Prime
Waangola kumchomoa winga Yanga, dili lipo hivi!
WAKATI ikidaiwa Yanga itaachana na winga nyota wa timu hiyo, Mgambia Buba Jammeh taarifa kutoka Angola zinaeleza uongozi wa C.D. Primeiro de Agosto inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola Girabola, umeonyesha nia ya kumsajili kwa msimu wa 2026-2027.
Nyota huyo alijiunga na Yanga Januari 31, 2026, katika dirisha dogo la usajili akitokea Interclube ya Angola kwa mkataba wa miaka miwili, ingawa kiwango chake hadi sasa hakijawaridhisha mabosi wa timu hiyo na mwisho wa msimu huu ataondoka.
Buba alisajiliwa na Yanga ikiwa ni pendekezo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mreno Pedro Goncalves japo maisha yake kwa sasa na mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu, yamekuwa shakani kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa.
Kabla ya kujiunga na Yanga, Buba aliitumikia Interclube katika mechi saba zote zikiwa za Ligi Kuu Angola na kufunga bao moja, akiwa ni miongoni mwa nyota waliotabiriwa makubwa ingawa mambo yamekuwa tofauti na sasa ataondoka mwisho wa msimu.
Katika Ligi Kuu Bara, nyota huyo hajafunga bao lolote kwa msimu huu wa 2025-2026, ingawa ameifungia mabao matatu kwenye Kombe la CRDB, japo hayajatosha kurudisha imani ya uongozi wa timu hiyo juu ya hatima yake mwisho wa msimu wa 2025-2026.
Wakati Yanga ikimfungulia mlango wa kuondoka mwishoni mwa msimu huu, C.D. Primeiro de Agosto inadaiwa imeanza mazungumzo ya kuipata saini yake msimu wa 2026-2027, japo hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili.
Katika Ligi Kuu ya Angola ya Girabola msimu wa 2025-2026, C.D. Primeiro de Agosto inashika nafasi ya tatu na pointi 57, baada ya kushinda mechi 15, sare 12 na kupoteza mbili, kati ya 29, nyuma ya vinara, Petro Atletico yenye pointi zake 69.