Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WA ilivyoenzi rekodi za Bayi Makumbusho ya Dunia

WA Pict
WA Pict

Muktasari:

  • Hafla hiyo ilifanyika jana iliongozwa na Rais wa WA, Sebastian Coe, huko Ufaransa lilipo jumba hilo la Makumbusho ya Riadha ya Dunia (MOWA) ambapo Bayi akiwa na nyota baadhi wa mataifa mengine waliowahi kuvunja rekodi wameshiriki, hafla iliyoenda sanjari na michezo ya Olimpiki inayoendelea Paris.

REKODI za nguli wa riadha nchini, Filbert Bayi zimepewa heshima ya kuwa katika Jumba la Makumbusho la Riadha ya Dunia, huku vifaa alivyokimbilia nyota huyo wa mbio za kati vikionyeshwa katika hafla iliyoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Dunia (WA).

Hafla hiyo ilifanyika jana iliongozwa na Rais wa WA, Sebastian Coe, huko Ufaransa lilipo jumba hilo la Makumbusho ya Riadha ya Dunia (MOWA) ambapo Bayi akiwa na nyota baadhi wa mataifa mengine waliowahi kuvunja rekodi wameshiriki, hafla iliyoenda sanjari na michezo ya Olimpiki inayoendelea Paris.

Hafla ya kumbukumbu za nyota hao imefanyika ukumbi wa Monnaie de Paris Museum, jijini Paris ikiwa heshima nyota hao akiwamo Bayi aliyevunja rekodi mbili za riadha za dunia, ambazo zimeorodheshwa katika Makumbusho hiyo iliyopo mjini Monaco.

Bayi, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), akizungumza na Mwanaspoti kwa simu kutoka Ufaransa amesema kupewa heshima ya kumbukumbu zake kuwepo katika  Makumbusho ya Riadha ya Dunia ni jambo kubwa.

"Hii sio kwangu tu, ni historia ya Watanzania, ni jambo ambalo wenzetu wanalipa uzito na kuendelea kuwaenzi nyota waliofanya vizuri kwenye riadha na inazidi kuwajenga hata vijana wa sasa kufuata nyayo," amesema.

Mafanikio makubwa zaidi ya Bayi yanatajwa katika fainali ya mita 1500 katika Michezo ya Madola ya 1974, jijini Christchurch, New Zealand, aliposhinda medali ya dhahabu mbele ya mwanariadha wa New Zealand John Walker na Mkenya Ben Jipcho.

Mwaka 1974,  Bayi aliweka rekodi mpya ya dunia ya dakika 3:32.16, iliyoidhinishwa na IAAF sasa WA ikivunja rekodi iliyowekwa na Mmarekani Jim Ryun wakati huo.

Rekodi hiyo ya Bayi katika Michezo ya Madola ilivunjwa miaka 48 baadae na mwanariadha kutoka Australia, Ollie Hoare  kwenye michezo hiyo ya mwaka 2022 iliyofanyika mjini Birmingham, Uingereza.

Kwenye michezo ya 2022,  Bayi ndiye alipewa heshima ya kumvalisha medali Hoare aliyevunja rekodi ya Bayi ya dakika 3:32.2 yeye akitumia dakika 3:30.12.

Mbali na rekodi ya mbio ya mita 1500 mwaka 1974, mwaka mmoja baadaye (1975) katika mashindano ya ‘Dream Mile’, jijini Kingston Jamaica , Bayi alivunja rekodi ya maili moja iliyokuwa inashikiliwa na Jim Ryun.

Mafanikio mengine ya Bayi yalikuwa Katika michezo ya Olimpiki ya Russia akiwa miongoni mwa Watanzania wawili walioshinda medali mwaka 1980 , akitwaa fedha kwenye mbio ya mita 3000 kuruka viunzi na kukanyaga maji, huku Suleiman Nyambui akitwaa medali kama hiyo kwenye mbio ya mita 5000.

Hadi leo, rekodi hiyo ya medali katika Olimpiki haijwahi kuvunjwa, huku tegemeo likiwa kwa nyota wanne, Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu ambao watachuana kwenye mbio ya marathoni kwa wanaume na wanawake Agosti 10 na 11.