Homeboyz presha tu inapanda inashuka

Homeboyz presha tu inapanda inashuka

POINTI nane ndizo zinazozitenganisha vinara wa Ligi Kuu Kenya, Kakamega Homeboyz, na mabingwa watetezi, Tusker FC, baada ya kila timu zikiwa zimecheza mechi 26 na zimesalia mechi nane msimu kumalizika.

Homeboyz ambao wanasaka taji lao la kwanza FKF-PL msimu huu, walipoteza nafasi ya kutanua wigo na Tusker FC baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Sofapaka wikendi iliyopita mchezo ukipigwa Uwanja wa Bukhungu kaunti ya Kakamega.

Ndani ya wiki moja, Homeboyz inayofundishwa na Bernard Mwalala imevuna pointi mbili wakati wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Tusker FC, wakijikusanyia pointi nne.

Sare ya bao 1-1 waliyopata dhidi ya Sofapaka ilikuwa ni sare ya pili mfululizo ambayo sasa inawapa presha katika azma yao kutwa ubingwa wa kwanza FKF-PL. Hata hivyo ahueni kwa Homeboyz waliyo kileleni ni kuwa wakishinda mechi zao zote nane zilizobakia, watachukua ubingwa.

Kocha wa Homeboyz Mwalala ambaye amekuwa akiwatahadharisha wachezaji na mashabiki kuanza kusherehekea mapema, amesema kila mchezo waliyobakisha ni sawa na fainali.

Nusura Homeboyz wapoteze mchezo wa tatu msimu huu na wa pili wakiwa nyumbani lakini shukurani za pekee zimwende kipa Godfrey Oputi aliyepangua mkwaju wa penalti ya kiungo Hansel Ochieng dakika ya 76 timu hizo zikiwa 1-1.

Wakati Homeboyz wanadondosha pointi mbili, Tusker FC walikua na Pasaka njema wakiwafunga Gor Mahia mabao 2-1 mchezo uliochezwa Uwanja wa William Ole Ntimama katika kaunti ya Narok.

Ushindi huo unawafanya Tusker FC kujiimarisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa FKF-PL wakiwa na pointi 46 huku Gor Mahia wakiwa na pointi 42.

Kocha wa Tusker FC, Robert ‘Simba’ Matano, ambaye hakufurahishwa na refa Anthony Ogwayo timu hizo mbili zilipokutana Aprili 9 mwaka huu, amemiminia sifa refa Zachariah Ashira aliyechezesha mechi yao ya marudio dhidi ya Gor Mahia wikendi iliyopita.

“Mechi ilichezeshwa vizuri sio kwa sababu nimeshinda lakini referee alichezesha kwa haki. Hatuna malalamiko yoyote na sidhani Gor Mahia nao pia wanayomalalamiko. Refa alikuja kutimiza wajibu wake kikamilifu, hakusumbuliwa na mtu yeyote na alifanya kazi yake vizuri na kwa haki,” alisema Matano.

Naye kocha wa Gor Mahia, Andreas Spier, alitoa kauli ya kukata tamaa mbio za ubingwa msimu na badala yake kusema anatengeneza timu ya ushindani tayari kwa msimu ujao.

“Nimekuwa nikisema mara kwa mara, sisi ni timu inayokarabatiwa, tumewaleta wachezaji chipukizi na tunajaribu kusuka timu nzuri kwa ajili ya msimu ujao,” alisema.