Polisi, Yanga ngoma ngumu

Arusha. Dakika 45 za kipindi cha kwanza mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Polisi Tanzania dhidi ya Yanga zimekamilika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha timu hizo zikifungana 1-1.
Mpira ulianza kwa kasi huku kila timu ikishambulia lango la mpinzani wake kwa zamu ambapo ilishuudiwa dakika ya kwanza tu Yanga ikishindwa kupata bao baada ya Fiston Mayele kushindwa kuunganisha krosi ya Dickson Ambundo.
Yanga waliendelea kukosa nafasi nyingi za wazi kupitia mshambuliaji wake Fiston Mayele ambaye licha ya kufunga lakini alijikuta akishindwa kuanza kufungua akaunti yake ya mabao mapema.
Dakika ya Tisa tu ya mchezo Mayele alikosa mkwaju wa penati baada ya Jesus Moloko kuangushwa katika eneo la hatari na mchezaji wa Polisi Tanzania Shaban Stambuli ambapo mlinda lango wa Polisi Kelvin Igenderezi aliucheza Mpira wake.
Licha ya kushambuliwa kwa kiasi kikubwa lakini Polisi Tanzania FC waliweza kuwashangaza Yanga kwa kufunga bao dakika ya 34 kupitia Salum Kipemba ambaye alipiga shuti iliyomshinda mlinda lango wa Yanga Dgui Diara.
Yanga walisimama na kusawazisha dakika ya 41 kupitia Fiston Mayele ambaye aliunganisha Mpira uliokuwa unazagaa langoni mwa Polisi Tanzania baada ya mlinda lango Kelvin Igenderezi kuokoa mpira wa kichwa iliyopigwa na Mwamnyeto ambaye aliunganisha kona ya Shaban Djuma.