Yanga yashindwa kwenda kambini Moro

Muktasari:
- Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alifichua ishu ya kufa kwa kambi hiyo, lakini asubuhi ya leo baadhi ya nyota wake waliendeleza mgomo baridi wa kukacha mazoezi licha ya ahadi mambo kwao sasa ni shwari.
Dar es Salaam.Hali bado si shwari Yanga baada ya leo jioni kushindwa kwenda Morogoro kambini kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, lakini safari hiyo ikafa ghafla baada ya Clement Sanga kujiuzulu.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alifichua ishu ya kufa kwa kambi hiyo, lakini asubuhi ya leo baadhi ya nyota wake waliendeleza mgomo baridi wa kukacha mazoezi licha ya ahadi mambo kwao sasa ni shwari.
Nyota sita wa kikosi cha kwanza walikosa mazoezi yaliyofanyika Chuo cha Polisi Kurasini, akiwamo Hassan Kessy aliyeshiriki kikao na mabosi wa Usajili juzi ili kuweka mambo sawa na wachezaji kuahidi kumaliza mgomo baridi.
Wengine waliokosekana kwenye mazoezi hayo yaliyofanyika kati ya Saa 3 asubuhi mpaka saa 6 mchana ni Kelvin Yondani, Haji Mwinyi, Benno Kakolanya, Andrew Vincent 'Dante' na Ibrahim Ajibu.
Hata hivyo Kessy alikiri ni kweli alienda katika kikao cha juzi, lakini kilichompeleka ni kumaliza shida zangu baada ya kumaliza mkataba na Yanga.
"Akili yangu haikuwa katika kikao nilitaka mambo yangu na Yanga yamalize na hata kilichozungumzwa jana hata sikumbuka maana akili yangu haikuwa hapo kabisa na sitakwenda mazoezini mpaka jambo langu la mkataba mpya litakapokamilika," alisema Kessy, huku Meneja wa Yanga Hafidh Saleh alifafanua kwa kusemaDante, Kessy, Benno na Yondani wanaogopa kufika mazoezini wasije wakaumia wakati hawana mikataba japo wapo kwenye mazungumzo ya kupewa mikataba mipya.
"Ajibu na Mwinyi hawa wanaumwa na wamepewa ruhusa ya kujiuguza na watakapokuwa kamili watarudi kuungana na wenzao mazoezini," alisema Saleh.
Katika mazoezi hayo ya jana chini ya Kocha Mwinyi Zahera alionekana kama aliyekamia kwa kuwapigisha kisawasawa waliojitokeza kwa kuwagawa wachezaji katika makundi tofauti yasiyopungua matano na kila kundi akitaka likimbie kuzunguka uwanja ndani ya dakika tano.
Amissi Tambwe na Mrisho Ngassa waliokuwa kundi tofauti walionekana kushindwa kwa kuachwa nyuma na wenzao, huku Papy Tshishimbi na Emmanuel Martin wakionekana fiti kinoma.
Kocha Zahera baadaye aligawa timu mbili tofauti na kucheza mechi huku akitaka kila timu itumie mbinu nyingi kufunga na kushambulia kwa haraka ikitumia pasi ndefu na fupi.
Kikosi cha kwanza kilikuwa na Ramadhani Kabwili, Said Makapu, Juma Abdul, Tshishimbi, Raphael Daud, Yohana Mkomola, Martin na Godfrey Mwashuiya na ndicho kilichoibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya kikosi cha kina Youthe Rostand, Abdallah Shaibu 'Ninja' Pato Ngonyani, Said Mussa, Pius Buswita, Juma Mahadhi, Deus Kaseke, Ngassa na Herieter Makambo.