SIO ZENGWE: Namuona Mkapa nje ya Uwanja wa Taifa

Muktasari:

Kama Wabrazili walishangaa vile, iweje sisi wa ndani tusiache kuuzungumzia kila tunapotaja jina la Mkapa. Haiwezekani!

KWAHERI Mkapa, ndilo neno linaloweza kufupisha hisia zangu zote kwa ‘Muasisi wa Tanzania ya kisasa’, yaani Benjamin William Mkapa, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu aliyefariki usiku wa kuamkia Julai 24 akiwa hospitalini jijini Dar es Salaam.

Jina la Mkapa katika michezo linahusishwa zaidi na Uwanja wa Taifa kwa kuwa ndio kitu pekee alichosema amepania kukifanya katika nyanja hiyo na akakifanya, tena kwa ustadi na kiwango cha juu.

Ilitushangaza wengi kuona wale Waandishi wa Habari na Wapigapicha walioambatana na timu ya Taifa ya Brazil ilipokuja nchini mwaka 2010, wakiangalia nyasi za Uwanja wa Taifa kwa kutoamini kama wangeweza kuukuta katika nchi kama zetu.

Wengi walionekana kuchuchumaa chini kupiga picha zile nyasi, kugeuka upande wa mashabiki na kushangaa umati uliofurika siku hiyo. Inawezekana kabisa kwamba wana viwanja vizuri zaidi ya Uwanja wa Taifa, lakini kuambatana na timu hiyo katika viwanja mbalimbali duniani kuliwafanya waone ajabu kwa nchi kutoka Afrika Mashariki kuwa na uwanja wa kisasa kama huo.

Kama Wabrazili walishangaa vile, iweje sisi wa ndani tusiache kuuzungumzia kila tunapotaja jina la Mkapa. Haiwezekani!

Lakini, yapo mengi zaidi ambayo Mkapa aliyafanya katika michezo bila ya kusema mdomoni kwake kwamba, anafanya hivi kusaidia michezo, ukiachilia mbali ahadi ya kujenga uwanja na ile ya kutunga sheria ya Michezo ya Kubahatisha, ambayo inataka asilimia fulani inayotokana na mapato ya Bahati Nasibu ya Taifa iende kusaidia michezo, ingawaje hilo halijafanikiwa bado.

Lakini, kubwa nililotaka kuzungumzia leo ni sera zake za kiuchumi ambazo zilijenga mazingira mazuri kwa michezo kuanza kupata wadhamini baada ya kusukumwa kwa muda mrefu na wafadhili.

Ingawa Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ndiye anasifika kwa kulegeza masharti ya kuichumi na kuleta uchumi huria uliompa jina la ‘Mzee Ruksa’, Mkapa aliingia na mkakati wa kuwezesha sekta binafsi kukua, akiijengea mazingira mazuri. Alibinafsisha baadhi ya mashirika ya umma yaliyoendeshwa kwa hasara au bila ufanisi na kuhamasisha wawekezaji kutoka nje.

Ingawa baadhi ya wawekezaji waliingia vibaya na baadhi ya mashirika yaliyobinafsishwa hayakuzinduliwa na uwekezaji mpya, lakini yale yaliyofanya vizuri yalianza kupanua shughuli zake hadi katika michezo.

Kampuni kama Tanzania Breweries (TBL) ilionyesha mfano kwa kuanza kudhamini Ligi Kuu (enzi hizo Ligi Daraja la Kwanza) na baadaye kuweka nguvu katika michezo mingine kama Mpira wa Wavu, enzi za Dareva, Kikapu, mashindano ya urembo na muziki. TBL ilishaanza kujiingiza katika michezo tangu 1995 mwanzoni ilipojaribu kudhamini Ligi Kuu ya Muungano (sasa haipo) na baadaye Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) kabla ya kutibuliwa na uongezaji ovyo wa timu na ikajitoa. Lakini, udhamini wake mkubwa ukaja baadaye.

Ukiangalia uhamasishaji wawekezaji kutoka nje, unamuona Mkapa nyuma katika udhamini wa Vodacom wa Ligi Kuu. Vodacom imefanya kazi kubwa kuwezesha Ligi Kuu kuchezwa bila ya vikwazo, kiasi cha kuipa kiburi TFF kutunga kanuni inayoshusha daraja timu inayoshindwa kufika kituoni, jambo ambalo awali lilikuwa la kawaida.

Pia namuona Mkapa katika uwekezaji wa Kampuni ya Sigara, ambayo licha ya kuwa na timu tangu awali, uwekezaji mkubwa kwa timu hiyo ulikuja kuanzia mwaka 1996/97 wakati kampuni wawekezaji kutoka nje waliponunua hisa.

Ni wakati huo tulianza kuiona Sigara ikiwa na jezi kama za Rothman’s na nyingine tofauti na zile zilizokuwa zimezoeleka. Lakini uamuzi wa kuondoa udhamini wa sigara michezoni, ukaua safari yao.

Ukiangalia uhamasishaji sekta binafsi, unaiona Serengeti ikiwa mdhamini wa kwanza mkubwa wa timu ya Taifa, Taifa Stars kiasi cha kufuta kabisa yale mambo ya zamani ya watu kuchangia kambi ya Stars au Stars kupewa msaada wa jezi.

Kwa wale ambao wanadhani hawakuwahi kumuona uwanjani kushuhudia mechi, Mkapa alikuwepo uwanjani wakati tulipoibwaga Kenya bao 1-0, mfungaji akiwa Peter Tino mwaka 1981 katika mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Chalenji, akisimamia michezo na utamaduni.