Platinum hofu tupu
Muktasari:
Simba inaihitaji ushindi wa tofauti ya zaidi ya bao moja dhidi ya Platnum, kesho, ili kutinga hatua ya makundi.
Dar es Salaam. Simba wamewasisitiza mashabiki wao kumwagika kwa wingi kesho kwenye Uwanja wa Mkapa, lakini kipa na nahodha wa FC Platinum, Petros Mhari amesema wataongeza umakini maradufu kwavile wanakumbuka dhahama waliyopata kutoka kwa Yanga.
Alisisitiza kwamba kamwe hawawezi kurudia makosa kama ya kipindi cha pili waliyofanya dhidi ya Yanga mwaka 2015 kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kujikuta wakiloa mvua ya mabao.
Katika msimu huo ambao FC Platinum walitolewa na Yanga walishindwa kumudu mchezo kipindi cha pili kutoka na hali ya hewa ya joto ambayo walikuwa hawajaizoea kwa kuchelewa kuwasili Dar es Salaam. Yanga ilishinda mabao 5-1 nyumbani na kufungwa bao 1-0 ugenini. Platinum ambao waliishinda Simba kwao bao 1-0, tayari wapo Dar es Salaam tangu Jumamosi.
Kipa huyo alisema jana kwamba walijifunza sana kutokana na makosa yale na hayatajirudia kwenye mechi na Simba kesho na hata mazoezini mpaka kambini wamekuwa wakikumbushana hilo lisijirudie.
“Tumeambiwa mpaka mazoezini kwamba tunapaswa kupambana mwanzo mwisho, vipindi vyote viwili ili tusirudie yale makosa yaliyotutoa,” alisema.
Simba inahitaji ushindi wa tofati ya mabao mawili ili kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo jana Ofisa Habari wao, Haji Manara alisema kwamba wamejipanga na wanataka ushindi wa kishindo ili kuweka rekodi nyingine ya kuvutia kwa masilahi ya soka la nchi.
Manara alisema hakuna mashindano yoyote haswa Simba wakitumia uwanja wao wa nyumbani na kama mashabiki wao wakajitokeza kwa wingi wakashindwa kupata matokeo mazuri.
Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck ameweka wazi kwamba morali ya wachezaji wake iko juu na wanaendelea kujinoa.
Mechi hiyo itaanza saa 11:00 jioni.