Rais Samia aongeze dau Simba, Yanga kufuzu nusu fainali CAF
Muktasari:
- Simba inacheza mchezo wa marudiano leo dhidi ya Wydad Casablanca nchini Morocco wakati Yanga itacheza mchezo wa marudiano siku ya Jumapili dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza hamasa kwa timu za Simba na Yanga zinazoshiriki mashindano ya CAF akiongeza dau kwa kila bao litakalofungwa katika mechi zao za marudiano kutoka Sh5 milioni hadi Sh10 milioni.
Mabao yatakayolipwa ni yale yatakalofungwa ndani ya dakika 90 au 120 za mchezo na sio yatakayopatina kwenye mikwaju ya penalti baada ya mchezo kuisha ili kumpata mshindi.
Simba inacheza mchezo wa marudiano leo dhidi ya Wydad AC katika Uwanja wa Mohamed V nchini Morocco mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Yanga itacheza mchezo wa marudiano siku ya Jumapili dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwenye Kombe la Shirikisho.
Simba inacheza mchezo wa marudiano ikiwa na mtaji wa ushindi wa 1-0 ilioupata katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati Yanga itacheza mchezo wa marudiano ikiwa na mtaji wa ushindi wa 2-0 ilioupata ugenini huko Nigeria.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema “Rais Samia Suluhu Hassan anazitakia kila la kheri Simba na Yanga na amewataka wachezaji kujituma uwanjani na kutumia maarifa yao yote kuhakikisha wanashinda michezo ya kukamilisha robo fainali ili wafanikiwe kuingia nusu fainali ambapo kila goli litakuwa Sh10 milioni.”