Pamba yajikwaa Championship

Wachezaji wa Mbeya Kwanza wakifurahia baada ya suluhu dhidi ya Pamba Jiji katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, leo. Picha na Damian Masyenene
Muktasari:
- Kama Pamba ingepata ushindi leo ingefikisha alama 50 na kukaa kileleni huku ikisubiri matokeo ya washindani wake, Biashara United na Ken Gold wanaomenyana kesho Jumamosi
Mwanza. PAMBA Jiji imejitibulia kwenye kampeni ya kupanda daraja baada ya leo kulazimishwa suluhu nyumbani huku ikiwapa nafasi washindani wake, Ken Gold na Biashara United kuongeza pengo la pointi katika vita ya kwenda Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo imelazimishwa suluhu na Mbeya Kwanza katika mchezo wa Ligi ya Championship ambao umepigwa Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.
Kama Pamba ingeshinda ingefikisha pointi 50 na kukaa kileleni huku ikiwasikilizia washindani wake Ken Gold walio na pointi 50 na Biashara United wenye alama 49 ambao watamenyana kesho Jumamosi. Mbeya Kwanza nayo imebaki kwenye nafasi ya nne na pointi zao 46.
Katika mchezo huo ambao ni wa pili timu hizo kukutana msimu huu umeshindwa kupatikana mbabe kwani mchezo wa kwanza uliopigwa Oktoba 27, 2023 katika Uwanja wa Nangwanda, Mtwara ulimalizika kwa sare ya 1-1.
Pamba haikuwa na mchezo mzuri ikitengeneza nafasi chache na kushindwa kuwa na ufanisi katika eneo la mwisho ikiibua kelele kwa mashabiki wake, huku ukuta wa Mbeya Kwanza ukiongozwa na kipa Rahim Sheikh aliyetokea Pamba Jiji katika dirisha dogo la Januari, mwaka huu, ukiwa imara kuokoa hatari nyingi.
Kipindi cha pili, dakika ya 50 Pamba imefanya mabadiliko ya mapema ya wachezaji wakiingia washambuliaji Mudathir Said, Rajesh Kotecha na kiungo Salum Kipemba kuchukua nafasi ya Peter Mwalyanzi, Jamal Mtegeta na Haruna Chanongo, huku Mbeya Kwanza wakiwapumzisha Arafat Adam, Ahmed Manzi na Evarigestus Mujwahuki na kuingia Geoffrey Upala, Abdulkarim Iddi na Mwani Thobias dakika ya 54 na 59.
Hata hivyo, dakika ya 90+3, Pamba imepata nafasi muhimu ya mkwaju wa penalti baada ya beki wake, Hassan Mwasapili kuangushwa eneo la hatari na mabeki wa Mbeya Kwanza, lakini mshambuliaji Issah Ngoah shuti lake likapaa juu ya lango na kuinyima timu yake ushindi.
Licha ya kukosa ushindi, Pamba imeendeleza rekodi safi ya kutopoteza mchezo katika Uwanja wa Nyamagana msimu huu tangu Septemba 11, 2023 ambapo imecheza mechi 10 na kushinda saba na sare tatu, huku mchezo pekee wa nyumbani iliopoteza ukiwa ni dhidi ya Biashara United (0-1) uliochezwa Mwadui Complex, Shinyanga.
Sare ya leo ni ya pili kwa Mbeya Kwanza ugenini kati ya mechi 10 ilizocheza, ikipoteza nne na kushinda nne, ikiwa ni timu ya tatu kushinda mechi nyingi msimu huu (14) sawa na Pamba Jiji, huku Ken Gold na Biashara United zikiongoza kwa kushinda mechi 15 kila mmoja.
Kipa wa Pamba, Shaban Kado amefikisha mchezo wa saba bila kuruhusu bao (cleensheet) tangu alipoanza kuidakia timu hiyo Novemba 9, mwaka jana, akifanya hivyo dhidi ya Polisi Tanzania (1-0), TMA (0-0), Mbuni (3-0), Cosmopolitan (1-0), Pan African (2-0), Copco FC (4-0) na Mbeya Kwanza (0-0), huku akiruhusu bao dhidi ya Ken Gold (2-1), FGA Talents (2-1) na Biashara United (1-0).