Yanga yabeba mwingine, Ni Mzambia anayejua kutupia

Muktasari:

YANGA haijamaliza Ligi Kuu Bara, lakini hesabu zao tayari ziko msimu ujao na juzi jioni imechukua beki wa maana pale jijini Kinshasa anayewaumiza kichwa Simba na leo hii wanajiandaa kubeba straika wa maana pale Sauzi kutoka klabu ya Kaizer Chiefs.

YANGA haijamaliza Ligi Kuu Bara, lakini hesabu zao tayari ziko msimu ujao na juzi jioni imechukua beki wa maana pale jijini Kinshasa anayewaumiza kichwa Simba na leo hii wanajiandaa kubeba straika wa maana pale Sauzi kutoka klabu ya Kaizer Chiefs.

Kaizer Chiefs ndio waliyoing’oa Simba kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuishindilia mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza kisha kukubali kichapo cha 3-0 ugenini jijini Dar es Salaam na yenyewe kusonga kwa jumla ya mabao 4-3.

Anayefanya vurugu hiyo ya anga kwa anga ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said ambaye anafanya vurugu za kimataifa akisomba mastaa wakubwa akizna na Djuma Shaaban aliyemsainisha mkataba wa miaka miwili.

Mwanaspoti, linafahamu leo Hersi atakuwa yupo nchini Afrika Kusini na atakutana na bosi mkuu wa Kaizer maarufu kama Amakhosi Bobby Kaizer ili kukamilisha dili la kumchukua Straika Lazarous Kambole.

Kambole amekuwa akikosa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza cha Amakhosi na ametaka kuondoka akihofia ubora wa straika Mserbia, Samir Nurkovic aliyeitungua Simba kwa mabao mawili kwenye mchezo wa kwanza kule Sauzi, ambaye amekuwa ndio chaguo la kwanza katika kikosi hicho.

Mabosi wa Yanga wakiongozwa na Mshauri wa Ufundi, Senzo Mazingisa akishirikiana na Hersi ndio wamemaliza dili hilo la kupewa Kambole ambaye ni mmoja kati ya mastraika bora kutoka Zambia.

Yanga itamchukua Kambole kwa mkopo kutokana na urafiki wao huo na Kaizer ambapo hakuna shaka kwamba mshambuliaji huyo atavaa jezi za njano na kijani msimu ujao.

Mapema wiki hii Mwanaspoti lilitoa orodha ya washambuliaji watano ambao wanatakiwa kati yao hao wawili wasajiliwe na haraka Hersi ametua Afrika Kusini kumalizana na Kambole ambaye alikuwemo kwenye orodha hiyo.

Orodha hiyo pia iliwahusisha mastraika, Fiston Mayele, Dark Kabangu, Magbi Gbagbo na Jean-Marc Makusu Mundele.

Msimu huu haukuwa msimu mzuri wa Kambole ndani ya Amakosi na hali hiyo imemchefua na kutaka kuondoka akishtuliwa na uamuzi wa kocha wake wa timu ya taifa ya Zambia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ aliyeamua kumuacha kwa mara ya kwanza Chipolochipolo.


DJUMA FRESHI

Yanga imeamua kuhamia kwa Kambole, baada ya kufanikiwa kumalizana na beki Mkongomani Djuma Shaaban aliyepo AS Vita.

Usajili wa Djuma, aliye nahodha wa Vita umekamilishwa juzi jioni jijini Kinshasa kwa kusainishwa wa miaka miwili kwa dau lililobaki kuwa siri baina ya pande hizo mbili, licha ya kuenezwa ni la dau ndefu.

Hii inakuwa ni safari ya tatu kwa Hersi, DR Congo kukamilisha usajili wa mastaa wapya wa Yanga, kwani mapema msimu huu alitua jijini hapo kuwasainisha winga Tuisila Kisinda kutoka Union Maniema na nahodha msaidizi na kiungo Mukoko Tonombe kuiongezea Yanga makali.

Djuma anakuwa mchezaji wa kwanza wa Yanga kusajiliwa kuelekea msimu ujao akisaini mkataba wa miaka miwili na Yanga na kwamba mbali na kumalizana na beki huyo wa kupanda nma kushuka na nayejua kufunga, pia Hersi amemalizana na klabu yake ya FC Renaissance du Congo iliyomtoa kwa mkopo AS Vita.