Waandishi wanawake kujifunza lugha zaidi ya tano
Muktasari:
Waandishi wa habari wametakiwa kujiwekea utamaduni wa kusoma vitabu mbalimbali, kujua lugha zaidi ya tano na kufanya kazi za kipekee.
WAANDISHI wa habari za michezo upande wa wanawake, wametakiwa kufanya kazi za kipekee ambazo zitawatofautisha na wengine, pia wajifunze lugha zaidi ya tano na kujiwekea utamaduni wa kusoma vitabu.
Lengo ni kuwafanya kuwa bora zaidi na si bora waandishi anayeishi ilimradi siku zinakwenda.
Hayo yameelezwa na mkufunzi wa semina ya siku mbili kwa waandishi hao, iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), Usher Kamugisha.
Katika semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam waandishi 27 walishiriki kutoka vyombo vya habari tofauti.
Usher alisema, mwandishi anayejua lugha zaidi ya tano, inamsaidia kufanya kazi zake kwa nafasi na kujiamini.
"Unaweza kujua lugha moja au mbili, mfano Kiswahili na Kiingereza lakini Afrika Magharibi wanajua Kifaransa, hivyo lazima ujifunze lugha tofauti,"alisema Usher.
Akizungumzia vitabu, Usher alisema, vitabu vinafanya kujifunza vitu vingi ambavyo vitamuongezea ubora katika kazi yake.
"Hata suala la lugha, kitabu kinaweza kuwa msaada mkubwa kwako. Kuangalia YouTube lakini kwa ajili ya kujifunza na vitu mbalimbali, "alisema Usher ambaye anafanya kazi na Supersport, FIBA pamoja na BBC.
Semina hiyo ilifanyika kwa muda wa siku mbili ilifungwa jana Alhamisi na Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani..