Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moallin akataa visingizio Yanga, ataka pointi tatu kwa Azam

Muktasari:

  • Moallin amesema kikosi chake kinalazimika kujiandaa haraka iwezekanavyo kutokana na ratiba yenye msongamano mkubwa wa mechi hasa kipindi hiki cha kumalizia msimu.

KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, amesema ingawa kuna sababu nyingi ambazo zingeweza kutolewa kama visingizio kutokana na mfululizo wa mechi zinazochezwa kwa muda mfupi, lakini yeye anapendelea kuelekeza nguvu zake katika kuandaa wachezaji vizuri zaidi badala ya kutafuta visingizio.

Moallin amesema kikosi chake kinalazimika kujiandaa haraka iwezekanavyo kutokana na ratiba yenye msongamano mkubwa wa mechi hasa kipindi hiki cha kumalizia msimu.

Ameeleza kuwa, hata hivyo hali ndani ya kikosi hicho ni nzuri na hakuna majeruhi wapya, jambo linalowapa nafasi ya kuwa na kikosi kamili kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni.

Amesisitiza kuwa, nyakati hizi zikiwa zimebaki mechi tatu kumaliza msimu, kila mechi iliyosalia ni kama fainali kwao kwa sababu bado wanapambana kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo amesema kesho wanatarajia kukutana na timu yenye ubora mkubwa na wachezaji wazuri, hivyo wamefanya uchambuzi wa mechi za wapinzani wao ili kupata taarifa muhimu zitakazowasaidia kujiandaa na kushinda.

"Tunaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili, na hilo linatupa nguvu ya kuendelea kusukuma mbele hadi mwisho wa msimu," amesema Moallin wakati ambao Yanga ipo kileleni na pointi 66 ikiiacha Simba nafasi ya pili na pointi 64, kisha Azam inazo 58.

"Ligi imekuwa na ushindani mkubwa zaidi na imekuwa ya kimkakati zaidi. Pamoja na maendeleo hayo yote, bado tunaongoza ligi huku kukiwa na mechi chache tu zilizobaki," amesema.

Kuhusu uwezekano wa kufanya mabadiliko kesho katika kikosi kutoka kile kilichofungwa 3-2 na Azam hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, amesema uamuzi huo utategemea hali ya wachezaji baada ya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo.

Kwa niaba ya wachezaji, beki wa kushoto wa Yanga, Mohamed Hussein amesema jukumu lao kesho ni kupambana uwanjani kupata alama tatu.

"Sisi kama wachezaji jukumu letu la kesho ni kuhakikisha kwamba tunapambana kuweza kupata alama tatu. Niseme tu sisi kama wachezaji hatuna presha yoyote kwa sababu tunaamini ndani ya uwezo wetu na mafunzo tunayopewa na walimu wetu.

"Ni kweli tumetoka kucheza na mpanzani huyu katika mashindano tofauti na tumepoteza, lakini niseme tu kwamba ile kama wachezaji imetupa funzo kwa mchezo huu wa kesho ambao hatupo tayari kukosa alama tatu," amesema Hussein.

Yanga imebakiwa na mechi tatu za kumaliza msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo ikitoka kucheza na Azam kesho, Juni 27, 2026 itakuwa nyumbani kuikaribisha TRA United, kisha Juni 30, 2026 itamaliza kwa kuikabili JKT Tanzania ugenini.

Ili kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao Yanga imeuchukua kwa misimu minne mfululizo, Yanga inatakiwa kushinda mechi hizo tatu zilizobaki bila ya kuangalia matokeo ya wapinzani wake.

Kuelekea mechi ya kesho dhidi ya Azam, Yanga inaingia ikiwa na rekodi nzuri msimu huu ikiwa Zanzibar kwani imeshinda zote mbili ikianzia fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba, kisha 2-1 ikiwa nusu fainali ya Kombe la Muungano iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.