Pamba Jiji mambo freshi Championship

Kiungo wa Pamba Jiji, Ismail Ally akijaribu kuwapita wachezaji wa Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Championship leo Machi 9, 2024 katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza. Pamba imeshinda mabao 3-1.
Muktasari:
- Ushindi huo unaipeleka Pamba Jiji katika nafasi ya pili ikifikisha pointi 51 nyuma ya ken Gold yenye alama 53 huku wakiishuka Biashara United iliyo na pointi 50.
BAADA ya kuwakata stimu mashabiki katika mechi iliyopita ya Ligi ya Championship, mchana wa leo Pamba Jiji imerejesha furaha jijini Mwanza kwa kuinyoosha Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 na kupaa hadi nafasi ya pili ikiiacha Biashara United yenye pointi 50.
Pamba Jiji imepata ushindi huo kwenye mchezo wa raundi ya 24 wa ligi hiyo uliochezwa kuanzia saa 7:00 mchana kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa.
Matokeo hayo yanaifanya Pamba ifikishe pointi 51 ikichupa kwa nafasi moja kutoka ya tatu hadi ya pili ikifikisha pointi 51, moja zaidi na iliyonayo Biashara United ambayo ilibanwa na Mbeya City na kutoka sare ya 1-1 jana.
Ikiwa na hasira za suluhu katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya Kwanza katika Uwanja wake wa nyumbani, leo Pamba imekuwa na mchezo mzuri ikitengeneza nafasi nyingi za mabao na kuwahakikishia ushindi muhimu ambao unakoleza moto kwenye kampeni yake ya kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.
Winga wa timu hiyo, Ismaily Ally aliyekosekana mchezo uliopita, ameifungia Pamba bao la kwanza dakika ya 19 kwa mkwaju wa friikikii uliozama moja kwa moja nyavuni kabla ya nyota wa zamani wa Mtibwa Sugar na Simba, Haruna Chanongo kupiga chuma cha pili dakika ya 33 kwa shuti kali nje ya eneo la hatari.
Ruvu inayoburuza mkia, ilicharuka na kupata bao la kufutia machozi kupitia Kelvin Faru dakika ya 35 kwa shuti kali lililomshinda kipa, Shaban Kado.
Dakika mbili kabla ya mapumziko, kiungo, Michael Samamba 'Arteta' akaiandikia Pamba bao la tatu akimalizia krosi ya Issah Ngoah na kuipeleka timu yake mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Hata hivyo, Dakika ya 53 mshambuliaji wa Pamba, Mudathir Said aliyeingia kuchukua nafasi ya Issah Ngoah alikosa mkwaju wa penalti na kushindwa kuiandikia bao la nne timu hiyo baada ya kiungo, Salum Kipemba kudondoshwa katika eneo la hatari na mwamuzi kuiamuru pigo hilo.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Pamba kushindwa kufunga penalti kwenye Uwanja wa Nyamagana na wiki iliyopita, mshambuliaji Issah Ngoah alikosa pia mkwaju kama huo dakika ya 90 dhidi ya Mbeya Kwanza na kuinyima timu hiyo kutoka na alama tatu na kulazimishwa suluhu.
Kwa sasa Pamba Jiji imefikisha mchezo wa 11 msimu huu katika Uwanja wa Nyamagana jijini hapa bila kupoteza, ikishinda michezo minane na kutoka sare tatu.
Kwa kipigo hicho cha 3-1, Ruvu Shooting inaendelea kuwa timu iliyofungwa mabao mengi katika Ligi ya Championship msimu huu, ikiruhusu 46 na kufunga 13 katika mechi 24 ilizocheza, ikifuatiwa na Pan Africans (40) na Copco FC (39).
Pia timu hiyo iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita, inaendelea kushika mkia katika ligi hiyo ikikamata nafasi ya 16 ikiwa na pointi 11, ikishinda mechi mbili, sare tano na kupoteza 17, huku Pan Africans ikikamata nafasi ya 15 na alama zao 15 na Copco FC wanashika nafasi ya 14 na pointi zao 18.
Kiungo wa Ruvu, Kelvin Raphael amesema bado wana nafasi ya kupindua meza kwa kuweka mikakati mizuri ya ushindi kuanzia mchezo ujao ugenini mbele ya Biashara United ili wapate ushindi na kujinasua kutoka mkiani na wasishuke daraja.
"Bado tuna nafasi ya kuja na mipango mizuri kwa mchezo ujao dhidi ya Biashara United, tunapaswa kutulia na Wana Ruvu watuunge mkono tuje na mipango mizuri ya ushindi tutoke huku chini kwa sababu inawezekana," amesema kiungo huyo.