Shikhalo: Nabi ndiye kaning'oa Yanga

YANGA imeanza maisha mapya ikiwa Morocco, bila ya kipa Faruk Shikhalo, aliyemaliza mkataba wake wa miaka miwili Jangwani na kusepa zake kurudi kwao Kenya.

Kipa huyo alioyesajiliwa na Yanga mwaka 2019 akitokea Bandari Kenya, kwa sasa ni mchezaji huru, lakini hadi anaondoka Jangwani alikuwa ni chaguo la kwanza katika timu hiyo licha ya mabadiliko ya mara kwa mara na kipa mwenzake Metacha Mnata aliyetemwa pia klabuni hapo.

Siku chache tangu aondoke Yanga, Mwanaspoti lilimtafuta na kufanya mahojiano maalum naye, kwa lengo la kutaka kujua maisha yake kabla na baada ya kuondoka kwa mabingwa hao wa kihistoria, huku akifichua tatizo kubwa lililomng’oa Jangwani ni Kocha Nasreddine Nabi.

Kama unakumbuka Yanga ilipotangazwa tu kuwa kipa huyo anaondolewa mashabiki walipokea kwa hisia tofauti wakiona bado alistahili kupewa muda zaidi. Ebu msikie mwenyewe anachokisema...!


MAISHA YA YANGA

Shikhalo anasema maisha ndani ya Yanga kwa ujumla yalikuwa ni mazuri na anamshukuru Mungu amefurahia kipindi chote cha miaka miwili aliyohudumu katika timu hiyo huku akiwashukuru wachezaji, makocha na viongozi wote aliowahi kufanya nao kazi kwa pamoja.

Shikhalo anasema anawashukuru makipa wote wawili kwa sababu wana viwango vya hali ya juu na wote ni makipa wa timu ya Taifa na uwepo wao uliongeza ushindani na kila mmoja kujituma zaidi ili kupata nafasi ya kucheza na kuleta manufaa kwa ajili ya timu.

“Ushindani ulikuwa mkubwa ukiangalia Metacha ni kipa wa timu ya Taifa na anachezea klabu kubwa, lakini Kabwili amekuwa akiitumikia timu ya taifa ya vijana, ndio maana kila kipa aliyekuwa anapewa nafasi alikuwa anaonyesha kiwango kizuri na kuleta utofauti kwa kila mmoja wetu,” anasema Shikhalo.

Juu ya kushindwa kwake kuwika mwanzoni anasema ilitokana na ugeni wake, lakini anamshukuru Mungu maana mwaka wake wa pili alianza taratibu kuzoea mazingira na kufanya vizuri, huku makipa aliowakuta wakiwa ni wazoefu wa soka la Tanzania.

Kuhusu kutemwa, Shikhalo anakiri alitegemea kuondoka Yanga kwa sababu hakuna chenye mwanzo kikakosa mwisho ingawa binafsi alitamani kuendelea kuitumikia timu, lakini tatizo likiwa nio kocha wake, Nasreddine Nabi.

Shikhalo anawashukuru viongozi wa Yanga kwa sababu wamekuwa wawazi kwake kwa kuwa mwanzo kulikuwa na utata kuhusu hatima yake lakini viongozi walimwambia wazi kuwa kutokana na mapendekezo ya kocha, aliyewaambia hawawezi kumuongezea mkataba mpya.


UHUSIANO NA NABI

Anasema uhusiano wake na kocha Nabi ulikuwa mzuri sana hivyo hawezi kulaumu kwa kilichotokea kwa sababu wamefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.

“Tumekuwa tukishirikiana sana mimi na kocha (Nabi) lakini mwisho wa msimu niliwafuata viongozi na kuzungumza nao, wakaja kuniambia kwamba kocha ana mipango yake na jina langu halipo katika akili yake kwa msimu ujao, hivyo naheshimu uamuzi wake ila Yanga ni klabu yangu nimefurahi jinsi mashabiki walipokuwa nami wakati wote, hawa ndio watu nitakaowakumbuka, hata siku nikiambiwa nirudi nitafanya hivyo kwa ajili yao,” anasema Shikhalo aliyezaliwa Desemba 10, 1996.

Kuhusu tofauti na soka la Kenya na Tanzania, Shikhalo anasema kwa miaka miwili au mitatu Ligi Kuu Bara imekuwa bora na yenye ushindani tofauti na ile ya Kenya ambayo imekuwa na changamoto ya kusimama mara kwa mara kutokana na janga la corona, ila pia hata uwekezaji wa soka la Bongo umekuwa mkubwa.

“Ligi ya Tanzania imekuwa bora ukilinganisha na ile ya Kenya, ukiangalia uwekezaji kwenye ‘TV Right’ (haki za matangazo ya Television) kwa miaka hii miwili linadhihirisha hilo licha ya kutopishana kwa kiasi kikubwa kwenye ushindani,” anasema.

Suala la viwango limemgusa Shikhalo kwa kiasi kikubwa akisema Tanzania ina viwanja vingi ila havishughulikiwi hivyo vinapaswa kuboreshwa zaidi.

“Tanzania imebarikiwa viwanja vingi na kama vitatuzwa na kunyunyuziwa maji naamini vitakuwa bora zaidi tofauti na vilivyokuwa kwa sasa,” anasema.

Juu ya panga pangua ya ratiba ya Ligi Bara anasema suala la kupanguliwa ratiba mara kwa mara linapaswa kutafutiwa ufumbuzi ila hawezi kulaumu sana japo viongozi wa TFF wanapaswa kulishughulikia hilo.


KARIAKOO DABI

Katika kipindi cha miaka miwili alichohudumu Yanga, Shikhalo anasema ladha ya Dabi haijawahi kupotea kwa sababu amekuwa akiifuatilia tangu akiwa nyumbani kwao Kenya katika timu yake ya Bandari.

“Dabi ni ile ile inakuwa na ushindani mkubwa na ni sehemu kama mchezaji ya kuonyesha thamani yako katika mechi za namna hiyo,” anasema kipa huyo aliyezichezea timu saba tofauti zikiwamo Muhoroni Youth, Posta Rangers, Tusker, KRA, Talanta na Bandari Kenya.

Shikhalo anasema siku zote mechi ya Dabi imekuwa na presha kubwa, hasa kutoka kwa mashabiki kwani kila shabiki ana matarajio yake, hivyo kama mchezaji inamuweka katika wakati mgumu wa kuhakikisha anakuwa na kiwango bora na kuongeza umakini mkubwa ndani ya uwanja.

Anasema kuwa mechi ya kwanza iliyoisha kwa sare ya 2-2, ndio ilikuwa mechi yake nzuri kwani alionyesha kiwango kizuri, licha ya kabla ya mechi kuingiwa na wasiwasi mkubwa kutokana na mashabiki kuwa wengi uwanjani ingawa kwa upande wa Yanga walikuwa wachache kuliko wa Simba.

“Kilichonisaidia katika ile mechi ni uzoefu wangu, namshukuru mwalimu wangu Manyika (Peter, aliyekuwa Kocha wa Makipa wa Yanga wakati huo), kwanialikuwa ametufanyisha mazoezi na kutujenga vizuri kisaikolojia, hivyo nilikuwa tayari kwa ajili ya mapambano,” anasema.


BOCCO NA KAGERE

Katika miaka miwili aliyocheza Tanzania, Shikhalo amekutana na washambuliaji mbalimbali bora, baadhi akiwajua majina na wengine hawajui, lakini alikuwa akiongeza umakini kwa wale ambao aliujua mziki wao uwanjani kwa nia ya kuepuka aibu.

Anasema kati ya wote, pacha iliyokuwa ikimnyima raha ni ile ya John Bocco na Meddie Kagere wa Simba na kufafanua; “Pacha ya Bocco na Kagere ilikuwa ikiniumiza kichwa ninapokutana nayo hivyo najikuta nikifanya mazoezi sana na kuongeza umakini mkubwa, lakini pia hata kwa Prince Dube wa Azam FC licha ya kuwa alikuja baadae,” anasema.

Kipa huyo anazungumzia pia pambano lao la kwanza kupoteza katika msimu uliopita dhidi ya Coastal Union kule Tanga yeye akiwa langoni na kueleza jinsi alivyoumizwa na matokeo ya mchezo ule ukizingatia walitoka umbali mrefu bila kupoteza.

“Malengo ya mchezaji mkubwa ni kutwaa mataji na kuacha kumbukumbu katika timu ambayo umeitumikia na kama uliona tulianza na moto kila mmoja akitaka kushinda taji hivyo ilikuwa ni kipindi kigumu ambacho nilipitia kwa sababu nilikuwa na malengo ya kuisaidia timu yangu ila ilishindikana na siku ile nakumbuka nilishindwa kula chakula kwa sababu ukiangalia bao la kwanza nilikuwa na uwezo wa kuokoa japo nilishindwa kufanya hivyo,” anasema.

Shikhalo anaongeza licha ya Kombe la Mapinduzi kutokuwa kubwa kivile ila anajivunia kulichukua kwa sababu lina hadhi yake nchini na anashukuru katika maisha yake kuisaidia Yanga, japo hajaweza kufanya makubwa zaidi kama alivyotegemea kutokana na kutoongezwa mkataba.


KUAGA MASHABIKI

Shikhalo anafichua alipotangazwa kuachwa na Yanga, aliandika ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) katika mtandao wa kijamii wa Instagram kuaga na kukiri ilimchukua masaa mawili kuiandika.

“Mashabiki wamesimama nami katika matatizo mbalimbali, hivyo ni watu ambao watakuwa na sehemu yao binafsi ndani ya moyo wangu,” anasema.

Anasema soka la Tanzania unachezwa Instagram, nje na ndani ya uwanja kwani mashabiki wanazipenda timu zao na kuzifuatilia mpaka kwenye mitandao ya kijamii, hivyo inakupaswa kujiandaa kiakili maana ipo siku unaweza ukafanya vibaya au vizuri kwa hiyo unapaswa kujiandaa na mapokezi ya mashabiki.

“Binadamu hatujakamilika hivyo watu wanapokuambia umekosea unapaswa kufanyia kazi madhaifu yako,”

Juu ya panga pangua ya makocha ndani ya Yanga, Shikhalo anasema kinakuwa na athari chanya au hasi kwani kila mwalimu anayekuja huja na wachezaji wake ambao anataka kufanya nao kazi tofauti na waliopo lakini pia anaingiza upya falsafa zake.

Mkenya huyo pia alizungumzia ishu za ushirikina, anasema anausikia tu, ila hana uhakika kama upo na juu ya tetesi kuwa hakuwa na maelewano mazuri na Metacha anasema hilo halina ukweli, kwani kwa miaka miwili aliokuwa Yanga amefanya naye kazi vizuri na kuna wakati kulikuwa hakuna kocha wa makipa hivyo wao wenyewe walikuwa wanafundishana mazoezi.


NJE YA YANGA

Alipoulizwa baada ya kuondoka Yanga nini mipango yake na kudai anaenda kupumzika kwa sababu ana miezi tisa hajaenda nyumbani kwao, kisha baada ya hapo ndipo atajua kitakachofuata ila yupo tayari kufanya kazi popote kwa sababu ni sehemu ya maisha yake.

Shikhalo aliyekuwa kipa bora kwa misimu miwili akiwa na Bandari amekuwa akikosekana kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Star’ na sababu kubwa iliyochangia, anasema ni kutopata nafasi ya kucheza mwanzo kwenye kikosi cha kwanza ndicho kilichomtoa Harambee ila anamini atarejea tena.

Anasema amekuwa kwenye soka kwa muda mrefu na amejionea mashabiki wa Tanzania wakizipenda timu zao hali ambayo inawafanya kujitolea kwenye jambo lolote linalohusu klabu zao, huku akiongeza kwa kusema kitu asichokisahau ni jinsi viongozi na mashabiki wa Yanga walivyomtendea wema katika miaka yake miwili aliyokuwa hapa Tanzania.

Kuhusu utofauti wa maisha ya kawaida Tanzania na Kenya, Shikhalo anasema kuwa hakuna tofauti kubwa kwani maisha ya ukanda huu wa Afrika mashariki na kati yanafanana kwa kiasi kikubwa labda kwenye suala la lugha ya kiswahili.


USAJILI MPYA

Yanga imekuwa ikisajili majembe mapya baada ya kina Shikhalo na wenzake kutemwa, naye anasema hawezi kuzungumzia sana kuhusu usajili, ila kutokana na majina ambayo yamesajili ni wachezaji wazuri kwa sababu kuna baadhi yao amecheza nao na wengine alipishana nao wakati anakuja Yanga.

“Makambo tumepishana nikija yeye anaondoka, lakini kapita Yanga na kafanya vizuri sana na kwa sababu anaijua ligi ya Bongo, hivyo Yanga wamepata mtu sahihi, kuhusu Aucho sina Doubt (mashaka) kuhusu kiwango chake kwani namjua tangu akiwa Tusker Kenya, naamini wamefanya usajili mzuri utakaowasaidia.”

Alipulizwa anaweza kurudi tena nchini kucheza, Shikhalo bila kumung’unya maneno anasema anaamini ipo siku atarudi kucheza Tanzania kwani haya ni maisha na lolote linaweza likatokea kwani anaweza pia kurudi kucheza Yanga au kufanya kazi nyingine nchini.

Shikhalo anasema hawezi kusema angecheza timu gani kwa sababu haya ni maisha na popote anaweza kucheza kwa sababu soka ni kazi yake hivyo kikubwa ni maelewano mazuri baina ya pande zote mbili.

Kuhusu ushindani wa viungo Mukoko Tonombe na Khalid Aucho, Shikhalo anasema bato yao itakuwa nzuri sana kwani timu inapokuwa na wachezaji wazuri katika nafasi moja hakuna mchezaji anayetaka kukaa nje na kumpa wakati mgumu mwalimu kuamua kubadilisha mfumo ili kupata kitu bora zaidi kama anahitaji kuwatumia wote.

“Ukiangalia kocha Nabi anapenda kutumia viungo wawili wakabaji, ndio sababu ameamua kumsajili Aucho kutokana na falsafa zake,” anasema na kufichua ni yeye aliyuechangia Aucho kuja Yanga.

Shikhalo anasema alizungumza na Aucho na kumuambia kuwa Yanga itampa Exposure (Mwanga) anayotaka, kwani ni timu yenye mashabiki wenye upendo na ni timu yao.