Sababu ya Ronaldo kurudi EPL hii hapa
TURIN, ITALIA. LISEMWALO lipo. Manchester United imeripotiwa kuwasilisha maombi rafiki ya kumsajili Cristiano Ronaldo kwa wakala wake Jorge Mendes.
Man United inataka kumrudisha Ronaldo uwanjani Old Trafford, ikiwa ni miaka 11 tangu alipoondoka kwenda Real Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwa wakati huo, Pauni 80 milioni.
Akiwa na umri wa miaka 35, Ronaldo anahusishwa na mpango wa kuachana na Juventus baada ya miamba hiyo ya Italia kutaka kujinasua na kasheshe la kulipa mshahara wa Pauni 28 milioni wanazomlipa kwa mwaka.
Gazeti la Ureno la Record, kupitia SportWitness, ambalo lilikuwa la kwanza kuripotiwa Ronaldo anakwenda Real Madrid mwaka 2009 na kila kitu kilivyofanyika sasa linaripoti kuhusu ofa ya Man United iliyotumwa kwa Mendes kwa ajili ya huduma ya mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or. Janga la corona linaripotiwa kuzivuruga timu kibao kiuchumi huko Ulaya na hilo ndilo linaloifanya Juventus kutaka kupunguza bili ya mishahara kutokana na Ronaldo kulipwa zaidi ya mara tano ya mchezaji anayefuatia kwa mshahara mkubwa kwenye kikosi hicho, Paulo Dybala. Mkataba wa sasa wa Ronaldo utakwisha 2022. Na kuna taarifa zinadai kwamba Ronaldo anataka kurudi Man United kwa ajili ya Lionel Messi. Kinachoelezwa ni kwamba Messi anahusishwa na mpango wa kwenda Manchester City, hivyo Ronaldo anataka kurudi Man United ili kuhamishia upinzani wa wakali hao wawili kutoka kweye El Clasico hadi kwenye Manchester derby.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari Christian Martin, mabosi wa Man United tayari wameshaanza mazungumzo na wenzao wa Juventus kwa ajili ya mshambuliaji huyo.
Kupitia El Grafico, Martin alifichua kile kinachomfanya Ronaldo atake kwenda England.
Kinachoaminika kwa sasa mkataba wa Messi utakapofika tamati mwishoni mwa msimu huu huko Barcelona atakwenda Etihad kuungana na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola.
Kutokana na Messi kuwa na mpango wa kwenda Etihad, hilo ndilo linalomfanya Ronaldo kutaka kurudi Old Trafford ili kuibua upya upinzani wa mastaa hao wawili.