Simba yakaa kwenye akili ya Chama

Muktasari:
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama ndiye mchezaji anayeonekana kubeba majukumu ya ushindi wa Simba kwa sasa.
Dar es Salaam. Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama ndiye mchezaji anayeonekana kubeba majukumu ya ushindi wa Simba kwa sasa.
Simba, ambayo inatakiwa kushinda dhidi ya FC Platnum ya Zimbabwe Januari 6, itamhitaji zaidi kiungo huyo wa kimataifa wa Zambia kuwa fiti kwa asilimia 100.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walichapwa bao 1-0 na miamba hiyo ya Zimbabwe katika mchezo wao wa kwanza waLigi ya Mabingwa Afrika wakisaka nafasi ya kutinga makundi.
Lakini Simba inaonekana kuwa mabegani mwa Chama kutokana na kuapata tabu katika michezo ya hivi karibuni.
Kiungo huyo mwenye mabao sita ya Ligi Kuu na pasi sita za kufunga amekuwa msaada mkubwa kwa Simba msimu huu, lakini zaidi katika mechi nne zilizopita, ambazo Simba imeonekana kupata tabu.
Katika mechi tatu za Ligi Kuu, Chama alianza kuonyesha umuhimu wake kikosini baada ya kuingia kipindi cha pili dhidi ya Polisi Tanzania na kufunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa Wekundu wa Msimbazi wa mabao 2-0.
Kiungo huyo pia alitoa pasi ya bao kwenye mchezo uliofuata dhidi ya Mbeya City lililofungwa na John Bocco, wakati Simba ikishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mchezo uliofuata wa Ligi Kuu ulikuwa dhidi ya KMC, ambao Simba ilishinda bao 1-0 kwa mkwaju wa penalti ya Meddie Kagere.
Lakini kimataifa, hadi sasa Simba imecheza mechi tatu, mbili dhidi ya Plateau United ya Nigeria na ile dhidi ya Platnum ya Zimbabwe.
Simba imeshinda bao moja pekee katika mechi hizo tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika, ambalo pia limefungwa na Chama nchini Nigeria.
Safu ya ushambuliaji ya Simba imeonekana kuwa na uhai kama Chama atakuwa katika kiwango chake muda wote wa mchezo.
Licha ya kuwa na nyota kama Kagere, Bocco, Chris Mugalu na Luis Miquessone, Simba bado inaonekana si bora sana kuliko inapokuwa na fundi huyo kutoka Zambia.
Na sasa, ikiwa haijafunga bao lolote katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba inahitaji ushindi wa nyumba unaozidi bao moja ili kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo makubwa Afrika.
Ni wazi kuwa kikosi cha kocha Sven Vandebroeck kitakuwa na mlima wa kupanda kutokana na kiwango chao cha sasa kuanza kuzua mawali.
Sven alisema ana uhakika kuwa kama kikosi chake kitacheza katika kiwango chao wanaweza kupata ushindi wa nyumbani wa kuwavusha katika hatua inayofuata.
Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema mchango wa Chama katika kikosi cha Simba ni mkubwa na amekuwa na uwezo wa kutoa pasi sahihi kwa wakati sahihi uwanjani.
“Ila ninachokiona katika mechi ya marudiano na Platinum, wapinzani wanaweza kuja wakiwa wamejipanga kumdhibiti kama walivyofanya kwa Luis Miquissone kwenye mechi iliyopita.
“Kwani katika soka wapinzani huwa wanawasoma wenzao wanafanyaje kufunga mabao, wanaweza kuja wamejipanga kumdhibiti pia Chama, hivyo ili wafanikiwe kwenye marudiano, Simba inaweza kucheza kwa kushambulia kwa pamoja na kukaba kwa pamoja.
Kipa wa zamani wa Simba, Mosses Mkandawile alisema mchango wa Chama kwenye kikosi cha Simba unaonekana kwani ni mchezaji mwenye uwezo wa kumiliki mpira, akautuliza na kisha kutoa pasi sehemu husika kwa wakati.
“Chama asipokufunga, basi atatoa pasi ya bao, amekuwa na mchango mkubwa, ingawa katika mechi ya marudiano na Platinum kuna uwezekano wapinzani wetu wakaja na ‘aproch’ ya kumdhibiti, hivyo kocha kama ataweza angetumia mbinu ya kutafuta mabao kupitia pembeni,” alisema Mkandawile.