Ronaldo kapita nao wote
Muktasari:
Katika kipindi chake cha ujana, Ronaldo, 35, alijikuta akiangukia kwenye mikono ya warembo wengi matata, wakiwamo wale maarufu na waliojijengea sifa kubwa kwenye jamii. Hizi hapa vurugu za Ronaldo na orodha ya wanawake waliwahi kupita kwenye mikono yake.
LISBON, URENO . KABLA Cristiano Ronaldo hajatulizana na mrembo Georgina Rodriguez, alikuwa moto, akifahamika kama ‘mzee wa totoz’.
Katika kipindi chake cha ujana, Ronaldo, 35, alijikuta akiangukia kwenye mikono ya warembo wengi matata, wakiwamo wale maarufu na waliojijengea sifa kubwa kwenye jamii. Hizi hapa vurugu za Ronaldo na orodha ya wanawake waliwahi kupita kwenye mikono yake.
GEMMA ATKINSON
Kwa kipindi cha miezi minne 2007, Gemma na Cristiano walikuwa gumzo na kuwa pamoja kipindi hicho alipokuwa Manchester United.
Hata hivyo, uhusiano wao haukudumu kwa muda mrefu na sasa mrembo Gemma anafurahia mahaba na mwanamume mwingine, Gorka Marques, ambapo wamefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike, Mia. Muda mfupi Ronaldo aliokuwa na Gemma, aliutumia kwa mikoto kibao ya kifahari nyakati za usiku.
PARIS HILTON
Baada ya mrembo Paris kuachana na mpenzi wake, Doug Reinhardt, mrembo huyo wa Los Angeles kutokea familia ya kitajiri aliangukia kwenye penzi la Ronaldo, na walitumia mapumziko ya majira ya kiangazi 2009 wakiwa pamoja huko California. Wawili hao walipigwa picha mara kadhaa wakiwa pamoja katika kumbi za starehe za usiku. Baadaye iliripotiwa Paris alimtema Ronaldo kwa sababu hakuwa akimwelewa.
KIM KARDASHIAN
Mwaka 2010, kabla ya Kanye West na Kim kuanzisha uhusiano, mrembo huyo maarufu kwenye televisheni alifurahia mitoko kadhaa na Ronaldo. Wawili hao waliripotiwa kubusiana huko kwenye Jiji la Madrid na kwenda kula bata kwa siku tatu mfululizo. Wadau wa maana walitamani uhusiano wa Kim na Ronaldo ungedumu kwa muda mrefu kwa sababu lingekuwa jibu la penzi maarufu la David Beckham na Victoria Beckham, Posh.
IRINA SHAYK
Inawezekana ukawa umesahau, lakini Ronaldo aliwahi kuwa kwenye uhusiano na mrembo mwanamitindo wa Russia, Irina Shayk kwa miaka mitano. Wawili hao walikuwa pamoja kuanzia 2010 hadi 2015 kabla ya kila mmoja kuchukua njia zake. Baada ya hapo Irina aliangukia kwenye penzi na staa wa Hollywood, Bradley Cooper na wamefanikiwa kupata mtoto wa kike anayeitwa Lea. Hata hivyo, Irina na Cooper waliachana 2019.
IMOGEN THOMAS
Mrembo Imogen, aliyewahi kushiriki shindano la Big Brother, aliwahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Ronaldo mwaka 2006. Wawili hao walikuwa kwenye mahaba mazito na baada ya kuachana walikuja kukumbushia uhusiano wao mwaka 2011. Hata hivyo, msemaji wa mrembo Imogen, alikanusha wawili hao kurudiana huku akisema, Ronaldo alikuwa akimpigia simu Imogen muda wote kuomba warudi kwenye mapenzi yao kama zamani.
DESIREE CORDERO
Mwaka 2016, mrembo Desiree na Ronaldo walikuwa maarufu kwenye vyombo vya habari baada ya kuripotiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi. Lakini, Ronaldo baadaye alimtuhumu mrembo Desiree kuwa alikuwa akilazimisha umaarufu, hivyo wakaachana haraka. Mrembo huyo wa Kihispaniola kwa sasa yupo kwenye mapenzi motomoto na staa wa Lazio, Joaquin Correa. Uhusiano wa Desiree kwa Ronaldo ulikuwa wa muda mfupi sana.
JORDANA JARDEL
Mwanamitindo wa Kibrazili, mrembo Jordana ndiye aliyekuwa mwanamke wa kwanza kabisa kuwa kwenye uhusiano siriazi na Ronaldo baada ya kuwa mwanasoka wa kulipwa. Jordana alikuwa dada wa mchezaji mwenzake Ronaldo huko Sporting Lisbon, Mario Jardel. Wawili hao walikuwa kwenye mapenzi matamu mwaka 2003 na kisha wakaachana, kila mmoja akishika njia zake. Baada ya hapo, Ronaldo alienda zake Manchester United, alikokwenda kuwa maarufu zaidi duniani.
MERCHE ROMERO
Staa Ronaldo alikuwa kwenye mapenzi na mrembo mtangazaji wa televisheni na mwanamitindo, Mreno Merche kwa zaidi ya mwaka mmoja kati ya 2005 na 2006. Mrembo Merche, ndiye aliyefanikiwa kudumu na Ronaldo kwa muda mrefu katika kipindi chake alichokuwa akiichezea Man United huko Old Trafford. Hata hivyo, walikuja kuachana kwa kuwa hawakuweza kumudu uhusiano wa mbali, mmoja akiwa Ureno na mwingine England.
NEREIDA GALLARDO
Kabla hajahamia Real Madrid, mwanamitindo wa Kihispaniola, mrembo Nereida Gallardo alinasa kwenye penzi la Ronaldo na kufurahia mitoko kadhaa wakiwa pamoja. Hata hivyo, uhusiano huo haukudumu kwa muda mrefu na kuachana huko mrembo huyo aliyekuwa akisomea unesi wakati huo kusema kwamba, hakuwa akipendezwa na nguo za ndani za Ronaldo. Nereida aliwahi kuhusishwa pia kuwahi kuwa kwenye uhusiano na staa mmoja wa Real Madrid kabla ya Ronaldo kutua kwenye timu hiyo.
LUANA BELLETTI
Mwaka 2009, beki wa Chelsea, Juliano Belletti alijaribu kumkutanisha dada yake na swahiba wake, Ronaldo. Jambo hilo likasababisha kuanza kwa uhusiano baina ya wawili hao, Ronaldo na Luana. Hata hivyo, penzi hilo halikudumu sana na kila mmoja akachukua njia zake akiendelea na mambo yake. Luana kwa sasa ni mbunifu wa mitindo na mtu wa staili mbalimbali za mavazi akijipatia kipato na umaarufu kupitia tasnia hiyo.
LUCIA VILLALON
Muda mfupi tu baada ya kuachana na Irina, Ronaldo aliangukia katika penzi la mrembo Lucia. Mrembo huyo wa Kihispaniola, ambaye alikuwa mtangazaji wa televisheni hakudumu sana na Ronaldo hivyo wakaachana. Miezi ya mwanzoni tu mwa mwaka 2015, penzi hilo lilovunjika huku familia ya Ronaldo ikisema kwamba, hakukuwa na kitu kama hicho kwa maana ya kukanusha Ronaldo na Lucia hawajawahi kuwa wapenzi.
SORAIA CHAVES
Mrembo Soraia ni mwigizaji anayeheshimika sana huko Ureno. Mrembo huyo aliangukia kwenye penzi la Ronaldo mwaka 2006, kabla ya Soraia hajapata umaarufu zaidi kwa kuigiza kwenye filamu ya Call Girl. Filamu hiyo iliuza sana Ureno mwaka 2007. Hata hivyo, penzi la wawili hao halikudumu kwani, kipindi hicho Ronaldo alipokuwa Man United alikuwa na mambo mengi kwelikweli.
KARINA FERRO
Huko nyuma, 2002, mwanamitindo wa Kireno, mrembo Karina, aliripotiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Ronaldo. Wawili hao waliwahi kupigwa picha wakiwa pamoja ufukweni katika mapozi ambayo hayakuhitaji maelezo mengi kujua kwamba, wawili hao kuna kitu kinaendelea kati yao. Hata hivyo, penzi hilo nalo halikuwa na muda mrefu sana likafa. Karina akaingia kwenye orodha ya wanawake waliowahi kutoka na staa wa Juventus, Ronaldo.
BIPASHI BASU
Mwaka 2007, mwanamitindo wa Kihindi na mwigizaji, Basu alipigwa picha akionekana kwenye jambo fulani na Ronaldo. Ronaldo mwenyewe alikiri kuvutiwa na mrembo huyo na kuna kitu baina yao. Baada ya kukutana mara kadhaa, Ronaldo na Basu wanaripotiwa kuendelea kuwa marafiki hadi sasa. Hiyo ndio orodha ya wanawake waliopamba maisha ya Ronaldo kabla ya kukutana na mrembo, Georgina, ambaye ameamua kufanya naye familia.