AWCL BADO KITENDAWILI

Thursday April 22 2021
awcl pic
By John Kimwere

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF) limesema bado halijapata mwenyeji wa mechi za Klabu Bingwa Afrika kwa soka la wanawake (AWCL). 

Uamuzi wa kuanzisha ngarambe hiyo uliafikiwa mwaka jana na makala ya kwanza ya kipute hicho yalitazamiwa kuandaliwa mwaka huu.
Michuano ya kipute hicho inapaswa kufanyika kati ya Oktoba na Desemba kila mwaka. Jumla ya timu saba zitafuzu kushiriki kinyang'anyiro hicho baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kanda kuwania tiketi ya kusonga mbele.
Taifa litakalopata nafasi ya kuandaa fainali hizo halitashiriki mechi za mchunjo. Shirikisho hilo lilitangaza habari hizo licha ya Shirikisho la Soka nchini Morocco (FRMF) kusema taifa hilo limeteuliwa kuwa mwandalizi wa kipute hicho.
Rais wa FRMF, Faouzi Lekjaa alisema hayo baada ya mkutano wa kikao cha Bunge jijini Rabat. Kupitia mtandao wa shirikisho hilo, rais huyo alisema "Morocco itaendelea na mipango ya kuandaa makala ya kwanza ya kipute cha Klabu Bingwa yatakayoandaa kuanzia Novemba mwaka huu."
Nalo shirikisho la Afrika liliandika ''Bado hatujateua taifa lolote kuwa mwenyeji wa ngarambe ya AWCL.''
Aprili 15 ndio tarehe iliyowekwa ya mwisho kuteua mwenyeji wa ngarambe hiyo. Kando na Morocco mataifa mengine yaliyotuma maombi ya kuteuliwa kuandaa michuano hiyo ni Afrika Kusini, Equatorial Guinea na Nigeria.

Advertisement