Viwanja, kifo cha soka la Mwanza
Muktasari:
Mwanza ina historia yake kiasi kwenye soka la Tanzania. Ndiko ilikotokea Pamba, moja ya timu zilizowahi kutamba nchini miaka hiyo na kuibua wanasoka wengi matata ambao baadaye walikuja kutamba pia na klabu za Simba, Yanga na hata timu ya taifa, Taifa Stars.
SAHAU kidogo matokeo ya mechi ya jana Jumanne ya Toto African iliyochezwa pale Taifa. Usiwaze sana kuhusu nafasi ya Mbao FC kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara itakayokunja jamvi mwishoni mwa wiki. Timu hizi za Mwanza hazijarejesha yale makali ya mkoa huo kwenye soka la Tanzania kama ilivyokuwa enzi ya Pamba.
Mwanza ina historia yake kiasi kwenye soka la Tanzania. Ndiko ilikotokea Pamba, moja ya timu zilizowahi kutamba nchini miaka hiyo na kuibua wanasoka wengi matata ambao baadaye walikuja kutamba pia na klabu za Simba, Yanga na hata timu ya taifa, Taifa Stars.
Kuna watu kama; Khalid Bitebo, Fumo Felician, George Masatu, Hussein Marsha, David Mwakalebela, Dan Mhoja, John Makelele, Bita John na wengineo wengi tu ambao waliingarisha Mwanza wakiwa na Pamba ‘Wana TP Lindanda’.
Si timu tu, Mwanza pia ni moja ya miji michache iliyobahatika kuwa na viwanja vizuri (kwa wakati huo) vya soka tangu enzi la ukoloni. Japo sasa unasikitisha kwa hali yake ilivyo, lakini Uwanja wa Nyamagana uliojengwa na wakoloni tangu mwaka 1945 ulishakuwa na umaarufu wake. Hata Simba na Yanga ziliwahi kukipiga hapo.
Kadiri miaka inavyosonga mbele, nyota ya soka la Mwanza imekuwa ikififia kuanzia kwenye vipaji hadi viwanja. Pamba haipo tena kwenye ramani, Toto ndio hiyo inachechemea na Mbao iliyoibuka juzi juzi nayo bado changa.
Kwa namna moja, ni wazi kuwa suala la uhaba wa viwanja limechangia kwa kiasi kikubwa kudumaa kwa soka la Mwanza.
Mwanaspoti limebaini kwa Mwanza, maeneo mengi yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya matumizi ya michezo yamevamiwa na watu kwa ujenzi au kubadilishwa matumizi, huku viwanja kama Nyamagana vikishindwa si tu kuendelezwa, bali pia kutunzwa. Sasa vinakufa.
Hata katika maeneo mapya, hakuna maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo. Vijana wameminywa mno katika kuhuisha vipaji vyao vya soka. Sasa wanalazimika kujibana kwenye viwanja vichache kama vya shule za msingi au sekondari ambazo nazo si zote zenye viwanja.
Mwanaspoti linakuletea uchunguzi uliofanyika katika baadhi ya maeneo ya mijini na vijijini ya Sengerema, Nyamagana na Ukerewe, ambayo ni kati ya wilaya saba za Mwanza jinsi yanavyokabiliwa na changamoto hiyo.
HALI ILIVYO UKEREWE
“Tuna viwanja vinane tu kwa ajili ya michezo. Hii ni idadi ndogo kulinganisha na zaidi ya timu 32,” anasema Deus Apolinary, Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Ukerewe.
Anasema licha ya vijana wa Ukerewe kujikita kwenye uvuvi, lakini wanazo timu 32 zilizosajiliwa na kati ya hizo, 28 zinacheza Ligi Daraja la Nne ngazi ya wilaya na zilizosalia zinashiriki Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Mwanza.
Hata hivyo, Apolinary anasema kati ya viwanja hivyo vinane vinavyotumika kwa ajili ya mechi za ligi hiyo ni viwili tu, Mongella Sokoni kilichopo Kata ya Kagera na Ukuta Mmoja unaomilikiwa na CCM, ndio kidogo vina afadhali.
Wakati Mongella unaomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe una uzio wa vibanda vya biashara, Ukuta Mmoja hauna uzio hivyo kuwepo kwa njia za miguu na magari yanayokatiza uwanjani hata wakati wa mechi.
“Viwanja vya wazi vya michezo vilivyovamiwa au kubadilishwa matumizi ni Nansio Kagera, Mahanda, Ukara na Busiri. Wanamichezo katika maeneo hayo hawana mahali mbadala pa kufanyia mazoezi au mechi,” anasema.
NYAMAGANA
Pamoja na Wilaya ya Nyamagana kuwa kitovu cha Jiji la Mwanza ikiwa na timu 29 zinazoshiriki ligi za wilaya na mkoa ukiziweka kando Toto na Mbao za Ligi Kuu Bara, Nyamagana ina uhaba mkubwa wa viwanja. Hata vilivyokuwapo zamani vimevamiwa.
Katibu Chama cha Soka cha Nyamagana (NDFA), Gilbert Dady, anasema kwa lundo la timu walizonazo, wanalazimika kuminyana katika viwanja vinane tu vya umma.
“Acha na Toto na Mbao, pia tuna timu 16 Ligi ya Wilaya na zipo nyingine 11 za Ligi Daraja la Tatu Mkoa. Kwa kweli hali ni mbaya,” anasema Dady.
Wilayani hapo pia kuna viwanja vingine vitatu; Butimba TTC, Nyamagana na Alliance. Hivyo vinamilikiwa na taasisi hivyo ni vya kulipia na timu nyingi zinashindwa kuvitumia.
Uwekezaji uliofanyika Uwanja wa Nyamagana hivi karibuni kwa kuwekwa nyasi bandia, kwa mujibu wa mbunge wa jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula, umegharimu zaidi ya Sh600 milioni.
SENGEREMA WAGOMBEA VYA SHULE
Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Sengeremea (Sedifa), Revocatus Buhembo, anasema wilaya hiyo ilipaswa kuvitegemea Viwanja vya Stendi ya Mwembe Yanga na Ibisabagenyi, lakini hakuna namna kwani vimevamiwa na kubadilishwa matumizi.
“Kutokana hali hiyo vijana wetu wanalazimika kutumia viwanja vya shule kwa ajili ya mazoezi na mechi za ligi,” anasema Buhembo.
Anasema viwanja hivyo vya shule vinatumika kwa masharti ikiwemo kutoingilia ratiba za masomo na vipindi vya michezo kwa wanafunzi, hivyo hali ni ngumu kwa timu za mitaani.
Sengerema ina timu tatu zinazoshiriki Ligi ya Mkoa wa Mwanza (Copco Veteran, Sedico na Igogo) na tano zipo Ligi ya Wilaya ambazo ni West Singer, Polisi, Mission, Young Boys na Leopard.
KIFO CHA VIPAJI
Msimamizi wa klabu ya Ncheye Academy, Manumbu Ncheye, hutumia zaidi ya Sh400,000 kwa mwezi kugharimia usafiri wa wachezaji wake kwa ajili tu ya kwenda kufuata uwanja vya mazoezi. Kituo chake kipo Nyambiti Buzuruga, wilaya ya Ilemela.
Ili kupunguza gharama, anasema kituo chake kinafanya mpango wa kuhama kutoka Nyambiti kwenda mabatini ambapo ndipo kuliko na uwanja wa kukodi.
Suleiman Abubakar, mchezaji wa Nyegezi All Stars anayeishi Nyamanoro jijini hapa, hutumia Sh800 kila siku kwa ajili ya nauli ya kwenda na kurudi mazoezini katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Nyablogoya, Nyegezi Kona. Katika eneo lake na la jirani hakuna uwanja. “Ninawashukuru wazazi wangu wananiunga mkono kwa kunipa nauli,” anasema Abubakar ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza.
SOKA LIMEDORORA
Kuporomoka kwa soka la Mwanza kumepunguza mashabiki katika mechi hata kwenye viwanja vilivyoboreshwa kikiwamo Nyamagana.
Ingawa Meneja wa Nyamagana, Manumbu Malwaza, hakuwa tayari kutaja wastani wa mapato ya uwanja huo, lakini chanzo chetu kimesema uwanja huo huingiza kati ya Sh400,000 na 500,000 kwa mchezo kutegemeana na timu zinazocheza.
“Timu kama Mwanza Terminal ndiyo inaingiza zaidi kwani ina mashabiki wengi, hao huingiza hadi Sh500, 000,” kilisema chanzo chetu.
Kwa maana hiyo uwanja huo unaweza kuingiza kipato kisichozidi Sh6 milioni kwa mwaka kutokana na mechi zisizozidi 10 za Ligi Daraja la Tatu ngazi ya mkoa.
Maana yake mwitikio wa mashabiki ukiendelea kuwa mdogo hivyo, huenda ikachukua hata miaka 100 kurejesha gharama za ukarabati uliofanyika.
Kwa mujibu wa Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire, ipo pia mipango ya kujenga maeneo ya biashara na majukwaa kuuzunguka uwanja huo.
KIRUMBA SASA
Uwanja wa Kirumba unaomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio kioo cha Mwanza kwa viwanja. Unatumiwa kwa mechi za Ligi Kuu Bara.
Itaendelea