Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga New Force

Wachezaji wa yanga wakishangilia ushindi wa penati jana baada ya kuifunga Simba na kutwaa ngao ya Hisani.

MICHAEL MOMBURI YANGA ilikuwa na nguvu mpya na ilianza na wachezaji watano wapya katika kikosi chake dhidi ya Simba katika mchezo wa Ngao ya Hisani jijini Dar es Salaam jana Jumatano. Simba ambayo ilikubali kipigo cha penalti 3-1, iliingia uwanjani na wachezaji wake wa zamani, kabla ya kuwaingiza wapya kipindi cha pili. Yanga new force! Ndio kauli waliyokuwa wakitamka mashabiki wa Yanga baada ya kushinda mchezo huo. Kauli hiyo ililenga nguvu mpya iliyoonyeshwa na wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga ambao ndiyo walichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa timu hiyo na uongozi kuahidi zawadi ya shilingi milioni 31 kama pongezi kwa wachezaji hiyo ikimaanisha kila mchezaji atalamba shilingi milioni moja. Lakini kama hiyo haitoshi Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisisitiza kuwa mambo ndio yameanza na wameingia na nguvu mpya ambayo ameahidi mashabiki wategemee mambo makubwa kwenye Ligi Kuu Bara inayoanza Jumamosi. Timu hizo zilikwenda kwenye penalti baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana huku zikishambuliana kwa zamu na kuonyesha soka la kuvutia, huku Simba ikitawala zaidi kipindi cha kwanza na kucheza soka maridadi. Penalti za Simba zilipigwa na Emmanuel Okwi, Uhuru Suleiman na Amri Kiemba ambao walikosa kwa kipa kupangua na kutoka nje huku Mohammed Banka akifunga moja. Yanga iliyotumia Waghana wote wanne kwenye kikosi cha kwanza, Mghana Ernest Boakye alikosa penalti yake ya kwanza huku nyingine zikifungwa na wachezaji Godfrey Bonny, Stephano Mwasika na Issack Boakye ambaye ndiye aliyemaliza kazi licha ya mashabiki wa Simba kumkejeli kuwa amezeeka kutokana na kushindwa kwenda na kasi ya Okwi na Mussa Mgosi. Ushindi huo wa Yanga umefanya historia ya Februari 17, 2001 kujirudia kufuatia wakati huo Yanga kuiliza Simba 2-1 kwenye mechi ya Ngao ya Hisani zilizokutana kwa mara ya mwisho katika mchezo kama huo. Washambuliaji wa pande zote mbili Okwi na Mgosi wa Simba pamoja na Kenneth Asamoah na Nsa Job wa Yanga walionyesha udhaifu kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi. Mgosi alipata nafasi ya wazi dakika ya tatu tangu kuanza kwa mchezo lakini akazidiwa ujanja na Nadir Cannavaro ambaye alimtuliza na kuurudisha mpira kwa kipa Yaw Berko ambaye hakuamini ushujaa alioonyesha kwenye penalti tano tano. Dakika ya tano Nsa alimtoka Joseph Owino lakini akachonga krosi ambayo Asamoah aliyeshindwa kung'ara katika mchezo huo, aliomba radhi baada ya kuuchelewa kuunganisha mpira huo. Kadri mchezo ulivyokuwa ukiendelea presha zilizidi kuwazonga makocha Patrick Phiri na Kosta Papic ambao wote walivaa suti nyeusi kwani hakuna aliyekaa kwenye kiti muda wote wa dakika 90, lakini tukio ambalo lilichekesha wengi ni dakika ya 15 wakati Mgosi alipompiga chenga Nsajigwa mpaka akaenda chini. Ukuta wa Simba chini ya Juma Nyoso na Owino ulidhibiti vilivyo makombora ya Yanga ingawa hakukuwa na uelewano baina ya mabeki wa Yanga, Nadir Cannavaro na Isaack Boakye na mara kadhaa walionekana kuchanganyana kimaamuzi hasa walipopigwa presha na wapinzani wao. Washambuliaji wa Yanga walipigiwa krosi safi zaidi ya tatu ambazo pengine zilikuwa zimalize mchezo lakini wakashindwa kufurukuta katika mchezo huo ambao kipa Ally Mustapha 'Barthez' hakuwa na lawama kutokana na kuziba vilivyo pengo la Juma Kaseja ndani ya dakika 90. Kipindi cha pili kilikuwa na mashambulizi ya kushtukiza ambapo Mgosi na Okwi walioongoza kwa kukosa mabao ya wazi, jambo ambalo lilimfanya Phiri kila mara ashike kichwa kwa mshangao. Phiri alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Jerry Santo, Nico Nyagawa na Mussa Mgosi na nafasi zao kuchukuliwa na Amri Kiemba, Shija Mkina na Patrick Ochan ambao waliongeza uhai lakini hakukuwa na aliyeweza kuleta matunda ndani ya dakika 90. Papic aliwatoa Asamoah, Shadrack Nsajigwa, Athuman Idd na Abdi Kassim na kuwaingiza Fred Mbuna, Godfrey Bonny, Jerry Tegete na Yahya Tumbo ambaye shuti lake la kwanza dakika ya 77 lilipenya mita chache pembeni ya mlingoti huku mashabiki wa Yanga wakishangilia kwa kudhani ni bao. Nsa Job angefunga bao dakika ya tisini baada ya kuwatoka mabeki wa Simba, lakini shuti lake ambalo lilikuwa linasubiriwa na Yahaya Tumbo liliokolewa na Haruna Shamte. Kocha Papic alisema timu yake haikuonyesha kiwango alichoahidi kwa mashabiki wa Yanga ingawa ilishinda mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa unaobeba mashabiki 60,000 ambao hata hivyo haukujaa. "Timu imecheza vizuri dakika 45 za mwanzo zilizofuata haikucheza vizuri, kiujumla ni kwamba haikuonyesha soka ambayo nilitegemea kuona, ilicheza kiwango cha chini ingawa mwisho wa siku ushindi ni ushindi." "Nilitegemea kiwango cha juu zaidi na kumaliza mchezo ndani ya muda wa kawaida lakini ikawa kinyume, hii ina maana tuna kazi kubwa ya kufanya hasa kwenye mbinu za mchezo katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inaanza Jumamosi." Phiri alisema: "Yanga imecheza vizuri ni timu imara imeonyesha ukomavu ndani ya dakika zote, sisi hatukuwa tumejiandaa kikamilifu kwa penalti na hata hivyo inapofika kwenye penalti huwezi kumlaumu kipa ile ni pata potea." Kocha Msaidizi wa Simba Suleiman Matola alilaumu wachezaji; "Wamefanya uzembe kwenye kupiga penalti tumeshindwa kushinda, tugange yajayo wala hiyo isiwatie presha Wanasimba. Itatusaidia kuelewa udhaifu wetu ili tujipange kutetea ubingwa wetu."