Yanga yafanya uamuzi mgumu

Kipa wa Yanga Deo Munishi 'Dida'
Muktasari:
Barthez tangu asajiliwe Yanga hakuwahi kusimama langoni kucheza mechi za kimataifa kwani walikuwa wakimtumia Dida na Juma Kaseja aliyesitisha mkataba na Yang
BENCHI la Ufundi la Yanga limefanya uamuzi mgumu baada ya kutangaza kwamba kipa namba moja wa timu hiyo, Deo Munishi ‘Dida’ ambaye amerejea mazoezini atakaa benchi na Ally Mustapha ‘Barthez’ ndiye atakayesimama langoni kwenye mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Jumamosi dhidi ya BDF XI ya Botswana.
Barthez tangu asajiliwe Yanga hakuwahi kusimama langoni kucheza mechi za kimataifa kwani walikuwa wakimtumia Dida na Juma Kaseja aliyesitisha mkataba na Yanga.
Kipa huyo akiwa Simba kabla ya kutua Yanga aliwahi kudaka mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Elan Club ya Comoro nyumbani na ugenini ambapo Simba ilisonga mbele kwa ushindi mabao 4-2 na kukumbana na TP Mazembe ambapo licha ya Simba kutolewa lakini ndiyo mchezo uliomuuza Patrick Ochan na Mbwana Samatta.
Kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali alisema wamefurahi kuona Dida amerudi kuungana na wenzake, lakini kwa sasa Barthez ndiye namba moja na atakuwa langoni katika mchezo huo wala hawana wasiwasi.
Pondamali alisema kwa sasa kila mmoja ndani ya timu hiyo anafurahia kazi safi inayofanywa na Barthez ambaye amekuwa akifanya vyema katika mechi za Ligi Kuu Bara ambazo ndiyo zimempatia nafasi ya kudaka katika mechi hiyo.
“Tutampa nafasi Barthez hilo halina mjadala, tunafurahi kuona Dida amerudi ni mchezaji mzuri, lakini kutokana na uwezo wa Barthez sasa hakuna ubishi kwamba ndiye atakayekuwa na kazi ya kulinda lango,” alisema Pondamali.
“Wakati nakuja hapa Yanga nilikuta makipa wote hawa uwezo wao mdogo, lakini niliwapa mafunzo ambayo kwa sasa hakuna utakayeweza kumuona hana uwezo, kila mmoja yuko sawa hata huyu Alfonce (Matogolo) naye atakuwa kama kaka zake.”
Naye nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amewaaminisha Wanayanga kwamba mambo yatakuwa mazuri.
Cannavaro alisema endapo washambuliaji wao wakiongozwa na Kpah Sherman, Amissi Tambwe, Simon Msuva na Mrisho Ngassa watafanya kazi yao kwa kupata mabao matatu, ushindi huo utakuwa mtaji mkubwa ambao utaisadia Yanga katika mchezo wa marudiano.
Alisema huku katika ulinzi hana wasiwasi anajua nini anatakiwa kukifanya kuwakumbusha wenzake Kelvin Yondani aliyepona tayari kwa mchezo huo pamoja na Mbuyu Twite na Oscar Joshua ambao watajipanga kutofanya makosa yoyote.
“Hata ikitokea tumepata bao moja haraka tunatakiwa kuacha kushangilia sana kanakwamba mechi tumemaliza turudi kati haraka kutamani la pili na baadaye la tatu na mengine, tutakapopata ushindi wa mabao matatu na kuendelea hapa nyumbani sina wasiwasi kwamba tutawatoa,” alisema Cannavaro.
“Tuna timu imara na makocha wanaojua, hapa tunatakiwa kuthibitisha ubora wetu, kama unakumbuka katika msimu uliopita kama tungeshinda kwa idadi kubwa ya mabao hayo nyumbani tungeweza kuwatoa Al Ahly kule kwao, lakini kitendo cha kupata bao moja hapa, kule tukawapa urahisi wenzetu.”