Wakenya Majuu: Olunga, Wanyama nomaree!

WAKATI Kenya ikijiandaa kurejea viwanjani, kikwazo kikiwa ni ripoti ya kamati maalum ya kuangalia njia nzuri ya kurejea viwanjani baada ya kusitishwa kisa ugonjwa wa corona, huko majuu unaambiwa wakenya wameendelea kuwakisha mbaya!

Kutokana na janga la Corona, Machi 16 mwaka huu, Serikali kupitia wizara ya Afya, ilipiga marufuku mikusanyiko yote, agizo ambalo pakubwa liliathiri sekta ya michezo, ambayo kuanzia hapo ilijikuta ikienda likizo ya lazima. Shirikisho zote za michezo zilizingatia agizo hilo.

Aprili 30, katika kutekeleza maagizo hayo, Shirikisho la soka nchini (FKF), ilifutilia mbali ligi zote, ikiwemo Ligi Kuu ya soka, ambapo mbali na kufuta msimu wa 2019/20 wa KPL, pia iliitawaza Gor Mahia, kuwa mabingwa huku Chemelil na SoNy Sugar zikishuka daraja.

Hata hivyo, wakati mashabiki wa soka wakiendelea kusubiri, huko majuu wakenya wanaopiga soka katika ligi mbalimbali duniani, wameendelea kuwasha moto, ambapo Straika wa Harambee Stars, Michael Olunga anacheka tu na nyavu za wajapani.

Michael Olunga
(Kashiwa Reysol)
Mpaka sasa ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu ya soka nchini Japan, maarufu J1 League. Nyota huyu wa zamani wa Gor Mahia, mpaka kufikia muda huu, amefunga mabao 14, katika michezo 13 aliyoingia dimbani, kuisakatia Kashiwa Reysol.

Bao lake hilo la 14, alilifikisha katika mechi kali iliyopigwa siku ya Jumamosi, ambapo timu yake iliangukia kichapo cha 3-2 nyumbani dhidi ya Kashima Antlers. Olunga, ambaye amewahi kuichezea Girona FC, alifungia timu yake mabao yote mawili kwenye mchezo huo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Tusker FC, Thika United, Djurgardens IF na Guizhou Zhicheng, alifunga bao lake la kwanza kunako dakika ya 57, kabla Misao hajaisawazishia Antlers katika dakika ya 72. Bao la pili la Olunga, lilipatikana katika dakika ya 84.

Hata hivyo, kitumbua cha Kashiwa kilitiwa mchanga na Doi aliyeifungia Antlers, mabao mawili ya haraka, kabla ya mchezo kumalizika. Matokeo hayo yanaiacha Kashiwa Reysol, katika nafasi ya saba kwenye jedwali la ligi.

Eric Johanna Omondi
(Jonkopings Sodra)
Nchini Sweden, kiungo wa Harambee Stars na Jonkopings Sodra, Eric Johanna Omondi, alifunga bao lake la sita msimu huu, na kuisaidia klabu yake kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Trelleborg.

Omondi, aliitungaliza Sodra kunako dakika ya 10, kabla ya Kozia, kufunga la pili, zikiwa zimesalia dakika chache mpira umalizike. Ushindi huo, uliifanya Sodra kupanda katika nafasi ya tatu, kwenye jedwali la Ligi ya Superettan. Mechi inayofuata ni dhidi ya AFC Eskilstuna.

Katika ligi hiyo ya Allsvenskan, Joseph Okumu aliisaidia IF Elfsborg, kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Malmo FF, huku IF Vasalunds ya Anthony Wambani, ikiendeleza ubabe kwa kuitandika Haninge 4-2. Ochieng Ovella (IF Vasalund) na Eric ‘Marcelo’ Ouma (AIK) bado ni majeruhi.

Johanna Omolo
(Cercle Brugge)
Nchini Ubelgiji kwenye Ligi Kuu ya Jupiler, Kiungo wa Harambee Stars, Johanna Omolo, alikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Cercle Brugge, akicheza kwa dakika 90 zote, na kushuhudia klabu yake ikitandikwa 1-0 na Kortrijk.

Hata hivyo, Omolo alioneshwa kadi ya njano katika dakika ya 39 ya kipindi cha kwanza. Kipigo hicho kinaiacha Cercle Brugge, ambayo ni bingwa mtetezi, katika nafasi ya saba, wakiwa na pointi sita tu, baada ya kushuka dimbani mara nne.

Victor Wanyama
(Montreal Impact)
Baada ya kuondoka Ligi Kuu ya England akiwa hana nafasi kwenye kikosi cha Tottenham Hotspurs ya Jose Mourinho, huku akiwa amegandwa na majeraha ya mara kwa mara, kila mtu aliamini kuwa, nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama amechapa mbaya!

Safari yake ikamfikisha nchini Marekani, akaangukia katika mikono ya gwiji wa zamani wa Arsenal, Thiery Henry. Akatua pale Montreal Impact na bila kuchelewa, Mugubi akaanza kufanya kazi yake. Zaidi ya mara mbili, akiibuka mchezaji bora wa mechi.

Wikendi iliyopita, siku ya Jumamosi usiku, kwenye Ligi Kuu ya Marekani, maarufu Major Soccer League (MLS), kiungo huyu mkabaji alikuwa sehemu ya kikosi cha Montreal, kilichoangukia kichapo cha 1-0 mbele ya Toronto FC. Wanyama alicheza dakika zote 90 za mchezo huo.

Anthony Akumu
(Kaizer Chiefs)
Huko Afrika Kusini, beki Anthony Akumu kwa mara nyingine, alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha klabu ya Kaizer Chiefs, katika kampeni ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu, Absa Premier League. Mechi hiyo ilipigwa siku ya Jumamosi.

Katika mchezo huo, ambao ulishuhudia Chiefs, wakitandikwa 1-0 na Bidvest Wits, inayonolewa na kocha wa zamani wa Gor Mahia, Dylan Kerr. Kichapo hicho kinawaweka katika nafasi ya kwenye msimamo wa jedwali

Joash Onyango na Francis Kahata
(Simba SC)
Beki Kisiki Joash Onyango, aliyesajiliwa hivi karibuni na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania, Simba SC alikuwa sehemu ya kikosi cha wekundu wa msimbazi, kilichotwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii, jumapili hii.

Onyango, maarufu kama Berlin Wall, aliyesajiliwa akitokea Gor Mahia, alisimama kwenye safu ya me ya ulinzi ya Simba SC, sambamba na Shomary kapombe, Mohammed Hussein na Kennedy Juma, na kukamilisha ukuta mrefu wa ‘Berlin’

Hata hivyo, huku Onyango akifurahia kuisaidia Simba kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo, kwenye dimba hilo la Sheikh Amri Abeid (Arusha), mkenya mwenzake, Francis Kahata, ameendelea kukosekana kikosini akiuguza majeraha.

Cliff Nyakeya
(FC Masr)
Nchini Egypt, kwenye mechi ya ligi kuu, kiungo Cliff Nyakeya alicheza kwa dakika 74, timu yake ya FC Masr ikichapwa 2-1 na Wadi Degla, huku John Avire, yeye akiingia dimbani katika dakika ya 67, Tanta SC ilipochapwa 3-0 na Smouha.