Uwanja umeshainama kwa Jonathan Sowah

Muktasari:
- Jamaa kaanza kucheza Ligi Kuu mwezi Januari tu mwaka huu baada ya kunaswa katika kipindi cha usajili cha dirisha dogo na akaweka kambani mara 11.
ILE kasi ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu ya Jonathan Sowah tangu alipojiunga na Singida Black Stars ilikuwa inatisha sana na jamaa ghafla aliteka hisia za wengi ndani ya muda mfupi.
Jamaa kaanza kucheza Ligi Kuu mwezi Januari tu mwaka huu baada ya kunaswa katika kipindi cha usajili cha dirisha dogo na akaweka kambani mara 11.
Basi baada ya kufunga mabao hayo 11 hapa kijiweni kuna kikundi cha wadau wa soka kikaanza kuamini Sowah atachukua kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.
Hata hivyo, wakati zikibaki raundi mbili tu kwa Ligi Kuu msimu huu kumalizika, kuna uwezekano finyu kwa Sowah kuwa mfungaji bora kwa vile tayari kuna gepu kubwa la mabao manne ambalo amepitwa na Jean Charles Ahoua anayeongoza kuwa kufumania nyavu akiwa na mabao 15.
Maana yake ili Sowah awe mfungaji bora anatakiwa kuhakikisha anafunga kadri iwezekanavyo katika mechi tatu zilizobakia dhidi ya Simba, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons.
Wakati huo anatakiwa pia kuwaombea nuksi nyota kutoka timu nyingine ili wasifunge mabao katika mechi zao zilizobaki ili amalize akiwa kinara wa kufumania nyavu msimu huu.
Hata hivyo, naona dalili nyingi Sowah hawezi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu lakini kiukweli wale jamaa wanaochezea Simba na Yanga wamejipanga sana na kadri msimu unavyozidi kukaribia kumalizika na wenyewe wanazidi kufumania nyavu tu.
Sio rahisi kwa Sowah kupachika namba kubwa ya mabao katika mechi ambazo Singida Black Stars imebakiza lakini hata akifanya hivyo hakuna namna anaweza kuwazuia kina Ahoua, Clement Mzize, Prince Dube, Steven Mukwala kufunga mabao katika mechi zilizosalia za timu zao.
Cha msingi Sowah anapaswa kufurahia kile ambacho amekivuna hadi sasa na kisha kuanza kujipanga kwa ajili ya msimu ujao.