TUONGEE KISHKAJI: Mzungu wa Simba amenikumbusha Top C wa ulofa

MZUNGU anaondoka Simba akiwa na bao moja na hit song moja kubwa kwelikweli. Wimbo wake wa ‘Mlete Mzungu’ umekuwa maarufu kiasi kwamba unapigwa kila sehemu hadi harusini.

Ukiwa harusini ikigongwa ‘Mlete mzungu, mlete mzungu’ ndiyo utaelewa maana ya furaha. Ukumbi mzima lazima usogee kwenye dance floor na watu wanaruka kwelikweli. Masistaduu hadi wanavuaga skuna wanaweka pembeni ili wacheze kwa kujinafasi.

Sio huko tu Mlete Mzungu ikipigwa club ni balaa - tena usiombe iwe ile mida mibovu saa sita flani hivi watu wameanza kunywa tangu saa nne kwa hiyo wameshalewa vibaya ni fujo mbovu mbaya. Dance floor inakoma.

Halafu wimbo wenyewe ni ‘parody tu’, yaani wimbo uliotengezwa kwa kuunganisha baadhi ya sauti za mazungumzo ya Ofisa Habari wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally wakati anamtambulisha mchezaji wao Dejan Georgijevic siku ya Simba Day.

Nina uhakika hatutasikia wimbo mwingine wa Dejan kwa sababu jamaa ndiyo anaondoka Simba.

Hiyo ni sawa na kusema Dejan ataingia kwenye list ya ‘wasanii’ waliowahi kutambaa na wimbo mmoja tu kisha wakapotea.

Kitu kinachonifanya niwaze hawa wasanii huwa wanaenda wapi? Wanakutwa na nini?

Msanii kama Top C alitamba na wimbo wake unaoitwa Ulofa. Hiyo ngoma ilikuwa ni hit song kali sio poa. Tena kipindi kile muziki ndo umechangamka balaa. Diamond wa moto, Bob Junior hashikiki, Alikiba yupo kazini, wasanii wanapishana airport kwenda kushuti video Afrika Kusini.

Top C akaachia bonge moja la ngoma lenye verse tatu na mashairi makali yenye uzito. Ukiyasikiliza unasema kweli huyu msanii alichukua kalamu na karatasi akasema sasa nataka kuandika wimbo.

Jamaa pia ana sauti zuri ya kupanda na anajua kuitumia sio poa. Kwenye hiyo ngoma alikuwa analalamika hadi mwenyewe utakubali kuwa jamaa alikuwa ni lofa kweli.

Na kwenye video pia alipatia alitoa video moja hivi kali ambayo alimtumia Shilole na Sharo Milionea kama video queen na king mtawalia.

Enzi hizo Shilole yuko serious na Bongo movie na Sharo Milionea ndiyo ametoka kucheza uhusika ambao uliwashangaza wengi. Alikuwa ametoka kuigiza kwenye filamu ya kimataifa ya inayoitwa Chumo pamoja na Jokate Mwegelo.

Na kwenye hiyo filamu Sharo Milionea hakuigiza kama Sharo Milionea aliigiza kama mtu wa kawaida na akaua mbaya na kufanya sasa watu wamchukulie kuwa ni msanii kwelikweli.

Watu wakamchukulia kwamba ana uwezo wa kubadilika kiasi kile kutoka kuwa mchekeshaji mpaka muigizaji serious kwenye filamu ya kimataifa? Halafu sasa uhusika kama huo ndiyo akauigiza kwenye video ya Top C. Kwa hiyo ilikuwa ni video moja kubwa sana tena sana sana sana!

Ukiangalia uwekezaji uliofanyika kwenye kuandaa wimbo wa kwanza wa Top C kuanzia audio mpaka video ni lazima utakubaliana na mimi kwamba Top C tayari alikuwa ameshakamata mioyo yetu. Kwa hiyo kama angejaribu kuachia wimbo mwingine ni lazima tungemsikiliza.

Lakini matokeo yake mambo hayakuwa hivyo, Ulofa ilikuwa ndiyo mara yetu ya mwanzo na ya mwisho kumsikia Top C na hadi leo tunamuweka kwenye list moja na Dejan. Yuko wapi Top C? Hii hali mara nyingi huwaacha mashabiki wasijue ni vipi wanakosa mwendelezo wa ukali wa wahusika na hivyo kuacha ombwe flani katika tasnia.