Visura 13 kuwania taji la Miss Ilala 2024

Muktasari:
- Tayari warembo hao wameingia kambini, kujiandaa na shindano hilo, huku washindi, pamoja na zawadi nyingine wataingia kwenye kinyang’anyiro cha kumsaka mrembo wa Kanda ya Dar es Salaam tayari kwa fainali ya Miss Tanzania baadae mwaka huu.
WAREMBO 13 wanatarajiwa kuonyeshana kazi wakati wa shindano la kuwania taji la Miss Ilala 2024, litakalofanyika Agosti 16 kwenye Ukumbi wa Warehouse, Masaki huku wakipania kufanya vizuri na kufuata nyayo za watangulizi wao katika fainali za taifa, Miss Tanzania.
Tayari warembo hao wameingia kambini, kujiandaa na shindano hilo, huku washindi, pamoja na zawadi nyingine wataingia kwenye kinyang’anyiro cha kumsaka mrembo wa Kanda ya Dar es Salaam tayari kwa fainali ya Miss Tanzania baadae mwaka huu.
Kwa nyakati tofauti, warembo hao wamejinasibu kufanya vizuri wakiamini Miss Tanzania 2024/25 atatoka katika kanda hiyo na kufuata nyayo za dada zao Hoyce Temu na Jacqueline Ntuyabaliwe waliotokea Ilala na kutwaa taji la Miss Tanzania kwa miaka tofauti.
Taji la Miss Tanzania mwaka huu linashikiliwa na Tracy Nabukeera atakayeiwakilisha nchi katika fainali za Dunia, Miss World baadae mwaka huu au mwakani kulingana na kalenda ya Miss World, huku Miss Tanzania wa 2024/25 akishiriki Fainali za Dunia zitakazofuatia.
Akizungumzia maandalizi ya warembo, Mkufunzi wa Miss Ilala, Irene Karugaba alisema kambini mbali ya urembo, washiriki hao wamefundishwa maadili na usafi wa kimwili na kiroho, kwa na malengo na kufanya kazi za jamii.
“Pia wamefundishwa ujasiriamali kwa kuwa urembo unaendana na vitu vyote hivyo, washiriki wote wako vizuri na majaji watapata wakati mgumu kupata mshindi na hakuna shaka miongoni mwa warembo hawa tutamtoa Miss Tanzania,” alisema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Locharl inayoandaa Miss Ilala, Love Msangi alisema kabla ya fainali, Agosti 16 warembo hao watakwenda kuwatembelea watu wenye mahitaji na watoto yatima katika kituo cha Buguruni kama moja ya ushiriki wao katika jamii.
Alisema, katika ziara hiyo wanatarajia kuwa na wadhamini wao wakiongozwa na mdhamini mkuu, Kmapuni ya Bia ya Serengeti, ziara ambayo inakwenda kuongeza kitu kwa warembo hao ambao baadhi yao watakuwa mabalozi kwenye kampuni mbalimbali zinazodhamini shindano hilo.
Wakizungumza kwa niaba ya warembo wenzao, Zena Habibu na Nelly Said kwa nyakati tofauti alisema, wameipanga kufanya vizuri na wanaamini Ilala itatoa mrembo atakayeshinda taji la Dar es Salaam, Tanzania na hata kufanya vizuri
“Tunajiamini na tunaamini tutafanya vizuri hadi ngazi ya taifa, tukiwa kambini tumejifunza na tunaendelea kujifunza vitu vingi, kwani wengi kama si wote hapa ni wanafunzi wa vyuo, tumefundishwa ujasiriamali na mambo mengi ya urembo na maisha,” alisema Nelly.
Zena anasema shindano la Ilala linakwenda kuleta fursa nyingine kwao, wamejipanga kufanya vizuri na kuendeleza historia ya Ilala kwenye fainali za taifa.
Ofisa Sanaa Mwandamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Abel Ndaga akizungumza kwa niaba ya Katibu mtendaji wa Baraza hilo amesema Miss Ilala mwaka huu anananafasi ya kutwaa taji la Miss Tanzania kutokana na ubora wa warembo wake.
“Tunaamini atapatikana mrembo bora ambaye atavchukua taji la Miss Tanzania na kuiwakilisha vema kwenye Miss world,” alisema.