Faili la Mwendwa latua kwa DPP

MAHAKAMA inayoshughulikia kesi za ufisadi imempa kiongozi wa mashtaka (DPP) Noordin Haji mwezi mmoja kuwasilisha ushahidi dhidi ya Rais wa zamani wa FKF, Nick Mwendwa.
Haji alifungua faili mpya ya mashtaka dhidi ya Mwendwa anayedaiwa kupora zaidi ya Sh38 milioni  kutoka kwa hazina ya Shirikisho  FKF.
Hakimu Mkuu anayesikiza kesi hiyo Eunice Nyuttu sasa amempa siku 30 kuwasilisha ushahidi alionao dhidi ya  kesi inayomkabili Mwendwa aliyefurushwa mamlakani.
Akiwasilisha  afisi ya DPP, kiongozi mashtaka  Eveylne Onunga alimwambia Hakimu Nyuttu kwamba afisi yao bado hajapitisha ushahidi wote walionao kwa upande wa mshtakiwa ili timu yake iweze kuipitia na hivyo kuomba siku 30 kutekeleza hilo.
Wakili wa Mwendwa, Charle Njenga, Victor Omwemba na Silvia Matasi walihakiki mbele ya hakimu kuwa ni kweli wamepokea sehemu ndogo tu ya ushahidi utakaotumiwa dhidi ya mteja wao.
"Nitakubali ombi la DPPP na kwa maana hiyo kesi hii itasikizwa tena Januari 24, 2022," Hakimu Nyuttu aliamuru.
Mwendwa anakabiliwa na kesi nne za uvujaji wa fedha za serikali zilizotolewa kwa FKF chini ya uongozi wake.
Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohammed alitembeza bakora lake na kumpindua Mwendwa kwa kuteua Kamati Shikilizi ya FKF inayoongozwa na jaji mstaafu Aaron Ringera kuendesha soka nchini kwa kipindi cha miezi sita.