Rock Solution yaanza kibabe Ligi ya Mikoa

Kocha wa Bweri FC, Ezekiel Samson (kushoto) akizungumza na wachezaji wake baada ya kufungwa mabao 2-1 na Rock Solution katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Muktasari:
- Kundi D ambalo mechi zake zinachezwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza lina timu saba ambazo ni Rock Solution (Mwanza), Bweri (Mara), Mambali (Tabora), Leo Tena (Kagera), Kandahari (Kigoma), Bukombe Kombaini (Geita) na Friends Rangers (Dar es Salaam).
LIGI ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) Tanzania Bara, imeanza leo katika mikoa minne, huku katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza wenyeji Rock Solution wakianza vyema kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bweri FC ya mkoani Mara.
Wataalamu hao wa miamba wamepata ushindi katika mchezo pekee wa ligi hiyo ambao umechezwa kuanzia saa 10:30 jioni katika Uwanja wa Nyamagana na kuvuna pointi tatu ambao zinawafanya waongoze kundi D lenye timu saba.
Rock Solution ambayo inawakilisha Mwanza baada ya bingwa wa mkoa huo kukumbwa na ukata, imepata mabao kipindi cha pili yakifungwa na Yusuph Mohamed dakika ya 46 na Peter Timoth dakika ya 65, huku Bweri wakipata bao la kufutia machozi dakika ya 74 baada ya beki wa Rock, Mudrik Salum kujifunga.
Akizungumzia ushindi huo, Kocha wa Rock Solution, Robert Magadula amesema wamepata ushindani mgumu kutoka kwa Bweri FC ambao waliwabana kipindi cha pili, lakini akawapongeza wachezaji wake akiwatetea kuwa mchezo wa kwanza wa mashindano unakuwa mgumu kwa sababu timu zinakuwa zimekamia.
"Mechi ilikuwa nzuri na ngumu kwa sababu ni mechi ya kwanza lakini mechi imependeza na wapinzani wameonyesha ushindani, tunashukuru tumeanza vizuri tunakwenda kuongeza nguvu tuendelee kufanya vizuri," amesema Magadula
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Bweri FC, Ezekiel Samson amesema mabeki wake wamemuangusha kwa kuruhusu mabao mawili ya haraka kipindi cha pili, huku akiahidi kwenda kurekebisha makosa mazoezini ili wafanye vizuri mchezo ujao.
"Vijana wangu wamejitahidi wamecheza vizuri nawapongeza wapinzani wetu nadhani sisi tulizubaa dakika za mwanzo kipindi cha pili, nakwenda kurekebisha upande wa mabeki wamejisahau sana," amesema Samson.
Kundi D ambalo mechi zake zinachezwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza lina timu saba ambazo ni Rock Solution (Mwanza), Bweri (Mara), Mambali (Tabora), Leo Tena (Kagera), Kandahari (Kigoma), Bukombe Kombaini (Geita) na Friends Rangers (Dar es Salaam).
Mechi za kundi hilo zitaendelea kesho Machi 9, 2024 ambapo saa 2:00 asubuhi Kandahari itamenyana na Mambali Ushirikiano huku saa 10:00 jioni Leo Tena wakichuana na Bukombe Kombaini.