Aussems: Ingwe bado sana ubingwa FKFPL

WANASEMA msema kweli ni mpenzi wa Mungu na kwa anayemfahamu kocha Patrick Aussems, huwa ni muwazi sana kwenye kutiririsha mawazo yake.
Kocha huyo wa AFC Leopards amekuwa na kikosi hicho kwa misimu miwili sasa akiwa anaingia wa tatu. Tangu alipoteuliwa, amefanikiwa kupevusha kiwango cha uchezaji cha kikosi hicho fauka ya changamoto kibao alizokumbana nazo kubwa ikiwa ni kulazimika kuunda kikosi kipya mara mbili.
Huku msimu mpya FKFPL 2022/23 ukiwa bado unasubiriwa, kocha huyo ambaye ameishia kuteka imani za mashabiki na uongozi wa timu, kawamwagia uchungu mkali.
Uongozi wa Ingwe na mashabiki wameonyesha imani kuwa huyu ndiye kocha mwenye uwezo wa kuwasaidia kutwaa taji lao la kwanza FKFPL ambalo mara ya mwisho kulibeba ilikuwa miaka 24.
Huku mabosi wa Ingwe na mashabiki wakitarajia Aussems atawasaidia kufanikisha hilo msimu huu, kocha huyo haoni jambo hilo likiwezekana na kuongeza kusema, Ingwe wategee tu kwani bado wapo mbali kiviwango.
“Wajua kikosi nilichonacho sasa nililazimika kukisuka upya kabisa mwanzoni mwa msimu uliopita baada ya wachezaji 16 kutukimbia. Kikosi hichi cha sasa, bado ni malimbukeni ila kwa sasa, angalau wana uzoefu wa msimu mmoja kwenye ushindani wa ligi kuu,” Aussems anafafanua.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji alisema kubwa wanaloweza kukifanya msimu mpya utakapoanza ni kufanya vyema zaidi ya msimu uliopita akisisitiza malengo ni kumaliza miongoni mwa tatu bora na kama ni mbaya sana basi top 4.
Msimu uliopita, Ingwe walimaliza katika nafasi ya sita kwa kukusanya pointi 45 baada ya kushinda mechi 11, kutoka sare 12 na kupoteza saba.