Waziri Mkuu kuongoza NBC Dodoma Marathon 2023
Muktasari:
- Fedha hizo zitasaidia kupambana na saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wakunga ikiwa ni sehemu ya kusaidia kuongeza wataalamu ili kupunguza vifo vya uzazi.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za NBC Dodoma Marathon 2023 zinazotarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu zenye lengo la kukusanya Sh500 milioni.
Fedha hizo zitasaidia kupambana na saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wakunga ikiwa ni sehemu ya kusaidia kuongeza wataalamu ili kupunguza vifo vya uzazi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mkoa umejipanga vyema kuwapokea wakimbiaji na wageni wote wataoshiriki.
“Tunaishukuru Benki ya NBC kwa kuandaa mbio hizi zenye faida kubwa kwetu kama nchi. Pili niwahakikishie washiriki wote kuwa mkoa wa Dodoma tumejipanga vyema kuwahudumia na kuwafanya wafurahie ujio wao pamoja na ushiriki katika mbio za mwaka huu,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi amesema mbio za mwaka huu pamoja na kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, zitasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wanaosomea taaluma ya ukunga ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.