Pamba inaitaka Ligi Kuu, Chanongo atakata Kirumba

Muktasari:
- Baada ya ushindi huo Pamba inafikisha pointi 54, huku Ken Gold (56) na Biashara United (50) zikicheza kesho.
Mwanza. PAMBA Jiji imeendelea kuonyesha kweli inataka kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya jioni ya leo Ijumaa kuifumua Mbeya City kwa mabao 3-0 katika mechi ya Ligi ya Champioship, huku timu hiyo ikipata penalti mbili kwenye Uwanja wa Nyamagana.
Ushindi huo umeifanya Pamba kufikisha alama 54 na kujichimbia kwenye nafasi ya pili nyuma ya vinara, Ken Gold wenye pointi 56 huku Biashara United ikikamata nafasi ya tatu ana alama 50.
Katika mchezo wa leo winga, Haruna Chanongo ametakata kwa kuifungia Pamba mabao mawili dakika ya 17 kwa shuti kali na kumshinda kipa, Kelvin Mfuse, na lingine dakika ya 40 kwa mkwaju wa penalti ambao umepatikana baada ya beki wa Mbeya City, Jonathan Mwaibindi kunawa.
Mabao hayo mawili yanamfanya nyota huyo wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar kufikisha mabao tisa na kuwa kinara wa timu hiyo akifuatiwa na Mudathir Said mwenye mabao saba. Pia amefunga mfululizo baada ya mchezo uliopita kutupia moja kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting.
Bao la tatu nalo limefungwa kwa mkwaju wa penalti na beki, Salehe Ferouz dakika ya 70, ikiwa ni penalti ya pili kwenye mchezo, huku timu hiyo ikiendelea kunufaika na penalti katika michezo yake hususan ya nyumbani ambapo katika mechi 25 wamepata penalti zaidi ya 10.
Pia katika michezo mitatu mfululizo dhidi ya Mbeya Kwanza, Ruvu Shooting na Mbeya City, klabu ya Pamba imepata penalti nne, ambapo dhidi ya Mbeya Kwanza, Issah Ngoah alipaisha dakika ya 90, dhidi ya Ruvu Shooting, Haruna Chanongo alikosa na leo dhidi ya Mbeya City, Chanongo amefunga.
Huo ni ushindi wa 16 kwa Pamba msimu huu katika mechi 25 ilizocheza ikiongoza sawa na Ken Gold kwa kushinda mechi nyingi Championship, ikipata sare sita na kupoteza tatu, huku ikifunga mabao 40 na kuruhusu 13.
Rekodi ya kutopoteza Mechi kwenye Uwanja wa Nyamagana imeendelea kulindwa leo, ambapo timu hiyo imefikisha mchezo wa 11 bila kupoteza kwenye Uwanja huo ikishinda tisa na sare mbili, huku mchezo pekee wa nyumbani ambao imepoteza ni dhidi ya Biashara United (1-0) uliochezwa Mwadui Complex, Shinyanga.
Baada ya kichapo cha leo, Mbeya Kwanza imebaki na alama zake 38 katika nafasi ya saba ikishinda michezo 10, sare nane na kupoteza saba huku ikifunga mabao 30 na kuruhusu 27, huku Maulidi Shaban akiongoza kwa mabao katika kikosi hicho (13).
Kocha Msaidizi wa Pamba, Renatus Shija amesema kikosi chake kinaendelea kuimarika na kupunguza makosa katika eneo la ulinzi na ushambuliaji, huku akiwataka wachezaji kuendelea kuzingatia na kutimiza kile wanachoelekezwa mazoezini.