Try Again: Bocco njia ya ukocha nyeupe

MWENYEKITI wa bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdalah 'Try Again' ni kama amemshtua nahodha wao John Bocco kugeukia upande wa ukocha ambao mchezaji huyo amekuwa akitamani.
Try Again ameyasema hayo wakati Simba ikisaini mkataba wa kuendeleza na kukuza vijana wa timu yao.
Try Again amesema Bocco mara kadhaa amekuwa akimwambia juu ya ndoto yake ya kuwa kocha na sasa njia kwake ni nyeupe kutokana na uwekezaji ambao umeanza kufanywa kwa vijana.
"Bocco nahodha wetu na wewe ndoto yako ya kuwa kocha wa vijana inatimia sasa maana mara kwa mara umekuwa ukiniambia kuhusu hilo, hivi karibuni tutaanza ujenzi wa akademi yetu na tayari niliongea na mwekezaji wetu," amesema Try Again.
Try Again amesema upande wa vijana bado wataongezwa aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola na meneja wao wa sasa Patrick Rweyemamu kwa ajili ya kuendeleza timu hiyo.
"Matola na Rweyemamu wataenda kwa vijana kupaimarisha, tunajua hili litaenda kuimarisha upande wa usajili wetu," amesema Try Again.
Simba imesaini mkataba wa miaka miwili na kampuni ya Mobiad Afrika kwa ajili ya kukuza na kuendeleza vijana wa timu hiyo wenye thamani ya Sh500 milioni.