madeni haya yaliyolimbikizana  katika kipindi hiki cha janga la Covid-19 sasa yamewaweka pabaya wakijikuta wakihandwa na FIFA.

Advertisement