OKWIIIIIIIIIII!

Muktasari:
Straika huyo Mganda jana Jumatatu alifikisha bao la 16 la Ligi Kuu Bara msimu huu, akifunika idadi ya mabao ya Mfungaji Bora wa msimu uliopita yaliyofungwa na Simon Msuva na Abdulrahman Mussa ambao kila mmoja alitupia mabao 14 msimu huo.
KUNA Emmanuel Okwi mmoja tu. Okwi anayeichezea Simba ambaye ameendelea kuwanyamazisha mashabiki wote waliokuwa wakimponda kwa kumwita Mhenga.
Straika huyo Mganda jana Jumatatu alifikisha bao la 16 la Ligi Kuu Bara msimu huu, akifunika idadi ya mabao ya Mfungaji Bora wa msimu uliopita yaliyofungwa na Simon Msuva na Abdulrahman Mussa ambao kila mmoja alitupia mabao 14 msimu huo.
Okwi alifunga mabao mawili wakati Simba ikitakata kwa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mbao FC.
Rekodi zinaonyesha Mbao haijaifunga Simba katika mechi tano walizokutana katika mashindano yote.
Katika mechi nne za Ligi Kuu tangu msimu uliopita, Mbao imelala mara tatu na kupata sare moja huku ikipoteza katika Kombe la FA. Katika mechi hizo Simba imevuna jumla ya mabao 16 dhidi ya sita ya wapinzani wao waliopanda Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
MZAMIRU KATISHA
Simba ikicheza bila nahodha, John Bocco, iliikimbiza Mbao ya kocha, Etienne Ndayiragije na kufanya kosa kosa nyingi kabla ya kocha wa Simba, Pierre Lechantre, kumtoa kiungo Said Ndemla na kumwingiza Mzamiru Yassin katika dakika ya 31.
Kuingia kwa Mzamiru kuliifanya Simba kutawala mchezo na dakika ya 37, krosi ya Okwi ilitua miguuni mwa Shiza Kichuya aliyepiga shuti kali lililobadilishwa mwelekeo na beki David Mwasa na kumpoteza kipa Iyvan Rugumandiye na kujaa wavuni. Hapo hesabu, Moja.
Dakika chache baadaye Okwi alianza mambo alipopiga penalti iliyotokana na faulo aliyofanyiwa na Mwasa aliyeambulia kadi ya njano kwa kosa hilo. Okwi akapiga mwenyewe penalti hiyo, hapo hezabu, Mbili.
OKWI HAFAI
Kipindi cha pili kilianza kwa Mbao kuwatoa James Msuva na Ibrahim Njohole na kuwaingiza Rajesh Kotecha na Said Said, lakini Okwi aliyeisumbua Mbao iliyoongozwa na nahodha, Yusuf Ndikumbana aliwaliza tena dakika ya 70. Akiwa ndani ya sita alipokea pasi ya Mzamiru na kuachia kiki kali wavuni, hesabu Tatu.
Hapo ikabidi Ndayiragije kumtoa Emmanuel Mvuyekule na kumwingiza Ismail Ally ambaye hakuiokoa timu yake pale Taifa.
Dakika nane baada ya bao la tatu, Okwi alifanyiwa madhambi akielekea kumsalimu tena kipa wa Mbao, aliumizwa kiasi cha kushindwa kuendelea na mchezo, Laudit Mavugo akaingia badala yake.
Simba iliendelea kucheka na nyavu dakika ya 82 pale beki Erasto Nyoni, alipopiga mpira mrefu wa faulo baada ya Mzamiru kuchezewa vibaya na mpira huo kumbabatiza mgongoni Mwasa na kutinga wavuni, hesabu Nne.
Ubabe wa nahodha wa Mbao, Ndikumana ulimponza dakika ya 84 aliponyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu kwa kumchezea faulo Mavugo.
Wakati mashabiki wakiamini Simba imemaliza kazi, straika kutoka Ghana aliyecheza sambamba na Okwi katika mchezo huo, Nicholas Gyan naye akafanya mambo katika piga nikupige alipoukwamisha wavuni, hesabu Tano. Bao hilo la dakika ya 86 ni la kwanza kwa Gyan.
YANGA KAZI IPO
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha alama 45 na kuipa kazi Yanga ambayo kesho Jumatano itashuka mjini Mtwara kuvaana na Ndanda ili kupunguza pengo la pointi nane lililopo sasa.
Aidha Okwi amempa kazi straika wa Yanga, Obrey Chirwa mwenye mabao 11 kumfukuzia kwani sasa amezidiwa mabao matano.
MAKOCHA WANENA
Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma alisema vijana wake walicheza vema hasa baada ya kufanya mabadiliko kipindi cha kwanza na kupata mabao mawili ya haraka yaliyowachanganya Mbao aliodai anawaheshimu kwa soka lao la ushindani.
“Tulikuwa na nia ya dhati ya kushinda tukiwa nyumbani ili kuzidi kujiweka pazuri kwenye mbio za ubingwa na tunashukuru tumepata matokeo mazuri,” alisema Djuma, huku Nyoni akisema kazi ndio kwanza imeanza mpaka kieleweke.
Naye Kocha Msaidizi wa Mbao, Ahmad Ally, alisema walicheza na timu kubwa na kuadhibiwa kwa makosa yao na matokeo hayo yamewaumiza kwani hawakutarajia kukutana na kipigo kikubwa cha aina hiyo.
“Simba wamekuwa wakitusumbua kila tunapokutana nao na tumeona makosa yetu na tunaendelea kurekebisha ili tufanye vema kwa mechi nyingine zijazo,” alisema na beki kiraka wa Mbao, Boniface Maganga alisema wameumizwa na matokeo hayo.
SIMBA: Manula, Kapombe, Kotei, Mlipili, Nyoni, Kwasi, Mkude, Ndemla/ Mzamiru, Kichuya, Gyan, Okwi/Mavugo.
MBAO: Iyvan, Maganga, Amos, Mwasa, Ndikumana, Njohole, Said, Lukindo, Sangija, Kyombo, Msuva/Kotecha, Mvuyekule/ Ismail