ASANTENI WADAU, ILIKUWA SAFARI POA!

Takribani miaka 13 tumekuwa wote katika kuhabarishana habari tofauti za michezo na burudani. Hakika tumekuwa na kipindi kizuri cha kukata kiu yako ya michezo na burudani.

Nikiwa kama msimamizi wa maudhui ya gazeti hili, najivunia kuongoza kwa takribani miaka mitano ya kuhakikisha wasomaji wetu wanakata kiu zao za michezo na burudani.

Katika kipindi hicho cha usimamizi na miaka mingine nyuma kama mhariri msaidizi wa gazeti hili, pamoja na timu nzima tumewafanya wasomaji wetu wapate habari za kina za mashinani na burudani kutoka ndani na nje ya Kenya.

Kuhakikisha wasomaji wanapata ladha pekee ya Mwanaspoti, kwa kuweka vichwa vya habari motomoto kwenye ukurasa wa mbele na hasa kwa ligi kubwa za soka ikiwamo Ligi Kuu England, Hispania, Italia, Ufaransa na Ujerumani. Pia Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) na habari nyingine za kuvutia za michezo mingine ikiwamo riadha na ndondi, kuogelea na raga na zile za burudani kutoka Tanzania zimewavutia wasomaji wengi.

Mashindano mbalimbali ya shule na mashinani, ngumi na riadha kutoka kwa waandishi wetu wenye uelewa mpana na michezo hiyo. Hakika tunajivunia watu hawa (Dominic Isiji, Abdulrahman Sheriff, Thomas Matiko, Arege Ruth 'Toto', Hamisi Ngowa, Hassan Pojjo, John Kimwere, Laurance Ongaro, Charles Ongadi, Fadhili Athumani, Pauline Ungaji, Osborne Manyengo na kwa upande wa picha ni Chris Omollo.

Nikiwa kama Mtanzania nimehariri habari za michezo za Kenya na kujifunza mengi kuhusu michezo ya Kenya hususani soka, riadha na ngumi ambayo imekuwa ikiandikwa kwa wingi katika matoleo ya Mwanaspoti na waandishi wetu hao.

Naamini kwa upande wa lugha wasomaji wetu wamefurahia kupata maneno mengi mapya hasa lugha ya michezo inayotumia maneno mengi zaidi ya mitaani lakini yenye kuvutia na kukupa burudani, hasa yale ya Misimu (yanayozuka na kupotea), yamelifanya gazeti hili kupendwa na wasomaji wake.

Mbali na michezo na burudani hasa za muziki na maigizo zilizoandikwa kwenye gazeti hili, pia kulikuwa na burudani ya Hadithi, nikiwa mmoja wa watunzi wa hadithi hizo, tumewafikia wasomaji wetu na kuwa pamoja nasi kwa ufuatiliaji wao, pia hatukuwasahau warembo kwa kuwepo na kolamu ya Afya na Urembo ikiandikwa mwanadada Pauline Ungaji.

Nawashukuru wadau wote wa shule, mashinani na wa michezo yote kwa jumla kwa kuwa karibu na mwanaspoti kwani tuliwafikia huko waliko na kusoma matoleo yenye habari zao na nyinginezo.

Pia wauzaji wa magazeti likiwamo Mwanspoti walipata wasaa wa kutoa maoni yao kwenye ukurasa wa 'Venda Wetu' kila Alhamisi na walieleza kile wasomaji wetu wanapenda na nini kiongezwe au kipunguzwe na hakika tulifanya kila njia kuhakikisha wasomaji wanaridhika na kile wanachotaka.


NAFURAHI KUFANYA KAZI NANYI ASANTENI


Hassan Kajia

Mratibu wa Maudhui

Mwanaspoti Kenya


Wasemavyo waandishi wa Mwanaspoti


ABDULRAHMAN SHERIFF

NINGALI nakumbuka siku ya Jumamosi Machi 5, 2011 tukiwa na wakuu Nation Media Group (NMG) na wale wa Mwananchi Communication Limited (MCL) kutoka Dar es Salaam, Tanzania ambapo gazeti hili la MWANASPOTI lilianza kusambazwa katika sehemu mbalimbali Kanda ya Pwani.

Siku hiyo husika itabakia kuwa ya kihistoria katika umri wangu wote kwani ni siku ambayo nilitambua kuwa wadau wa michezo na burudani, wachezaji, wasanii na mashabiki kumbe walikuwa wana hamu ya kuwa na jarida lenye habari hizo.

Nakumbuka vyema namna MWANASPOTI lilivyopokelewa vizuri na uzinduzi wake ulifana chini ya aliyekuwa Meya wa Mombasa, Ahmed Muhdhar, akisaidiana na aliyekuwa mwanasoka wa timu ya taifa Ahmed Breik ambaye aliaga dunia Desemba 11 mwaka huu baada ya kuugua kwa kipindi kirefu.

MWANASPOTI liliendelea kupata umaarufu na baada ya kuuzwa Kanda ya Pwani ambapo nakumbuka kuna wakati idadi ya mauzo ilipanda hadi nakala 14,000 kwa kila toleo, likaenezwa kote nchini ambapo lilipokewa vizuri.

Kuna mengi ambayo sitaweza kuyataja hapa ambayo yalinifanikisha kutokana na kuwa mwandishi wa jarida hili lakini niruhusu niwaeleze matukio mawili ambayo yatabaki kwenye kumbukumbu yangu daima dawamu.

Nakumbuka kwa miaka miwili mfululizo kabla ya kuingia kwa mwaka 2020, nimewahi kushinda tuzo la Mwandishi Bora wa spoti katika Kanda ya Pwani.

Tukio lingine ambalo sitalisahau ni kuwa kutokana na umaarufu wa MWANASPOTI niliweza kufanikiwa kuwasaidia mayatima wawili wa Kaunti ya Taita Taveta walioshinda mbio za riadha katika Uwanja wa Dawson Mwanyumba mjini Wundanyi kupata udhamini wa masomo na mafunzo ya mchezo huo. 

Wasichana hao wawili, Agnes Mwashigadi na mdogo wake Maria Shali, walihitajika na shirika moja lisilokuwa la kiserikali baada ya kushinda mbio walizoshiriki, lakini wakapata kipingamizi ambacho nashukuru niliweza kukitatua.

Nina furaha kuwa mwaka huu, Agnes amemaliza masomo yake ya kidato cha nne wakati Maria amefanya mtihani wa daraja la nane. Nina imani wataendelea kuongeza talanta za mchezo huo na pia kuchukulia masomo kwa umuhimu wake.

Inanibidi niwashukuru waandishi wenzangu tuliyoanza tangu toleo la kwanza nao ni kina Thomas Matiko, Charles Ongadi, Hassan Pojjo, Hamisi Ngowa na John Kimwere kwa jinsi tulivyoshirikiana kwa kipindi chote.

Pia sina budi kumpa ahsante nyingi kiongozi wetu Isiji Dominic kwa uongozi bora na wa busara ambao nahisi ulisaidia gazeti hili kuzidi kunawiri.

Kwa uhakika nimefanya kazi katika gazeti hili kwa bidii na nashukuru kwa kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wakubwa zangu walioko Mombasa na huko Dar es Salaam, Tanzania.

Ninawashukuriu waandishi wenzangu wote ambao tumekuwa tukishirikiana kikamilifu kulifanya MWANASPOTI litambe siku za Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.



HASSAN POJJO

TANGU toleo la kwanza la gazeti la MWANASPOTI lilipoanza kujitokeza nchini Kenya, wapenda michezo na hususan wasomaji wa majarida ya lugha ya Kiswahili walifarijika kwa kiasi kikubwa mno.

Ujio wa MWANASPOTI ulifanya kiwango cha wapenda michezo mashinani kuongezeka maradufu ikizingatiwa kwamba wengi waliokuwa wakilisoma walifarijika kuona timu zao za mashinani ndani ya gazeti hili tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Tangu niwe mwandishi wa gazeti la MWANASPOTI, nimejiona nikiongeza maarifa yangu ya uandishi wa michezo na burudani na hakika limekuwa gazeti pendwa mashinani kutokana na kuwa linapenya kila kona.

Pia MWANASPOTI limepata sifa na kusifiwa sehemu za mashinani kwani limekuwa likiangazia ile michezo ambayo ilikuwa inaelekea kusahaulika katika jamii.

Zaidi ya yote gazeti hili linatumia lugha tamu ya kimichezo ambayo imekuwa ikiwavutia wasomaji pamoja na muonekano wake wenye mvuto.

MWANASPOTI limefanya vijana wengi kutambua talanta zao kupitia taarifa zao kuangaziwa mara kwa mara na hili nadiriki kusema mimi mwenyewe ni shahidi nikiwa mwandishi kutoka Kaunti ya Mombasa na eneo nzima la Kanda ya Pwani.

Ni dhahiri gazeti la MWANASPOTI limekuwa lenye manufaa mengi na makubwa kwa sekta ya michezo nchini.



JOHN KIMWERE

SAFARI ya kulitumikia gazeti la MWANASPOTI Kenya ambalo huchapisha kwa kina habari tendeti za michezo mbalimbali, imekua ya fahari na kujivunia kwa upande wangu nikiwa moja wa waandishi waanzilishi humu nchini.

Ujio wa MWANASPOTI hapa nchini ulifungua ukurasa wa kuchapishwa kwa habari za michezo hususan timu za mashinani ambazo kwa muda mrefu havikuwa vinapata nafasi kuangaziwa.

Aidha MWANASPOTI ilisukuma wachezaji wengi mashinani kuanza kujituma zaidi wakijuafika habari zao zitapata fursa kuchapishwa na jarida hili.

Hapa Kenya hakuna gazeti la Kiswahili ambalo huchapishwa habari za michezo kwa kina isipokuwa MWANASPOTI.

Bila kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa itakuwa vigumu kwa wasomaji wa MWANASPOTI kukubali na kuamini gazeti hili litatoweka sokoni.

MWANASPOTI limekuwa likichapisha makala ya burudani ikiwemo muziki na uigizaji na kufanikiwa kuibua wasanii wapya kutokana na kuangazia taarifa zao.

Ufanisi wa MWANASPOTI umechangiwa pakubwa na mchango wa waandishi na wahiriri wote kwa jumla.

Katika mpango mzima, sina shaka kutaja kuwa itakuwa giza totoro kwa wasomaji wa gazeti la MWANASPOTI katika maeneo ya Pwani, Magharibi mwa Kenya, Nairobi pamoja na maeneo ya Mkoa wa Kati.

Gazeti la MWANASPOTI limechangia wanahabari wengi kutangamana na wanamichezo wakiwamo wachezaji, makocha, maofisa wa viwango tofauti vya vikosi vya spoti.

Ni maamuzi magumu yaliyochukuliwa kusitisha uchapishaji wa gazeti hili lakini kinachotia moyo imekua safari ya furaha kutangamana na wasomaji wetu.



CHARLES ONGADI

WAKATI gazeti la MWANASPOTI lilipoingia sokoni jijini Mombasa kwa mara ya kwanza mwaka 2011, nilibahatika kuwa kati ya waandishi wa kwanza kupewa fursa kuandikia gazeti hili mahusisi kwa habari za michezo na burudani.

Ilikuwa hivi; chini ya uongozi wa mwanahabari mkongwe Abdulrahman Sheriff na wenzangu kama Kazungu Samuel, Hassan Pojjo na Hamisi Ngowa, tuliweza kuangazia kwa mapana na marefu habari za michezo za mashinani ambazo kwa muda mrefu hazikuwa zikiangaziwa kipindi hicho.

Kikosi hiki cha nguvu kilihakikisha habari na makala za michezo Mombasa na Pwani kwa ujumla zinaangaziwa kwa ustadi mkubwa.

Kupitia gazeti hili, wanamichezo wengi mashinani walifurahi kuona habari na picha zao zikiangaziwa na kujikuta wakiwa wapenzi wakubwa wa gazeti hili.

Mara baada ya kupata umaarufu, gazeti la MWANASPOTI lilisambazwa katika kila kona ya nchi na kuzidi kutia fora kwa habari za mashinani, kitaifa na kimataifa.

Na hata gazeti lililopanua mbawa zake hadi maeneo mengine nchini, lilikuwa tayari lina sifa zinazohitajika kwa gazeti la michezo na burudani.

Licha ya kupitia changamoto za hapa kule, nilihakikisha ninafanya kila niwezalo kupata habari motomoto nikilenga kuboresha gazeti la MWANASPOTI kupitia makala na habari.

Ni masikitiko makubwa kwa wanamichezo kote nchini na hususan wateja wetu walioko maeneo mbalimbali ya nchi kwamba watalikosa gazeti hili wakati ndipo wanaanza kuifurahikia.



THOMAS MATIKO

KWAHERI huwa sio neno salamu ila tulipofikia hizi ndizo salamu na hatuna budi kuikumbatia tukiamini pia ni salamu ya heri.

Imekuwa ni safari ya kufana sana kuwa miongoni mwa waandishi waasisi wa MWANASPOTI toleo la Kenya.

Hakika imekuwa ni fursa ya kipekee, kusema kweli nitakuwa mtovu wa nidhamu nisipotoa shukrani zangu za dhati kwa bosi Ndaya Kasongo aliyenipa fursa kwenye MWANASPOTI

Kwa miaka 10 tumelikuza gazeti kutoka kuwa gazeti la kipekee la michezo la Kiswahili lakini pia la burudani. Najivunia sana kuwa mwasisi wa makala ya burudani kwenye MWANASPOTI.

Imekuwa furaha yangu kuwaleteeni habari za michezo na burudani na kwa hilo nasema asante sana.




ISIJI DOMINIC

KWA siku 4,683 ambazo ni wastani wa miaka 12, Mwanaspoti Kenya limekua gazeti la kipekee na hakika la aina yake kutokana na uwasilishwaji wake wa taarifa za michezo na burudani.

Hii ni safari ambayo tumetembea kwa pamoja na wasomaji wetu na chochote walichohitaji au kutaka kukifahamu kwa undani, tulijitahidi kadri ya uwezo wetu kulifanyia utafiti na kuwaletea ili kutimiza kauli yetu mbiu ‘Kata Kiu ya Michezo na Burudani’.

Upekee wa Mwanaspoti unatokana na taarifa nyingi kuandikwa kwa lugha adhimu ya Kiswahili na wakati mwingine kutumia lugha ya vijana kufikisha ujumbe.

Riadha ni moja ya michezo ambayo imeipatia sifa kedekede taifa letu la Kenya na kupitia Mwanaspoti, tumekua tukiangazia kwa kina mashindano mbalimbali maarufu ndani na nje ya nchi ambayo wanariadha wetu wamekuwa wakitamba ikiwemo kuvunja rekodi za dunia.

Hili limekua gazeti ambalo nimefarijika kulitumikia kwa takribani miaka miwili tukichambua kwa pamoja mashindano maarufu ya riadha duniani, Ligi Kuu Kenya, raga na pia kupata taarifa za ndani zinazohusu mchezaji kupitia safu ya ‘Alibamba’.

Safari ya Mwanaspoti Kenya inachukua nukta na tunawaambia wasomaji wetu ‘Asanteni na Kwaherini, japo napenda kuamini haya ni mapumziko tu, yajayo huenda yakafurahisha zaidi.




HAMISI NGOWA

IMEKUWA safari ndefu tangu kuanzishwa kwa gazeti la Mwanaspoti nchini Kenya.

Japo mwanzoni kulikuwa na changamoto za kusaka wasomaji lakini hatimaye lilikuwa moja ya magazeti yaliyopendwa zaidi nchini kutokana na jinsi lilivyoangazia habari tofauti za michezo na burudani hususan zile za mashinani.

Binafsi nikiwa mmoja miongoni mwa kikosi cha waandishi wa gazeti hili, nimejifunza mengi katika tasnia ya uandishi wa michezo na burudani kupitia gazeti hili kinyume na yale niliyokuwa nikiyajua.

Gazeti hili pia limeniwezesha kutangamana na watu tofauti wakiwemo wachezaji na viongozi mbalimbali wa timu.

Aidha lilinipa fursa ya kuangazia michezo ya mashinani ambapo kupitia baadhi ya taarifa nilizoandika wapo wachezaji waliokuwa wamekataa tamaa ya kuendelea kusakata soka kwasababu tofauti walibadili maamuzi na kurudi tena viwanjani.

Kwangu ni masikitiko makubwa kusitishwa uchapishaji wa gazeti hili la Mwanaspoti ukizingatia limekua mkombozi wa michezo na hususan michuano mbalimbali mashindani ambayo imeshuhudia washindi wakitunukiwa zawadi za fedha.

Mwisho nawashukuru wakuu wangu wote kwa ushirikiano wao katika kujenga hadhi ya gazeti la Mwanaspoti na kulifanya miongoni mwa magazeti pendwa zaidi nchini Kenya.



LAWRENCE ONGARO

KWA zaidi ya miaka 10 ambapo gazeti la MWANASPOTI Kenya limekua sokoni, limeweza kuleta mchango mkubwa kwenye sekta ya michezo na burudani.

Wakati mwingi unapotaja jina MWANASPOTI, kila mwanamichezo anajihi anauhakika wa kupata taarifa za kina ikiwemo uchambuzi thabiti inayohusu michezo kuanzia mashinani, kitaifa hadi kimataifa.

Nikiwa mwandishi wa muda mrefu wa MWANASPOTI nikiripoti kutoka Kanda ya Kati hususan Mlima Kenya, maeneo kama Nyeri, Murang’a, Thika, Kiambu, Ruiru na Gatundu, nadiriki kusema hili ndilo lilikua gazeti pendwa kwa wanamichezo.

Ni gazeti ambalo wasomaji wake walikua hawalikosi kila linapotoka mara tatu kwa wiki wakifurahia kuona timu zao zimeangaziwa.

Hawakufurahia tu kusoma habari kuhusu timu zao mbali pia walikua wanajifunza lugha tamu ya kispoti ambayo ilitiririka kwa ufasaha mkubwa.

Timu ambazo viwango vyao vya soka vimebadilika baada ya taarifa zao kuandikwa kwenye MWANASPOTI ni Marafiki, Rware, Police (zote kutoka Kaunti ya Nyeri), Kandara FC, Mung’aria (zote z Kaunti ya Murang’a), Sunveat, Landless na Karia (zote za Kaunti ya Kiambu) na timu hizi zilikua zinakipiga Ligi Kanda ya Kati.

Maofisa waliojitolea kikamilifu kuchapa kazi vilivyo mashinani huku utendaji kazi wao ukichangiwa pakubwa kupitia MWANASPOTI ni Paul Gathirwa ambaye ni katibu mpanga ratiba wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) Tawi la Thika pamoja na Mwenyekiti wa FKF Kanda ya Mlima Kenya, Gordon Chege, na Mwenyekiti wa Marefa Kaunti Ndogo ya Ruiru, Simon Kariuki.

Gazeti la MWANASPOTI Kenya hata kama linasitisha uchapishaji wake, bado litazidi kuenziwa na wengi kwasababu mchango wake wa miaka mingi umekuza michezo na vipaji kibao wakati huo huo likitoa darasa lugha ya kispoti pasipo kubagua umri, jinsia, kabila wala dini.



TOTO AREGE

NINAPOANDIKA ujumbe huu wa kuaga gazeti la MWANASPOTI Kenya, moyoni mwangu nahisi uzito huku nikikumbuka nilivyoshiriki pamoja na kila mmoja wenu kuanzia wahariri, waandishi wenzangu na hata wasomaji wetu.

Safari ya MWANASPOTI Kenya inahitimishwa leo ila tunajivunia kuwaletea wasomaji wetu habari za michezo kutoka mashinani hadi kimataifa na kimataifa huku tukiweka paruwanja mafanikio na changamoto za wanamichezo.

Nachukua fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa msaada na urafiki niliyopokea tangu nijiunga na familia ya MWANASPOTI mwezi Novemba mwaka 2021 nikiwa mwandishi pekee wa kike. Najaribu kumanisha nini?

Fani ya uandishi wa habari na hususan michezo na burudani ipo wazi kwa jinsia zote na mimi kufanya kazi MWANASPOTI Kenya ni udhibitisho wanawake wanaweza kufanikiwa katika tasnia hii.

Ingawa ninasikitika kwamba gazeti hili halitakuwepo tena, nina imani mahusiano niliyoyajenga na maarifa niliyoyapata yataendelea kuniongoza katika jitihada zangu za baadaye.

Asanteni kwa kumbukumbu, kicheko na uzoefu usioweza kupimika. Urafiki niliyojenga na mafunzo niliyopata yatabaki daima kuwa na nafasi maalumu moyoni mwangu.

Kwa wanahabari wenzangu wa michezo, najua tutaonana mara kwa mara katika majukwaa mengine ila, nawatakia kila la heri katika jitihada zenu za baadaye. Kwaheri.

Kwa wasomaji wetu, napenda kwa heshima kuwashukuru nyote kwa upendo wenu mkubwa mliyoonyesha kuhakikisha mnapata nakala ya MWANASPOTI kila Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.

Mlikuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha gazeti la MWANASPOTI linakuwa miongoni mwa magazeti ambayo yamepata umaarufu mkubwa humu nchini.

Safari yangu imejaa furaha na mafanikio kutokana na uungwaji wenu mkono. Sina maneno ya kutosha kuelezea shukrani yangu kwenu.

ADIOS...!