Umewahi kuifikiria vita ya Wawa na Madaraka Suleiman?

Mchezaji wa Azam FC,Serge Wawa .
Muktasari:
Hata baada ya miaka mingi sasa tangu aachane na soka, mwili wake haujasinyaa. Bado ana mwili mkubwa kuliko asilimia 80 ya washambuliaji wa kileo. Unakaa chini na kujiuliza, nyakati zimekwenda wapi?
KATIKATI ya jiji, katika ofisi moja hivi, wiki iliyopita nilikutana na Madaraka Suleiman. Bado ana siha njema. Bado ni mtulivu kama alivyokuwa. Bado mwili wake umejengeka kama ulivyokuwa.
Hata baada ya miaka mingi sasa tangu aachane na soka, mwili wake haujasinyaa. Bado ana mwili mkubwa kuliko asilimia 80 ya washambuliaji wa kileo. Unakaa chini na kujiuliza, nyakati zimekwenda wapi?
Namwamkia Madaraka mara mbili. Kwanza kwa sababu amenizidi sana umri. Kama amemzidi umri mdogo wake Idd Suleiman ‘Kibode’ ambaye ni kaka yangu, vipi kwa Madaraka mwenyewe?
Hata hivyo, namwamkia Madaraka kwa mara nyingine kwa sababu ya kukumbuka ubora wake. Aliitwa Mzee wa Kiminyio kwa sababu ya kuwaminya mabeki na kwenda kufunga. Alitumia nguvu, akili, maarifa na kila alichojaliwa kuweza kuzifikia nyavu za adui.
Nazungumza mambo mengi na Madaraka, lakini ghafla namuuliza, ni kwa nini siku hizi mashabiki wa Simba na Yanga huwa wanaanguka na kuzimia sana pindi timu zao zinapopata matokeo mabovu?
Madaraka ananishangaa “Edo, sio mashabiki tu, hawa wachezaji wenyewe wanaangukaanguka tu, itakuwa mashabiki? Yaani wachezaji hawapo fiti kabisa nakuambia,” anasema Madaraka.
“Ukienda uwanjani sasa hivi mchezaji akiruka hewani akirudi chini lazima daktari aingie uwanjani. Mimi nashangaa sana. Muda mwingi wachezaji wako chini. Kila dakika daktari anaitwa. Ni kwa sababu hawapo fiti.”
“Mpira unachezwa dakika chache tu aisee. Wachezaji wetu wa siku hizi sio wabaya, lakini hawapendi mazoezi magumu. Mpira ni mchezo wa mazoezi magumu na inabidi ucheze ukiwa fiti.”
Hii ndiyo inakuwa topiki kubwa kati yangu na Madaraka. Ndiyo ni kweli. Wachezaji wa sasa Tanzania hawapo fiti. Hakuna ubishi kuhusu hilo. Kumpata mchezaji mwenye nguvu kama za Paschal Wawa ni shida kweli kweli katika nchi hii.
Hapo hapo najikuta nikijiuliza. Ingekuwa vipi kama Wawa angekutana na Madaraka katika enzi zao? Wawa ni bingwa wa nguvu na akili, lakini na Madaraka alikuwa vivyo hivyo kama Wawa. Tofauti ni kwamba walicheza katika nafasi mbili tofauti.
Kumbe Madaraka anaufahamu vyema mpira. Anachonieleza kuhusu vita ya Wawa ni kitu tofauti na fikra zangu. Nilidhani kwamba angenieleza jinsi ambavyo angepambana naye katika nguvu. Kumbe hapana.
“Beki kama Wawa ni rahisi kumpita kama ukipata viungo wazuri washambuliaji. Unajua siyo lazima upambane kinguvu na mabeki wenye nguvu. Beki kama Wawa unahitaji uwe na kiungo mzuri mshambuliaji. Kiungo ambaye anakokota mpira vizuri na kumtamanisha Wawa aje kumkaba. Wakati Wawa anatoka, kiungo huyo anaupitisha mpira jamaa anapishana nao. Siyo lazima nguvu,” anasema Madaraka.
Hata hivyo, Madaraka ananidokeza kuwa alipokwenda kucheza soka la kulipwa Uarabuni aliwahi kukutana na wachezaji wengi wa Afrika Magharibi waliokuwa wanacheza soka kama la Wawa.
“Matajiri wa kule walikuwa wanachukua wachezaji wengi kutoka nchi hizo za kina Wawa. Tulikuwa tunapambana nao lakini ukicheza nao unajua kabisa huyu jamaa ni mchezaji wa kulipwa. Wana nguvu, akili na kujituma sana aisee.”
Mazungumzo yangu na Madaraka yanazidi kuwa matamu. Tunaongea hili na lile. Baadaye ananifafanulia jinsi ambavyo duniani hakuna mshambuliaji mzuri kama hakuna viungo wazuri.
“Washambuliaji wa sasa hivi wanapata shida sana. hakuna viungo wazuri. Mshambuliaji inabidi uwekewe mipira ukutane nao njiani na kumtazama kipa. Lakini kama kila wakati unapewa pasi wakati umegeuka unatazama pasi ilipotokea, ni vigumu kufunga.”
Baadaye maongezi yetu na Madaraka nayapeleka katika maisha binafsi ya wachezaji. Madaraka ni mkimya na mnyenyekevu kama alivyokuwa. Nafahamu kuwa anaheshimika katika mitaa ya kwao Manzese Uzuri. Ananiambia kuwa anashangaa kwa nini wachezaji wa kileo wana maringo sana.
“Waambieni hawa wachezaji, hizi timu wamepita wachezaji wengi sana. wakati ukiwa katika fomu inabidi ufanye mambo ya maana katika maisha. Ukiwa vizuri katika hizi timu unapata sana pesa. Wakati wako ukipita basi,” anaongeza Madaraka.
Muda si mrefu naachana na Madaraka. Hata hivyo ananiachia mawazo. Ingekuwa vipi kama Madaraka angecheza katika zama hizi? Ingekuwa vipi kama ubora wake ule angeuonyesha katika zama hizi?
Katika ubora wake, nchi sahihi kwa wachezaji wa Tanzania kwenda ilikuwa ni Uarabuni. Madaraka aliwahi kujaribu bahati yake katika nchi hizo. ina maana katika zama hizi Madaraka angekuwa na sifa zote za kucheza Ulaya?
Kama yeye katika zama za zamani alijaribu kutoka, vipi kuhusu wachezaji wa kileo ambao wanaishi katika dunia iliyo mkononi? Wanashindwa nini kujaribu? Kuna mengi niliyoendelea kujifunza kupitia Madaraka wiki iliyopita.
Wachezaji wa zama hizi wana mengi ya kujifunza kutoka kwake, lakini nadhani wanatumia muda mwingi kukaa katika Facebook, Whatsapp, Instagram wakibishana kuhusu ubora wa Ally Kiba au Diamond Platinumz. Wakati utatuambia.