Yanga Noma

Muktasari:
Ndani ya mechi 17 ilizocheza msimu huu, Yanga imefanikiwa kuvunja mwiko wa kutoshinda kwenye viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro na Mkwakwani, Tanga. Kwa misimu mitatu Yanga haikuwahi kushinda kwenye viwanja hivyo zaidi ya kuambulia vipigo au sare.
ANGALIA rekodi hizi za Yanga msimu huu halafu utagundua kwanini jamaa wameingia Tanga na mikwara mizito. Yanga ndiyo timu pekee kwenye Ligi Kuu Bara iliyoshinda mechi 10 ambazo hazijafikiwa na klabu nyingine yoyote ingawa Azam imejaribu kuwasogelea kwa kushinda mara tisa.
Ndani ya mechi 17 ilizocheza msimu huu, Yanga imefanikiwa kuvunja mwiko wa kutoshinda kwenye viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro na Mkwakwani, Tanga. Kwa misimu mitatu Yanga haikuwahi kushinda kwenye viwanja hivyo zaidi ya kuambulia vipigo au sare.
Yanga iliwapiga Polisi Morogoro bao 1-0 kabla ya kuiangamiza Coastal Union kwa bao 1-0. Kiongozi wa Wachezaji wa Yanga uwanjani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ameangalia rekodi hizo pamoja na mzuka wa wachezaji wenzake akawahakikishia mashabiki kwamba leo Jumamosi Mgambo JKT wanalala hakuna cha Fully Maganga wala Malimi Busungu.
Wachezaji hao wawili wamekuwa na kiburi baada ya kufanikiwa kuzinyanyasa klabu nyingi kwenye uwanja huo zikiwamo Yanga na Simba.
“Kama tuliweza kuuvunja mwiko kwa Coastal Union, hatuoni vipi tushindwe kwa Mgambo,” alisema Cannavaro ambaye ndiye aliyefunga bao la kufutia machozi la Yanga dhidi ya Mgambo katika ligi ya msimu uliopita ambapo Yanga ilicharazwa mabao 2-1 katika pambano lililiochezwa Machi 30, 2014.
“Hata Jamhuri Morogoro tulikuwa hatujashinda kwa muda mrefu, lakini msimu huu tumevunja rekodi hiyo na siku sote historia zipo kwa ajili ya kuvunjwa, hatuna hofu yoyote,” alisema Cannavaro kwa kujiamini huku kiungo aliye katika ubora wa hali ya juu kwa sasa, Salum Telela akisisitiza wanapiga mtu.
“Tunataka pointi tatu, ili kuzidi kujikita kileleni. Tutapambana na Mungu atatusaidia,” alisema Telela mchezaji huyo kiraka.
Naye beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua alisema wameenda Tanga kwa kazi moja kushinda. “Tumekuja kusaka ushindi, tunaamini tuna kikosi bora na lengo letu ni kuona tunarejesha ubingwa Jangwani,” alisema Oscar.
Aliongeza ni kweli wanapaswa kuingia Mkwakwani kwa tahadhari ikizingatiwa wenzao wa Simba wametoka kujeruhiwa, lakini akabeza kwa kusema Yanga hailingani na klabu yote kwa sasa nchini. Yanga inaingia kwenye uwanja huo ambao Simba iliambulia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Mgambo.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema: “Kule hatutaweza kucheza soka la pasi fupi fupi kama tulivyozoea kucheza hapa Dar es Salaam, tutacheza pasi ndefu na soka la kasi ili kuhakikisha tunapata matokeo.
“Tunakwenda kusaka ushindi kwa hali na mali ili kuhakikisha kuwa tunajiweka pazuri katika mbio za ubingwa.” aliongeza kocha huyo wa zamani wa Chelsea ya Ghana.
Pluijm amekiri kuwa kukosekana kwa Mbrazili Andrey Coutinho kumefanya baadhi ya mipango yake kufeli kwani timu yake imelazimika kupandisha mashambulizi yake kupitia upande mmoja.
Mabingwa hao wa mara 24 wa ligi kuu, awamu hii wanakwenda na matumaini kibao ambapo wachezaji watano walioukosa mchezo wa Kagera Sugar Jumatano iliyopita wanatarajia kurejea kikosini na kuongoza ari ya ushindi. Nyota hao ni pamoja na nahodha Cannavaro aliyekuwa majeruhi na Haruna Niyonzima aliyekuwa anatumikia adhabu.
Coutinho anasumbuliwa na goti lakini Pluijm amepanga kumtumia Hussein Javu ama Kpah Sherman.
Pluijm aliongeza: “Nakumbuka vizuri kipigo cha mabao 2-1 msimu uliopita, nafahamu pia ugumu wa uwanja wa Mkwakwani, itabidi tupunguze ufundi na kucheza soka la pasi ndefu.
“Najua kukosekana kwa Coutinho kumezuia kidogo mipango yetu ya kupandisha mashambulizi kupitia pembeni, lakini nitaangalia kati ya Hussein Javu ama Sherman nani atakuwa katika kiwango bora kuziba nafasi hiyo,” alisema
Kocha wa Mgambo, Bakari Shime alisema: “Yanga wasiicheke Simba kwa kilichowapata hapa, tumepania pia kupata ushindi dhidi yao, Yanga ni timu kubwa kwa jina lakini wachezaji wake ni wa viwango vya kawaida kama wa timu nyingine tu.”