Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Phiri: Maximo kapata

Muktasari:

Mrwanda alisaini Yanga Jumatatu na kuanza mazoezi siku iliyofuata ambapo keshokutwa Jumamosi ataichezea timu hiyo katika mechi ya Nani Mtani Jembe huku usajili wake Yanga sasa ukileta hofu Simba.

SAA chache baada ya kutua katika kikosi cha Yanga, straika Danny Mrwanda amepewa jezi namba 24 iliyokuwa ikivaliwa na kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ lakini mwenyewe ameikataa na anataka apewe namba 33.

Kocha wa Simba, Patrick Phiri, aliposikia mchezaji huyo amesaini Jangwani akachanganyikiwa, lakini akafunguka ya moyoni.

Katika siku yake ya kwanza ya mazoezi na kikosi cha Yanga juzi Jumanne kwenye Uwanja wa Boko Veterani, Mrwanda alionekana amevaa jezi namba 24 na kuonyesha uwezo wake mbele ya Kocha Marcio Maximo.

Meneja wa Yanga mwenye mamlaka ya ugawaji wa jezi na namba za wachezaji, Hafidh Saleh, alisema amempa Mrwanda jezi hiyo iliyokuwa ikivaliwa na Chuji, lakini ameikataa na sasa anajipanga kumpa jezi nyingine namba 33.

“Nimempa Mrwanda jezi namba 24 ya Chuji ambayo haikuwa na mtu kwa sasa, lakini ameivaa kwa shingo upande na sasa haitaki anataka namba 33 ambayo tupo katika mchakato wa kumpatia,” alisema Hafidh.

Katika hatua nyingine, Mrwanda anaingizwa katika orodha ya wachezaji wapiga penalti wa Yanga akiwa na wenzake wanne ambao ni Oscar Joshua, Mrisho Ngassa, Simon Msuva na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Hata hivyo, kati ya wote hao Mrwanda ndiye aliyeonekana kufanya vizuri zaidi katika mipigo yake ya penalti hizo kuliko wenzake.

Phiri afunguka

Kocha wa Simba, Patrick Phiri, amesikitika kusikia Mrwanda ametua Yanga na kudai kuwa mabeki wake watakuwa na shughuli pevu ya kumkaba straika huyo kwenye pambano la Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga keshokutwa Jumamosi.

Mrwanda alikuwapo katika mipango ya kocha huyo na alimpendekeza kwenye ripoti yake aliyoipeleka kwa viongozi ambayo ilijadiliwa na kupitishwa, lakini viongozi wengi wa Simba walionekana kutomkubali Mrwanda na hivyo kuamua kuachana naye huku wakieleza kuwa walishindwa kumsajili kwa sababu alikuwa na mkataba na timu yake ya zamani, Polisi Moro.

Mrwanda alisaini Yanga Jumatatu na kuanza mazoezi siku iliyofuata ambapo keshokutwa Jumamosi ataichezea timu hiyo katika mechi ya Nani Mtani Jembe huku usajili wake Yanga sasa ukileta hofu Simba.

Phiri aliliambia Mwanaspoti: “Najua Mrwanda atacheza mechi ya Jumamosi, imenisikitisha sana kuona kwamba Yanga wamemchukua mchezaji ambaye nilimpendekeza, najua viongozi walikuwa katika hatua ya mwisho kumalizana naye iweje leo hii aende Yanga?

“Ni mchezaji ambaye atanisumbua sana Jumamosi na ninajua atatufunga, Mrwanda najua ni Simba, bado siamini kama amekwenda Yanga, nakikubali kiwango chake toka zamani kwani namfahamu uchezaji na ubora wake, natakiwa kujipanga zaidi.

“Kama tatizo lilikuwa ni fedha, bado viongozi wangefanya jitihada zozote zile za kuhakikisha wanampata ili mipango yangu itimie.”

Akizungumzia safu yake ya ulinzi ambapo Simba ipo katika mpango wa kumsajili beki kutoka Gor Mahia ya Kenya, David Owino, alisema:

“Nataka mchezaji wa kusajiliwa moja kwa moja na si wa majaribio, najua David akija ataisadia timu, kwani ni mzuri.”

Jana Jumatano asubuhi, mchezaji kutoka timu ya Victoria University FC, Juko Mushid, alitua visiwani Zanzibar kwa ajili ya majaribio ambapo Phiri alisema kuwa hawezi kumzungumzia zaidi kwani hana uhakika kama ana nafasi kwenye kikosi chake.

“Ndio kwanza ameingia leo (jana) asubuhi na ninafikiri amekuja kwa ajili ya majaribio tu na si kumsajili, hivyo ngoja tuone inakuwaje kwani hayumo kwenye mipango yangu kwa sasa,” alisema Phiri huku akiweka wazi kuwa timu yake itarudi Dar es Salaam kesho Ijumaa.