Queretaro kutamrejeshea makali Enekia?
Muktasari:
- Uhamisho huo umefanyika baada ya kumalizika kwa mkataba wake na FC Juárez Femenil, klabu ambayo hakuwa na msimu mzuri kama ambavyo wengi walitarajia kutokana na kiwango kikubwa alichowahi kuonyesha.
WIKIENDI iliyopita zilienea taarifa kuhusu uhamisho wa kiungo mshambuliaji Enekia Lunyamila ambaye alitimkia Querétaro FC Femenil ya Mexico akitokea FC Juarez ya nchini humo pia.
Uhamisho huo umefanyika baada ya kumalizika kwa mkataba wake na FC Juárez Femenil, klabu ambayo hakuwa na msimu mzuri kama ambavyo wengi walitarajia kutokana na kiwango kikubwa alichowahi kuonyesha.
Sasa je kusajiliwa Querétaro FC kunaweza kumrejesha kwenye makali ya kupachika mabao kiungo huyo ambaye ndani ya misimu miwili hakuwa na msimu mzuri.
Akiwa Juarez, Enekia alicheza mechi 11 na kufunga bao moja
Lakini wanamfahamu vizuri uwezo wa kiungo mshambuliaji huyo wanaamini kuwa uwezo wake haujapotea, bali amekuwa akipitia kipindi cha mabadiliko na ushindani mkubwa katika moja ya ligi zenye ushindani mkali kwa soka la wanawake barani Amerika Kaskazini.
Kilichomfanya Enekia kuwa mmoja wa viungo bora wanaofanya vizuri ni rekodi zake za mabao tangu alipokuwa akiitumikia Alliance FC mwaka 2016. Katika mechi 23 pekee alifunga mabao 37, takwimu zilizomuweka kwenye ramani ya soka la wanawake nchini.
Baadaye alihamia Ruvuma Queens ambako aliendelea kuonyesha uwezo wake wa kufunga kwa kupachika mabao 27 katika mechi 34 kabla ya kuhamia Morocco mwaka 2021 kujiunga na AUSF Assa-Zag.
Akiwa Assa Zag Enekia alikuwa na misimu bora zaidi katika maisha yake ya soka baada ya kufunga mabao 49 katika mechi 41, rekodi iliyomfanya kuonekana kama mmoja wa viungo hatari zaidi kutoka Afrika Mashariki.
Kiwango hicho kilimfungulia milango ya kucheza katika mazingira tofauti ikiwemo Ukraine na baadaye Mashariki ya Kati kabla ya kutua Mexico mwaka 2024.
Akiwa Mazatlán FC, Enekia aliendelea kuonyesha kiwango bora kwa kufunga mabao nane katika mechi 29, jambo lililomfungulia mlango wa kuhamia Juárez. Hata hivyo, mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa na sasa ametimkia Querétaro FC Femenil.
Swali ni kama Querétaro itakuwa sehemu ya kurejesha makali ya mshambuliaji huyo.Kwa upande mmoja, umri wake, uzoefu wa kimataifa na historia ya kufunga mabao vinaonyesha bado ana nafasi ya kuonyesha kiwango chake, upande mwingine anahitaji kuonyesha haraka kuwa bado ana uwezo wa kufanya tofauti katika ligi ambayo ushindani wake unaongezeka kila msimu.