TRA yaanza kujenga uwanja wa kisasa Kurasini

BAADA ya kuzindua wiki ya shukrani kwa mlipa kodi, Kamishna wa TRA Alphayo Kidata amesema tayari wameanza kujenga uwanja wa kisasa wa michezo maeneo ya Mivinjeni, Kurasini, Dar es salaam.
Wiki hiyo ya shukrani kwa mlipa kodi imezinduliwa jana kwa mbio na matembezi ya kilomita tano na 10 zilizoanzia katika viwanja vya Gymkhana Jijini Dar es salaam.
Matembezi hayo ambayo yalihusisha mashirika na kampuni mbali mbali zilizoalikwa yalihudhuriwa na kamishna mkuu wa TRA Alphayo Kidata ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi.
Mbali ya kuzindua wiki ya shukrani kwa mlipa kodi, Kidata alisema TRA inajenga uwanja wa kisasa wa michezo maeneo ya Mivinjeni, Kurasini.
Kidata alisema TRA imeandaa sera maalumu ya michezo katika kusaidia maendeleo ya michezo nchini na katika kuhakikisha hilo linafanyika kwa vitendo wameanza kutengeneza kiwanja hicho cha kisasa ambacho kitakuwa kikitumiwa na wafanyakazi wa TRA na wananchi wa kawaida.
Mbali ya kutoa shukrani pia wiki hii itakuwa na matukio mbali mbali ya kusaidia jamii ikiwa pamoja na kugawa madawati kwa shule.