Timu 20 kumenyana Jimbo Cup Ilemela
Mwanza. Msimu wa sita wa mashindano ya Angeline Jimbo Cup Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza utafunguliwa rasmi Jumamosi katika viwanja vinne wilayani humo ukishirikisha timu 20 zinazowania kombe na zawadi ya fedha.
Michuano hiyo itaanza Agosti 19, mwaka huu katika viwanja vya Baptist, Sabasaba, Buswelu na Kayenze huku bingwa akibeba kombe na zawadi ya Sh2.5 milioni.
Mshindi wa pili atapata Sh2,000,000, timu yenye nidhamu Sh500,000, kata yenye amsha amsha Sh500,000, mwamuzi bora Sh300,000, wachezaji bora Sh200,000 na mwandishi bora Sh300,000.
Akizungumza leo Agosti 16, 2023 wakati akikabidhi jezi na mipira kwa timu shiriki, Mwandaaji wa mashindano hayo, Angelina Mabula amesema msimu huu wameboresha zawadi ili kuwahamasisha vijana jimboni Ilemela kuvutika kushiriki kwenye michezo na kuachana na makundi mabaya.
Mabula ambaye ni Mbunge wa Ilemela na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema kupitia mashindano hayo wanawajenga vijana kiafya, kuwaondoa kwenye makundi hatarishi, kuwaandaa kwenye ajira huku lengo likiwa ni kuona michezo inazidi kushamiri na kuwajengea afya.
"Namshukuru Mungu azma niliyoiweka ya kuibua vipaji vya vijana kupitia michezo mbalimbali, leo ni msimu wa sita na tunaona faida mbalimbali za vijana wengi kujulikana akiwemo Kelvin John aliyetokea hapa, natamani kuona michezo inazidi kupaa katika Jimbo letu na wilaya ya Ilemela kwa ujumla,"
"Mwaka huu tumeongeza mchezo wa kikapu, mikono (volleyball), netiboli na soka la wanawake tunataka watu washindane siyo kubebwa, tucheze kwa ustaarabu tusiumizane kwa sababu ya zawadi," amesema Mabula
Naye, Kocha wa timu ya Kata ya Buswelu, Emmanuel Kingu amesema msimu uliopita waliishia hatua ya robo fainali lakini safari hii wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa michuano hiyo, huku akiomba mashabiki wa kata hiyo kuiunga mkono timu yao.
"Tumeshaanza maandalizi timu yetu imekuwa bingwa kata yetu tunaahidi tutafanya vizuri msimu huu, tunaomba sapoti yao tutapambana kwa ajili yao, tunaahidi kuchukua kombe msimu huu. Wachezaji ni waelewa mapungufu ni machache, nina kikosi kizuri na tutafanya vizuri," amesema Kingu