Siyo saizi yenu

Muktasari:
Siyo hilo tu, Simba imeendelea kuikejeli Yanga kwamba wao si saizi yao inapofika kwenye soka la uwanjani, wao watawazidi kwenye mikwara ya uswahilini tu pamoja na siasa za soka la Bongo.
STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi jana Jumapili alifunga bao pekee lililothibitisha ndani ya uwanja kwamba yeye ni bora kuliko mpinzani wake, Kpah Sherman wa Yanga ambaye wanapokea mshahara unaofanana wa dola 3,500 (sawa na Sh5.3milioni).
Siyo hilo tu, Simba imeendelea kuikejeli Yanga kwamba wao si saizi yao inapofika kwenye soka la uwanjani, wao watawazidi kwenye mikwara ya uswahilini tu pamoja na siasa za soka la Bongo.
Okwi aliipatia Simba bao hilo la pekee katika dakika ya 51 baada ya kumchungulia kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyetoka mbali kidogo ya lango na Okwi alimuona na kutumia makosa hayo, Okwi alifunga bao hilo akipokea pasi nzuri kutoka kwa beki Hassan Kessy na hivyo kuifanya Simba ipande mpaka nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26 ingawa Yanga bado ipo kileleni ikiwa na pointi 31.
Okwi alikuwa na bahati ya kupata nafasi nyingi lakini alishindwa kuzitumia vizuri ambapo alikosa bao katika dakika ya 44 akiwa nje kidogo ya eneo la hatari ukiwa ni mpira wa faulo na shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango, faulo hiyo ilitokana na Haruna Niyonzima kumuangusha Ramadhan Singano ‘Messi’ huku Ibrahimu Ajibu naye akikosa bao dakika ya 43 shuti lake lilipaa.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm aliamua kufanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa mshambuliaji mzoefu Dan Mrwanda ambaye alionekana kujichanganya jambo ambalo lingeigharimu timu zaidi na nafasi yake ilichukuliwa na Hussein Javu ikiwa ni dakika ya 29 tu ambaye alituliza timu. Huku mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya akisimamisha mpira kwa muda baada ya Barthez kuumia baada ya kugongana na Messi.
Kabla ya kutolewa uwanjani, Mrwanda alionekana kushikwa na kigugumizi baada ya kushindwa kumalizia pasi safi ya Msuva na kuipoteza nafasi hiyo ya wazi kwa Yanga, Mrwanda alionekana kulalamikiwa na baadhi ya viongozi waliokwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko kuzungumza na wachezaji wakidai kuwa Mrwanda anaigharimu timu kwa kushindwa kuifungia.
Yanga nao walipoteza nafasi tatu za wazi katika shambulizi moja, krosi ya Hussein Javu ilikuwa ndefu kuipata Amissi Tambwe ambapo mpira ulimkuta Msuva aliyemtengenezea pasi Mrisho Ngassa ambaye pia alipiga shuti lililodakwa na Ivo.
Katika kipindi hicho hicho Tambwe alikosa nafasi nyingine baada ya kupiga shuti kali lililodakwa na Ivo, shuti hilo lilitokana na pasi ya Msuva. Messi alipoteza nafasi ya wazi dakika 65, shuti lake lilipaa juu kidogo ya lango ikiwa ni pasi ya Ajibu ambaye pia alipoteza nafasi dakika ya 60 shuti lake lililopaa pasi ikiwa ni ya Abdi Banda. Javu wa Yanga naye alikosa bao dakika ya 69, baada ya kupiga shuti kali ambalo Ivo alilipangua na kuwa kona ambayo pia haikuzaa matunda kwa Yanga.
Saanya alimtoa nje kwa kadi nyekundu Niyonzima baada ya kupata kadi mbili za njano katika mchezo huo, moja aliipata baada ya kumfanyia faulo Messi na nyingine kwa kupiga mpira wakati tayari filimbi imepigwa, hivyo kuifanya Yanga icheze pungufu kuanzia dakika ya 44.
Pluijim alionekana kutokuwa na imani na wachezaji wake kwani alifanya mabadiliko mengine kipindi cha pili ,alimtoa Ngassa na kumwingiza Kpah Sherman, jambo lililoonekana kuwakera mashabiki wa Yanga ambao walipiga kelele za kumtaka Ngassa aendelee kucheza na kuhimiza kwamba Msuva ndiye alistahili kutolewa nje.
Kocha wa Simba naye alifanya mabadiliko kwa kumtoa Banda ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Simon Sserunkuma huku Okwi na Simon wakikosa mabao dakika za 80 na 89, mashuti yao yaliokolewa na Barthez.
Wakati mpira unaanza Ivo alilitundika taulo lake katika nyavu za goli kwa mapana ambapo mwamuzi Saanya alimfuata na kumtaka aliondoe, alipoliondoa akalitandika chini pembeni ya goli, ingawa awali kulitokea malumbano kati ya Saanya na Ivo aliyekuwa akikataa kutoa taulo hilo.
Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kuwasili uwanjani hapo ambapo waliingia saa 8:20 mchana huku wakiongozwa na msafara wa magari madogo manane yaliyokuwa ya viongozi huku basi lao likiwa la tisa. Yanga wao waliingia saa 8:37 mchana wakiongozwa na msafara wa magari sita ya viongozi huku basi la wachezaji likiwa la saba.
MANJI VS MUSLEY
Baada ya mechi hiyo kumalizika, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji alizua sintofahamu kwa mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo kutokana na kushikwa na jazba na kujibizana maneno na mmoja wa viongozi wa Friends of Simba ambaye pia ni Mjumbe wa kuteuliwa katika Kamati ya Utendaji, Musley Ruwey kwa kilichodaiwa kuwa ni kusukumwa mtoto wa Manji walipokuwa kwenye ‘lifti’ za uwanjani hapo. Hata hivyo, kiongozi wa Yanga Mussa Katabaro na askari waliokuwa uwanjani hapo walituliza tafrani hiyo. Mwanaspoti lilimfuata Musley ambaye alisema: “Sijafurahia hii hali iliyotokea, sijamsukuma mtoto makusudi ilikuwa ni katika hali ya kuingia kwenye ‘lifti’ siwezi kufanya kitendo hicho kwa mtoto, nitamtafuta Manji kumwomba radhi, hili si jambo ambalo nililikusudia,”
NIYONZIMA, MSUVA
NA MRWANDA
Mashabiki wa Yanga walionekana kuwatupia lawama wachezaji hao kwa madai kwamba hawakustahili kuwemo katika kikosi cha jana kilichocheza na Simba kwani hawakuwa katika hali ya mchezo na walifanya makosa mengine ya makusudi.
Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika, Niyonzima alisema: “Sikusikia filimbi ya mwamuzi wakati napiga mpira hiyo ni kutokana na kelele zilizokuwa zimetawala uwanjani hapo, hivyo naomba radhi kwa mashabiki wetu kwa hili lililotokea ambalo lilinifanya nicheze kwa kuchanganyikiwa zaidi,”.
Katibu wa Yanga, Jonas Tibohora alikiri timu yake kucheza chini ya kiwango na kukubali matokeo hayo “Wachezaji wengi hawakuwa mchezoni kabisa na ndiyo maana tumepata matokeo haya.” Katika dakika tatu za nyongeza Simba ndiyo iliyoweza kumiliki mpira ambapo walipigiana pasi 24 bila Yanga kugusa mpira mpaka refa alipopuliza filimbi ya kumaliza mchezo.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana. Yanga ilifungwa na Simba katika mechi ya Nani Mtani Jembe bao 2-0.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa/Sherman na Dan Mrwanda/Hussein Javu.
Simba: Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Ramadhan Singano ‘Messi’, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na Emmanuel Okwi.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo Ndanda ililala kwa mabao 3-1 mbele ya Mgamboa wakati Mtibwa na Mbeya City ziligawana pointi kwa sare ya bao 1-1.