Wachezaji, viongozi 13 Majimaji FC watimuliwa hotelini kisa deni
Muktasari:
- Hii ni tukio la pili kwa ndani ya wiki moja kwa timu kufukuzwa hotelini kwani Februari 17 Mkwawa Queens ya mjini Iringa inayoshiriki ligi kuu ya Wanawake nayo ilijikuta ikifukuzwa kwa deni la Sh 810,000.
Wakati Majimaji ikitarajia kushuka uwanjani leo kucheza dhidi ya Dar City katika mwendelezo wa first league, timu hiyo imewaangukia wadau ikiomba msaada ili kulipa deni katika hoteli waliyofikia na kuweza kusafiri kurudi mjini Songea.
Timu hiyo kongwe nchini iliyowahi kutesa ligi kuu kabla ya kushuka daraja misimu mitatu nyuma kwa sasa inashiriki first league na haijawa na matokeo mazuri ikiwa nafasi mbili za mwisho katika kundi A kwa pointi -10.
Bingwa huyo wa zamani wa kombe la Muungano (1999) imeelezwa kukwama Dar es Salaam baada ya kutimuliwa kwenye hoteli waliyofikia kwa deni la Sh 398,000.
Mjumbe wa bodi ya timu hiyo, Catherine Masasi amesema tangu walipomaliza mchezo wao uliopita dhidi ya African Lyon walipofungwa 5-2 timu iliendelea kubaki jijini humo huku ikikabiriwa na changamoto nyingi licha ya kuvumilia.
Amesema kwa siku tatu mfululizo wachezaji 13 na viongozi watatu wamelala nje baada ya kufukuzwa hotelini kwa deni hilo na kwamba hata leo hawajajua muafaka wao na kuomba wadau kuisaidia.
"Hadi sasa deni ni Sh 398,000 japokuwa hatujajua tunaondoka lini na kwa usafiri upi, hakuna chakula wala kitu chochote hatujawasiliana na mamlaka yoyote japokuwa tulikuwa na wazo la kuwatafuta bodi ya ligi ili tuone wanatusaidiaje" amesema Catherine.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas amesema kuendesha mpira ni gharama akisema hata yeye ana majukumu mengi kwani Mashujaa FC nao wanamtegemea huku akiahidi kulimaliza kiutawala.
"Utawasiliana na RAS (Katibu Tawala) aone anawakwamuaje kwakuwa ni suala la utawala, mengine timu kuendeshwa na viongozi wababaishaji wanaidharirisha kwa manufaa yao, kuendesha mpira siyo masihara, nimeita kikao Jumatatu niongee nao" amesema Thomas.