Aussems kupambana na hali yake

MAJANGA yanaiandama kikosi cha AFC Leopards ambacho leo Alhamisi kinashuka katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya FC Talanta ili kuendelea kuweka hai matumaini ya kurudia historia ya mwaka 1998.

Ndiyo! 1998 ilikuwa mara ya mwisho Ingwe inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya na kocha Patrick Aussems amedhamiria kurudisha furaha za ubingwa kwa mashabiki kindakindaki wa Leopards.

Japo Leopards bado ipo kwenye mbio za kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Kenya (FKF), ni taji la ubingwa wa FKFPL ambalo wengi wa mafans wao wanalitolea macho.

Wakiwa wamebakisha mechi 11 kabla ya kuhitimisha msimu wa 2022/23, Leopards wanahitajika kushinda mechi zao na kusubiri kuona nini kitakachotokea kwa timu zilizoko juu yao kwenye msimamo.

Hata hivyo, mtihani aliyonayo kocha Aussems ni namna atakavyowatumia wachezaji wake katika kila mechi ukizingatia miongoni mwa timu za FKFPL msimu huu, Ingwe ndicho chenye kikosi finyu.

Timu hiyo ilianza msimu kwa kupigwa STOP na FKF kutumia wachezaji waliowasajili na wakati huo huo walikuwa pia wakitumikia kibano kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Na licha ya FIFA mwishoni mwa mwezi uliopita kuwaondoa kifungoni, uongozi wa Leopards haukuingia sokoni hivyo kumlazimu Aussems kuendelea kuwaamini wachezaji ambao amekuwa nao na ambao wamekuwa wakimpa matokeo mazuri.

Leo katika Uwanja wa Nyayo, kocha huo raia wa Ubelgiji anakabiliwa na mtihani ya kuwakosa wachezaji wanne tegemeo akiwemo kipa namba moja Levis Opiyo ambaye alionyeshwa kadi ya njano gemu iliyopita dhidi ya Kenya Police FC na kumfanya kukusanya jumla ya kadi tano za njano msimu huu.

Kwa mujibu wa kanuni za FKFPL, kipa huyo atakosa mchezo unaofuata hivyo nafasi yake itachukuliwa na Maxwell Mulili.

“Opiyo alipata kadi ya tano ya njano na atakosa mechi dhidi ya Talanta na hivyo inakua tatizo kwasababu tunaye Maxwell pekee kwa gemu hii,” alisema Aussems ukizingatia Ingwe waliorodhesha majina ya makipa wawili tu.

Hii itakua ni gemu ya pili msimu huu kwa kipa huyo kinda kucheza kwani ndiye aliyekuwa mchumani na kuweka clean-sheet Ingwe ikitoka sare tasa na Kariobangi Sharks.

Wachezaji wengine ambao Aussems atawakosa kutokana na kuwa majeruhi ni mabeki Tedian Esilaba, Lewis Bandi na Kayci Odhiambo huku Washington Munene akiwa ni mgonjwa.

Leopards ilishinda mechi ya mzunguko wa kwanza mabao 6-0 lakini FC Talanta watataka kulipiza kisasi hususan baada ya kushinda mechi yao ya wikendi iliyopita mabao 2-0 dhidi ya Wazito.

Katika mechi nyingine leo, KCB waliyotoka sare tasa na Ulinzi Stars, watawakaribisha Vihiga Bullets iliyopata ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Mathare United gemu itakayopigwa Uwanja wa Police Sacco jijini Nairobi.

Nao Ulinzi Stars ambao hawajashinda katika mechi tano za mwisho FKFPL, watakuwa wageni wa Sofapaka katika mchezo wa mapema utakaopigwa uga wa Police Sacco.