Vihiga bado ipo

Vihiga bado ipo

KOCHA Juma Abdalla alipokabidhiwa mikoba kuinoa Vihiga Bullets, timu hiyo ilikua mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu Kenya lakini sasa zikiwa zimesalia mechi nane msimu kumalizika, ndoto ya timu hiyo kubaki kwenye ligi bado ipo hai.

Ushindi wa mechi mbili mfululizo dhidi ya Mathare United umeifanya Vihiga Bullets kupanda hadi nafasi ya 16 kabla ya mchezo wa jana kati ya Wazito FC dhidi ya AFC Leopards.

Timu inayomaliza katika nafasi ya 16 inacheza ‘playoff’ na timu itakayoshika nafasi ya tatu kwenye National Super League (NSL) ili kupata nafasi moja iliyosalia kucheza FKF-PL msimu unaofuata.

Abdalla aliyemrithi Evans Mafuta aliweka imani timu hiyo haitarudi kucheza NSL baada ya msimu moja tu wa kupanda kucheza FKF-PL.

Novemba mwaka jana akiteuliwa kuwa kocha wa Vihiga Bullets, Abdalla alinukuliwa akisema timu yake ikipata angalau ushindi katika mechi saba, wataepuka panga la kushuka daraja.

Hadi sasa, Vihiga Bullets wameshinda mechi tano dhidi ya Wazito FC, Talanta FC, mara mbili wakiwapiga Mathare United na ushindi wa mezani kufuatia vurugu zilizosababishwa na mashabiki wa Gor Mahia.

“Lengo langu ni kupata matokeo mazuri kwa kushinda angalau mechi saba ili msimu ujao tuendele kucheza FKF-PL,” alisema Abdalla.

Wakati Vihiga Bullets wakiendelea kuweka hai matumaini yao kubaki FKF-PL, hali ni ngumu kwa Mathare United ambapo kocha John Kamau amesema inachangiwa na ukata na kudokeza walilazimika kufanya mazoezi mara moja kwa wiki kabla ya kuwavaa vijana wa Abdalla.

Kocha Kamau alisema anajivunia wachezaji wake ambao wanapambana uwanjani licha ya hali ngumu wanayopitia.