Yao Kouassi apewa mchongo mpya

BAADA ya kupata majeraha ya nyama za nyuma ya paja,  beki wa kushoto wa Yanga Kouassi Attohoula Yao amepewa akili nini anatakiwa kufanya ili arejee uwanjani mapema.

Yao ambaye aliumia nyama za paja kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam ambao Yanga ilifungwa mabao 2-1, amekuwa nje kwa muda na ataukosa mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Mamelodi Sundowns, Jumamosi wiki hii.

Daktari za zamani Yanga, Shecky Mngazija amesema mchezaji aliyepata majeraha ya aina hiyo kwanza hana muda maalumu wa kurudi kwa sababu inategemea na ukubwa wa jeraha.

"Ukubwa wa jeraha ndio utaamua kwamba anakaa nje muda gani, lakini jambo kubwa zaidi ili arudi mapema uwanjani inatakiwa afuate masharti. Kawaida 'hamstring' (nyama za nyuma ya paja) ni msuli uliopo kwenye paja ambao kama ukiumia halafu ukawa hupumziki, basi unakuwa kwenye hatari ya kuugua kwa muda mrefu," amesema Dk Mngazija

"Pia mchezaji hatakiwi kula vyakula vitakavyomsababishia uzito zaidi kwa sababu itamchelewesha kupona. Inatakiwa ale vyakula vyenye vitamini kwa wingi na protini kidogo.

"Kwa hiyo kimsingi ukitulia, ukipata lishe nzuri na matibabu mazuri unaweza kupona haraka ingawa siwezi kusema inachukua muda gani kwa sababu kuna vitu vingine vinavyosababisha urudi mapema kama umri. Mchezaji mwenye umri mkubwa huwa anachelewa kupona ukilinganisha na mwenye umri mdogo."

Mngazija amesema kama vitu hivyo vyote vitafuatwa, basi mchezaji aliyeumia majeraha ya aina hiyo anaweza kurudi mapema uwanjani.

Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya The Institute of Sport Exercise & Health (ISEH), majeraha ya aina hiyo yapo ya aina tatu.

Kuna madogo ambapo mtu akiumia inaweza kumchukua wiki moja hadi mbili kupona, pia yale makubwa hukuchukua kati ya wiki mbili hadi sita.