Simba, Yanga zimechemsha kuwaacha mastaa hawa

Hamis Kiiza
Muktasari:
Wachezaji ambao hata usiowadhania husajiliwa na klabu hizi, kwa njia sahihi ama kwa visa na fitina. Ni kipindi ambacho Simba na Yanga hutambiana katika idara tofauti, kila timu huonyesha ubabe wake.
KIPINDI cha usajili kwa Ligi Kuu Bara ni kipindi cha vituko. Mambo mengi ya kushangaza, visa na vitimbi vingi hutokea kipindi hiki hususan kwa timu za Simba na Yanga.
Wachezaji ambao hata usiowadhania husajiliwa na klabu hizi, kwa njia sahihi ama kwa visa na fitina. Ni kipindi ambacho Simba na Yanga hutambiana katika idara tofauti, kila timu huonyesha ubabe wake.
Ubabe na tambo hizi za Simba na Yanga zimesababisha timu hizi kufanya baadhi ya maamuzi ya kishabiki. Wamekuwa wakisajili ama kuwaachana baadhi ya wachezaji bila sababu za msingi.
Mwanaspoti inakuletea orodha ya mastaa ambao Simba na Yanga ziliachana nao kimakosa. Timu hizi zilipaswa kufanya jitihada binafasi kuwabakisha klabuni hapo kutokana na umuhimu wao.
Frank Domayo, Yanga
Yanga ilikosea kuachana na kiungo, Frank Domayo wakati akiwa kwenye ubora wake. Domayo, 22 aliondoka Yanga baada ya mkataba wake kumalizika msimu uliopita na kuamua kujiunga na Azam FC.
Wakati Domayo anaondoka Yanga, alikuwa kwenye kiwango cha juu na hata alipoondoka pengo lake lilionekana katika kikosi hicho. Licha ya kukaa nje kwa muda mrefu baada ya kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini mapema mwezi Julai mwaka jana bado nafasi yake pale Yanga ilikuwa wazi.
Domayo amerejea uwanjani kwa sasa na Jumanne ya wiki hii aliichezea Azam mechi yake ya kwanza ya mashindano na kuonyesha kiwango cha juu kilichomshtua kocha wa timu hiyo, Joseph Omog raia wa Cameroon.
Didier Kavumbagu, Yanga
Hapa Yanga ilibugi zaidi. Iliamua kuachana na mshambuliaji Didier Kavumbagu baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wakati straika huyo akiwa bado moto. Yanga haikuonyesha jitihada zozote za kuongeza mkataba wa mchezaji huyu raia wa Burundi hadi akajisajili Azam FC. Kavumbagu aliifungia Yanga mabao 10 msimu uliopita licha ya kukosa baadhi ya mechi kutokana na kuwa majeruhi. Straika huyo alitua Azam ambako anang’ara kwa sasa.
Kavumbagu tayari ameifungia Azam mabao matano kwenye mechi za ligi huku akiifungia mawili kwenye michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika Kigali Rwanda na bao lingine moja kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar. Kavumbagu ndiye aliyeifungia Azam bao moja katika sare ya mabao 2-2 na timu yake ya zamani Yanga kwenye mechi ya ligi.
Hamis Kiiza, Yanga
Hapa majibu hakuna. Kulikuwa na sababu gani ya Yanga kuachana na mshambuliaji Hamis Kiiza raia wa Uganda? Ni siasa tu. Kiiza aliifungia timu hiyo mabao 11 msimu uliopita huku akitengeneza mengine zaidi ya 10. Hakukuwa na swali juu ya kiwango cha mshambuliaji huyo.
Tatizo lilianza pale Kocha Mbrazili Marcio Maximo alipopewa kazi ya kuifundisha timu hiyo, kwani alipendelea zaidi kuwatumia viungo ili kucheza soka la kujilinda jambo lililofanya Kiiza aonekane si lolote kwenye kikosi hicho na baadaye Yanga kuamua kuachana naye kwenye usajili wa dirisha dogo. Hapa Yanga ilibugi. Hakukuwa na haja ya kumwacha Kiiza na kuhangaika kutafuta washambuliaji wengine hususan timu ilipoamua na kuachana na Maximo.
David Luhende, Yanga
Hapa Yanga ilikosea zaidi. Timu hiyo iliamua kuachana na beki wake wa kushoto David Luhende kwa sababu tu za kisiasa wakati kiwango chake uwanjani kilikuwa juu. Baada ya Yanga kuachana na Luhende iligundua kuwa haina beki mwingine wa kushoto wa kusaidiana na Oscar Joshua. Hapa Yanga ikaamua kumsajili beki wa JKT Ruvu, Edward Manyama ambaye ameshindwa kufiti moja kwa moja kwenye kikosi hicho.
Luhende aliamua kujiunga na Mtibwa Sugar ya Morogoro na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Hakika Yanga ilibugi na sasa inahaha tu kwani kiwango cha Oscar nacho ni cha kawaida mno.
Amissi Tambwe, Simba
Simba hapa ilibugi pengine zaidi ya timu zote baada ya kuamua kuachana na straika Mrundi Amissi Tambwe. Straika huyo aliibuka mfungaji bora wa msimu uliopita akiwa amefunga mabao 19 (tisa ya penalti) lakini baada ya mechi saba tu za msimu huu timu hiyo iliamua kumfungulia mlango wa kutokea. Aliyekuwa Kocha wa Simba, Patrick Phiri raia wa Zambia alidai kuwa Tambwe hawezi kufanya vizuri kwenye mfumo wake hivyo kuishia kumweka benchi.
Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga kwenye pambano la Mtani Jembe huku Tambwe akiwa benchi, ulionekana kuwapa kiburi watu wa Simba na kuamua kuachana na straika huyo ambaye alitua Yanga saa chache baadaye. Tambwe tayari ameifungia Yanga bao moja katika mechi tatu alizocheza huku akionekana kuwa na uchu wa kufunga zaidi na zaidi. Hapa Simba walibugi.
Kelvin Yondani, Simba
Beki Kelvin Yondani alimaliza mkataba wake na Simba baada ya kumalizika kwa msimu wa 2011/12 huku timu hiyo ikionekana kuwa kimya. Baada ya mazungumzo, viongozi wa Simba walimpa ahadi ya kumpatia mkataba mpya punde kabla ya msimu mpya kuanza.
Baada ya Yondani kuona Simba haina dhamira ya kumpatia mkataba mpya aliamua kujiunga na Yanga. Hapa Simba ilikurupuka kwani baada ya kuondoka kwa Yondani mambo yalionekana kwenda ndivyo sivyo kikosini hapo. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwani mbali na kuondoka kwa Yondani, timu hiyo pia ilimwondoa beki Juma Nyosso na kuifanya beki ya kati ya timu hiyo kuwa uchochoro.
Pengo la Yondani limeendelea kuitesa Simba hadi sasa kwani baada ya kuondoka tayari mabeki zaidi ya wanne wamesajiliwa na kushindwa kuziba nafasi hiyo wakati Yondani ameendelea kuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Yanga.
Salum Kanoni, Simba
Simba iliamua kuachana na beki wa kulia Salum Kanoni mwaka 2012 baada ya Said Nassoro ‘Chollo’ kuonyesha kiwango cha juu kikosini hapo. Simba haikuona umuhimu wa kuwa na Kanoni wakati Chollo tayari amejihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Hilo lilikuwa ni tatizo kwani hali ilibadilika baadaye kwani Chollo alikosa mpinzani wa kiwango chake na alipoanza kusumbuliwa na majeraha eneo la beki hiyo ya kulia liligeuka kuwa uchochoro. Simba ikaanza kuhaha kutafuta beki mwingine wa kuziba nafasi hiyo.
Msimu huu imemsajili Hassan Kessy kutoka Mtibwa Sugar kwa Sh 30 milioni pamoja na kumtoa beki Miraji Adam akacheze kwa mkopo klabuni hapo kama sehemu ya uhamisho huo. Kanoni bado ameendelea kutamba ligi kuu akiwa na kikosi cha Kagera Sugar huku baadhi ya viongozi wa Simba wakionekana kummezea mate.
Juma Kaseja, Simba
Yawezekana Simba walikuwa na hoja juu ya kipa Juma Kaseja lakini haikuwa wakati muafaka kuachana naye. Kwa kifupi ni kwamba walistahili kuachana naye lakini hawakujiandaa kwa ajili ya hilo. Ilikuwa hivi, Simba iligoma kumwongezea mkataba Kaseja baada ya ule wa awali kumalizika baada ya msimu wa 2012/13 na kuamua kumsajili kipa Mganda Abel Dhaira ili kuziba pengo lake.
Hapa walibugi. Dhaira alikuja na kucheza kwa nusu msimu pekee. Kiwango chake kilionekana kuwa duni. Baada ya kuachana na kipa huyo Simba iliamua kuwasajili makipa wa zamani wa Yanga, Yaw Berko na Ivo Mapunda ili kuimarisha lango lao jambo ambalo limeonekana pia kufeli. Berko alichemka na kuondoka tu baada ya nusu msimu,
Mapunda amekuwa akilaumiwa kuwa anafungwa mabao mepesi. Viongozi wa Simba wenyewe wanajua kuwa walibugi kuachana na Kaseja. Kwenye usajili wa dirisha dogo mwezi uliopita viongozi wa Simba walipambana kumrejesha Kaseja lakini jitihada zao ziligonga mwamba kutokana na kuwa na mkataba na Yanga.