Tamasha la Wana Makete kurindima siku tatu Dar

Muktasari:

Tamasha la Utamaduni wa mtanzania kwa jamii ya Makete linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.

Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania kwa jamii ya Makete linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Oktoba 13, 2021 na Katibu wa Chama cha Maendeleo cha WanaMakete (Makete Development Association), Award Mpandila, katika mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia tamasha hilo.

Mpandila amesema tamasha hilo litafanyika kwa siku tatu mfululizo katika kijiji cha Makumbusho Kijitonyama kuanzia Novemba mwaka huu lengo likiwa kuwaunganisha wanajamii wote waishio Wilaya ya Makete na walio nje ya Wilaya hiyo.

Shughuli zitakazofanyika katika kipindi chote cha Tamasha ni pamoja na maonyesho ya vifaa vya asili vinavyoonyesha mila, desturi na utamaduni.

Kutakuwepo pia na maonyesho ya ngoma za asili, vyakula na vinywaji mbalimbali vya asili, mavazi na vivutio vinavyopatikana Wilayani humo.

“Ukiachilia mbali kuwa na maonyesho pia kutakuwa na warsha zitakazoongelea kwa mapana historia , mila na desturi pamoja na maendeleo ya jamii za Makete,kiafya, miundombinu, kilimo,rasilimali, utalii pamoja na hali ya uchumi kwa  ujumla,”amesema Mpandila.

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Monny Luvanda alitumia fursa hiyo kuwahimiza WanaMakete kujumuika nao katika tamasha hilo kwa kuwa lina manufaa makubwa kwa jamii yao ya Makete.

Kwa upande wake Mhifadhi Mila Mwandamizi wa  Makumbusho, Wilbard Lema amesema kufanyika kwa tamasha  hilo ni utaratibu uliowekwa na bodi ya Makumbusho ya Taifa tangu mwaka 1994 kuzipatia fursa jamii za Tanzania kuonyesha tamaduni zao katika kijiji hicho kila mwaka.

Lema amesema hii itakuwa mara ya 25 kufanyika kwa tamasha la aina hiyo,ambapo sasa ni zamu ya WanaMakete.

Mhifadhi huyo amesema pamoja na faida nyingine matamasha ya aina hiyo yanasaidia kushirikisha jamii kuendeleza mila na desturi za jamii ya Mtanzania.